AZIZA MASOUD NA EVANS MAGEGE
SAA chache baada ya Jeshi la Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuwaokoa madereva 12 wakiwamo wanane kutoka Tanzania waliotekwa nyara juzi na waasi wa Mai Mai katika eneo la Namoyo Jimbo la Kivu Kusini, MTANZANIA Jumamosi limedokezwa mbinu iliyotumika kuwanasua.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Simba Logistics, Azim Dewji ambaye ni mmoja wa wamiliki wa malori yaliyokuwa yakiendeshwa na madereva hao, amefichua siri iliyosaidia Jeshi la nchi hiyo (FARDC) kuwaokoa madereva hao bila kuwasababishia madhara.
Madereva hao waliookolewa ni pamoja na Hamdani Zarafi, Athuman Fadhili, Juma Zaulaya, Adam James, Issa Iddi Omari, Bakari Shomari, Hussein Mohamed na Mwamu Mbwana Twaha.
Katika mazungumzo yake na gazeti hili yaliyofanyika kwa njia ya simu jana akiwa nchini Kongo, Dewji alieleza jinsi mawasiliano yake na waasi hao yalivyotumika kung’amua eneo walipo na hivyo kulisaidia Jeshi kufika mahali walikokuwa wakiwashikilia.
Dewji alisema baada tu ya madereva wake hao kutekwa juzi alipigiwa simu na hata kuwa na mazungumzo ya mara kwa mara na Kiongozi wa waasi hao ambaye hakumtaja jina akitaka awalipe kiasi cha dola 4,000 kwa kila dereva.
Kwa mujibu wa Dewji, taarifa zote za mazungumzo kati yake na Kiongozi huyo wa waasi aliziwasilisha kwa watu wa usalama hapa nchini na Kongo.
Alisema kwa maagizo ya vyombo hivyo vya usalama ambavyo vilitaka kung’amua eneo la mawasiliano kwa njia ya kimtandao alifanikiwa kufanya mazungumzo na kiongozi huyo kwa muda mfupi huku lengo likiwa ni kukubaliana mahali watakapokutana kwa ajili ya kukabidhi fedha hizo.
“Serikali ya Kongo kupitia vyombo vya usalama waliniruhusu kuongea nao, niliongea na kiongozi huyo ambaye hakujitambulisha jina mara ya mwisho jana (juzi) saa 11:20 jioni, tulipanga jinsi ya kuonana ili niweze kukabidhi fedha wanazozihitaji,” alisema Dewji ambaye alilalamika kupata hasara ya shilingi bilioni 1.5 kutokana na kitendo cha waasi hao kuchoma malori yake sita.
Alisema kwa mujibu wa makubaliano yao ilikuwa wakutane jana asubuhi ili aweze kuwakabidhi fedha hizo na baadaye wawaachie madereva hao.
Wakati Dewji akisema hayo, usiku wa kuamkia jana Jeshi la Kongo lilitangaza kufanikiwa kuwaokoa madereva hao 12 kati yao wanane wakiwa Watanzania na wanne kutoka nchini Kenya.
Akizungumzia hasara aliyoipata Dewji, alisema pengine ingeweza kuzidi bilioni 1.5 endapo kama malori hayo yaliyokuwa yakirudi Dar es Salaam yangekuwa na mzigo.
Naye Msemaji wa Serikali DRC, Lambert Mende, akizungumza na MTANZANIA Jumamosi kwa njia ya simu kutoka Kongo alikiri kuokolewa kwa mateka hao wakiwa salama baada ya jeshi la nchi hiyo kufanya operesheni kali katika eneo la Kivu Kusini.
“Wote wamekutwa wakiwa salama baada ya jeshi letu kufanya msako katika eneo la Namoyo na vitongoji vya jirani. Hata hivyo, hawa wahalifu waliotekeleza tukio hili wamechoma moto malori sita,” alisema Mende.
Akifafanua hatari ya kundi la Mai Mai, Mende alisema kwamba kundi hilo halina nguvu wala hatari yoyote ya kutikisa amani ya nchi hiyo kwa sababu asilimia kubwa ya wapiganaji wake hawana silaha za kivita.
“Unaposema Mai Mai ujue kuna makundi madogo madogo mengi ambayo yametawanyika katika sehemu mbalimbali za Mashariki ya DRC, makundi haya hayana nguvu ya kijeshi kwa sababu FARDC limewanyang’anya silaha hivyo wengi wao wanatumia silaha za jadi kufanya ujambazi na uharamia huko vijijini,” alisema.
Kwa upande wa Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Jimbo la Maniema nchini Kongo, Saleh Zakuani, akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu mbali na kusema Mai Mai wanaotajwa kuhusika na utekaji huo ni majambazi, lakini alikiri Jeshi la nchi hiyo kuingilia kati.
“Wanajeshi wetu yameyapiga yamekimbia na sasa yanawafuatilia huko walikokimbilia,” alisema Zakuri.
Akizungumzia tukio hilo Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki hapa nchini, Mindi Kasiga, alisema madereva wote wanane wa Tanzania waliokolewa na Jeshi la Serikali ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC).
Katika maelezo yake, alisema baada ya tukio la kutekwa kwa madereva hao, FARDC lilifanya jitihada kubwa kwa kuendesha operesheni kabambe ya kijeshi katika eneo la Namoyo Jimbo la Kivu Kusini na kufanikiwa kuwaokoa madereva hao.
Alisema madereva wote wamekutwa katika afya njema na kwa taarifa ya uhakika waliyoipata kutoka Serikali ya DRC, hapakuwa na fedha yoyote iliyotolewa kama kutimiza masharti ya kuwaokoa.
“ Leo asubuhi (jana) tumepata taarifa kupitia Ubalozi wetu huko Kongo kuwa operesheni ya jeshi la nchi hiyo imekwenda vizuri kwa kufanikiwa kuwaokoa ndugu zetu, madereva wanane kutoka Tanzania pamoja na wale wa Kenya na jambo hili lilitokana na jitihada za mshikamano mkubwa tulio nao na wenzetu wa DRC ambao jeshi lao limepambana kuwakomboa watu wetu,” alisema Mindi.
Kutokana na muktadha wa tukio hilo, Mindi aliwashauri Watanzania hususani wafanyabiashara kuomba taarifa ya hali ya usalama kwa maeneo yenye matatizo ya kiusalama kama Mashariki ya Kongo hususani Kivu ya Kusini kabla ya kusafiri kwenda maeneo hayo.
Aidha, katika taarifa yake ya juzi Mindi alisema waasi hao waliwateka nyara madereva hao wa Tanzania pamoja na wale wa nchini Kenya na kutishia kuwaua mateka hao endapo hawatalipwa kiasi cha Dola za Marekani 4,000 kwa kila mmoja hadi kufikia jana.
Mindi alisema katika tukio hilo, madereva wawili wa Kitanzania walifanikiwa kutoroka na ndio waliosaidia kutoa taarifa kuhusu tukio hilo.
Alikaririwa akisema kwa taarifa zilizopatikana watekaji walikuwa ni kikundi cha waasi cha Mai Mai ambao baada ya kuyateka magari hayo, waliwashusha madereva na kuwapeleka porini na kisha kuteketeza kwa moto malori manne ambayo yote ni ya Dewji.
Kabla ya kukimbizwa waasi hao walikuwa wametoa saa 24 kuanzia juzi saa 10 jioni walipwe fedha hizo vinginevyo walikuwa tayari kuwaua.