MAMBO mawili yametulazimisha kwa mara nyingine kuandika kukumbusha umuhimu katika kuhakikisha suala la usalama barabarani.
Mambo hayo ni madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani, lakini pia askari wa usalama barabarani kuhakikisha usalama na si kutanguliza mbele ukusanyaji wa fedha.
Upo ushahidi mwingi unaoonyesha kwamba ajali nyingi zinazotokea barabarani, chanzo chake ni uzembe au sifa za kijinga zinazofanywa na baadhi ya madereva wawapo barabarani.
Ukitaka kuthibitisha hili, hebu jaribu kupita barabarani nyakati za usiku ambazo mara nyingi askari wa usalama barabarani  hawapo.
Nyakati hizo utashuhudia baadhi ya madereva wakiendesha magari yao ovyo na wengine kwa mwendo kasi pasipo kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Tunaamini madereva wenye tabia hizi si kwamba hawafahamu madhara ya kutozingatia sheria za usalama barabarani muda wote, bali ni sifa za kijinga na za kitoto.
Sisi tunaamini dereva mjanja ni yule anayeendesha gari kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani nyakati zote, bila kujali askari wa usalama barabarani wapo au hawapo.
Tunaamini dereva mjanja na mstaarabu ni yule anayefahamu madhara ya kutozingatia sheria za usalama barabarani.
Lakini pia kwa upande wa askari wa usalama barabarani, wapo baadhi ambao wanaonekana kufanya kibarua chao kama mradi wa kujipatia fedha.
Ipo mifano na ushahidi mwingi wa askari wa namna hii ambao unaweza ukadhani huenda wanafanya biashara au wafanyakazi wa mamlaka ya kukusanya mapato kutokana na namna walivyolipa kisogo suala zima la kuhakikisha usalama, huku wakionekana kutanguliza fedha mbele.
Kinachoudhi wengi ni tabia ya baadhi ya askari hao kuwabambikia baadhi ya madereva makosa na wakati mwingine kuwatoza fedha dereva pasipo kutumia busara.
Pamoja na kwamba sisi kwa upande wetu tunaamini kwamba kila mmoja wetu kwa nafasi yake ana jukumu la kuzuia ajali, lakini ajali zitakoma pale tu madereva na baadhi ya askari wa usalama barabarani watakapokubali kubadili mwenendo wao.
Tunaamini askari wa usalama barabarani wana eneo lao katika kuhakikisha suala zima la usalama.
Tunadhani sasa wakati umefika si tu kwa serikali kwa maana ya vikosi vya usalama barabarani kuhakikisha vinachukua hatua zinazopaswa au madereva kuchukua tahadhari za kujikinga na ajali za barabarani, lakini pia na mamlaka zinazohusika na miundombinu kuhakikisha pia zinaiboresha.
Hatuwezi tu tukabaki na msemo unaosema ajali haina kinga, lakini ukweli ni kwamba  yapo mambo mengine yaliyo chini ya uwezo wetu ambayo tunaweza kuyafanya kuepuka madhara makubwa yanayoweza kuzuilika.