Ruth Mnkeni na Asifiwe George, Dar es Salaam
MADEREVA wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka(UDART), jana waliendesha mgomo baridi kwa madai kwamba mshahara wanaolipwa ni mdogo na haukidhi mahitaji yao.
Mgomo huo ulidumu kwa saa mbili na MTANZANIA ilishuhudia abiria wengi wakiwa katika vituo mbalimbali kikiwamo cha Kimara Mwisho wakisubiri huduma hiyo.
Magari hayo yanatakiwa kuanza kutoa huduma saa 11.00 alfajiri ambako madereva wanakuwa wawili kwa kila gari na kila mmoja anatakiwa kufanya kazi kwa saa nane.
Akitoa ufafanuzi kuhusu mgomo huo, Mkurugenzi Mkuu wa Udart, David Mgwassa, alisema madereva 30 ambao hawajasaini mkataba ndiyo waliofanya mgomo na wengine 300 tayari wameshasaini mikataba yao na wanaendelea na shughuli kama kawaida.
Alisema madereva wanatakiwa kulipwa Sh 800,000 lakini mshahara huo umegawanyika mara mbili ambako kuna Sh 400,000 ambazo hulipwa kila mwezi na kiasi kingine cha Sh 400,000 hulipwa kwa kuangalia kutimizwa kwa vigezo vya masharti ya mkataba.
“Shilingi 400,000 ni kiwango kisichobadilika kwa mwezi lakini baada ya kupimwa vigezo sita ambavyo ni usafi, kuwahi kazini, kutopata ajali na kuwahi kwa wakati kutoka kituo kimoja hadi kingine ndiyo hulipwa Sh 400,000 nyingine,”lisema.