Na Mwandishi Wetu
Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imezindua madawati ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs)katika Sekta hiyo.
Akizindua madawati hayo Septemba 04, 2024 kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk. Dorothy Gwajima, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Jinsia, Felister Mdemu amesema ushirikiano huo utafanikisha malengo ya kuwa na taifa lenye maendeleo endelevu na wananchi wenye ustawi thabiti.
Felister amesema madawati hayo yatakuwa ni kiungo kati ya Sekta Binafsi, Serikali na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na kuwa mwanzo wa kufungua fursa mpya, kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa endelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wa miaka mitano.
“Madawati haya tunayozindua leo ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha tunaimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika kutekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kuboresha na kukwamua hali za maisha ya wananchi, maendeleo endelevu na ukuaji wa uchumi wa Taifa.” amesema Felister.
Amebainisha kuwa kanzi data ya usajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali hadi sasa inaonesha jumla ya Mashirika 9650 yamesajiliwa katika ngazi tofauti kuanzia kimataifa, kitaifa, mkoa na halmashauri na yamekuwa yakichagiza jitihada za Serikali katika kuleta maendeleo kwa wananchi kwa kutekeleza miradi ya afua mbalimbali hususani Afya.
Akizungumza katika majadiliano hayo, Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Vickness Mayao amesema kuna fursa nyingi za ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi kwa manufaa ya jamii hasa kupitia uanagenzi kwenye Vyuo vya Maendeleo ya Jamii.
Kwa upande wake mmoja wa wadau, Mwakilishi wa Shirika la World Vision Tanzania Dk. Joseph Mayala, amesema ni wakati muafaka wa ushirikiano kati ya Sekta binafsi na Serikali ns kuomba kiundwe Kikosi kazi ili kushiriki mjadala wa Sera ya Taifa ya Maendeleo unaoendelea pamoja na kuwa na mkakati endelevu wa mashirikiano.