26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Madawati ya ulinzi na usalama wa mtoto shuleni, mwarobaini matukio ya ukatili

Na Derick Milton, Simiyu

Taasisi isiyokuwa ya kiserikali Mass Media ya Mjini Bariadi mkoani Simiyu, imekuwa ya kwanza mkoani humo kuanza kuunga mkono juhudi za Serikali za uanzishwaji na uundwaji wa madawati ya ulinzi na usalama wa mtoto shuleni.

Madawati hayo ni moja ya mkakati uliopo kwenye Mpango wa Taiifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWA), ambapo Mass Media imesaidia kuanzishwa kwa madawati 13 katika shule za msingi wilayani Busega na Bariadi mkoani Simiyu.

Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu Adolf Temba akitoa mafunzo kwa wanafunzi Shule za Msingi, jinsi ya Kupambana na vitendo vya ukatili kwa watoto.

Kupitia mradi wake wa Kampeini ya kuimarisha usawa wa kijinsia Mkoa wa Simiyu, Mass Media inatekeleza mradi huo kwa awamu ya pili chini ya ufadhili wa The Foundation For Civil Sociaty, ambapo uundwaji wa Madawati hayo unatajwa kuwa mwarobaini wa matukio ya ukatili hasa kwa watoto.

Mratibu wa Mradi kutoka Mass Media, Frank Kasamwa akizungumza na Mtanzania Digital Julai 20, amesema kuwa mbali na kuunda madawati hayo ambayo wameshilikiana na Maafisa wa ustawi wa Jamii wa halmashauri, wajumbe wa kwenye madawati hayo wakiwemo walimu wakuu, wanafunzi na walimu wa malezi shuleni wamepewa mafunzo.

“Maafisa Ustawi wa Jamii wamewafundisha wahusika wote, aina ya vitendo vya ukatili, jinsi ya kuepuka lakini na wapi wanaweza kuripoti matukio hayo ikiwa yatajitokeza kwenye jamii zao, nyumbani au shuleni, walimu wa malezi wao pia wamefundishwa mbinu za kumtambua mtoto aliyefanyiwa vitendo vya ukatili” amesema Kasamwa.

Mratibu huyo amesema katika mafunzo hayo wanafunzi na walimu wamesisitizwa zaidi kutokukaa kimya dhidi ya vitendo vya ukatili, kwani kukaa kimya itasababisha vitendo kuendelea kushamili na kuadhiri ndoto na matamanio ya watoto.

Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi,
Eliza Mbena, akitoa mafunzo kwa wanafunzi na walimu shule za msingi Sapiwi ‘A’, Masewa ‘A’, ‘B’ na ‘C’ amewasisitiza walimu kuwa na usiri pindi wanapopata taraifa za mtoto kufanya kitendo chochote cha ukatili.

Mbena ameongeza kuwa katika kushughulikia matukio ya ukatili hasa kwa mtoto, mwalimu au mlezi lazima azingatie usiri, ili kuweza kufanikisha uchukuliwaji wa hatua za kisheria kwa mtu au watu waliomfanyia kitendo hicho mtoto.

Aidha, Mbena amesema kuwa mabaraza ya wanafunzi shuleni nayo ni sana kwani wanafunzi wamekuwa wakitumia njia hiyo kutoa maoni, kuwasilisha malalamiko yao lakini pia kujadiliana na kupewa elimu ya jinsi ya Kupambana na matukio ya ukatili.

Mwalimu wa Malezi Shule ya Msingi Sapiwi ‘A’, George Mtebe amesema kuundwa kwa madawati hayo pamoja na kupewa mafunzo hasa wanafunzi itasaidia kwa kiwango kikubwa kukomeshwa kwa matukio ya ukatili kwa watoto.

Amesema kuwa katika mafunzo hayo, kila kitu ambacho wanafunzi wameelezwa na kufundishwa hicho tayari wamekishika na kamwe hakitatoka kwenye akiri zao, kama ni kibaya basi watakuwa makini na watatoa taarifa mapema kwa wahusika.

“Hapa tunaweza kukomesha kabisa ukatili, Mass Media wamefanya jambo kubwa sana kuwapa elimu hawa watoto, kila ambacho wamefundishwa hakitatoka kwenye vichwa vyao, na hapo itakuwa rahisi kuripoti tukio lolote ambalo wataliona au kuambiwa la ukatiri,” amesema Mtebe.

Naye Magori Ayubu Mwalimu Shule ya Msingi Masewa ‘C’ anasema kuwa baada ya mafunzo hayo na kuundwa kwa Madawati hayo, sasa Utakuwa wakati wa wanafunzi hao kwenda kuwafundisha wenzao shuleni.

“Shuleni tumekuwa na vipindi vya kutoa elimu mbalimbali hasa kwenye muda wa ziada siku za Ijumaa kila wiki, sasa kupitia vipindi hivyo, Hawa ambao wamepata elimu watakwenda kuwafundisha wenzao leo elimu hii iweze kuenea Shule nzima,” amesema Ayubu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles