23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Madaktari  wasimamishwakazi kwa kutoa lugha chafu

doctorNA NORA DAMIAN, DAR ES SALAAM

UONGOZI wa Hospitali ya Rufaa ya Amana, Dar es Salaam,  umewasimamisha kazi madaktari wawili na muuguzi mmoja wakidaiwa kutoa lugha chafu kwa wagonjwa.

Hatua hiyo inatokana na malalamiko   kutoka kwa wagonjwa wakilalamikia utoaji huduma katika hospitali hiyo.

Matukio ya hivi karibuni kuhusu hospitali hiyo ni yale yaliyotokea Machi 23, 30, na Aprili 29 mwaka huu.

Tukio la Machi 23 ni la Asha Sudi (17) aliyejifungulia chooni wakati la Machi 30 linahusu kifo cha mtoto na Aprili 29 ni la mwendesha bodaboda, Nassor Hamis aliyekufa akipatiwa huduma hospitalini hapo.

Akizungumza hospitalini hapo jana, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Meshack Shimwela, alisema licha ya kusimamishwa kazi, watumishi hao pia wameshtakiwa katika mabaraza yao ya taaluma.

“Tumefanya uchunguzi wa awali na sasa tunaendelea kufanya uchunguzi wa kina.

“Kama tutaona kuna upungufu wa wauguzi au madaktari kuna mabaraza ambayo yako kisheria na kama kuna mapendekezo kwa mkurugenzi yatatolewa,” alisema Dk. Shimwela.

Dk. Shimwela alisema mwendesha bodaboda Nassor hakufa kwa uzembe kama inavyodaiwa bali alichelewa kufika hospitalini hatua iliyosababisha kupoteza damu nyingi njiani.

“Inasemekana alipigwa risasi saa 4.00 na alifika hospitali saa 6:30 usiku, risasi alipigwa katika mshipa mkubwa wa damu.

“Walimfunga na kumpakia kwenye bodaboda miguu ikiwa inaning’inia hivyo damu iliendelea kupotea,” alisema.

Mganga huyo alisema hivi sasa majeraha yanayotokana na silaha ni mengi na kushauri kuwa kuna haja ya jamii kupewa elimu ya awali kwa sababu jeraha la risasi ni tofauti na jeraha jingine, kama la kupigwa na panga.

Dk. Shimwela alishauri watu wanapopata matatizo kwenda katika vituo vya kutolea huduma vilivyoko karibu na maeneo yao badala ya kukimbilia hospitalini.

Alisema  kesi nyingi wanazopokea ni za kawaida ambazo zingeweza kudhibitiwa katika vituo vya pembezoni.

“Kama yule binti aliyejifungulia chooni ana miaka 17 tu halafu ni uzazi wake wa kwanza.

“Kwa hali ya kawaida huyu hafahamu chochote na alipoambiwa aende akabadilishe nguo ndipo alipojifungua ghafla…hakuwa na shida kubwa kumlazimu kuja kwetu na pengine angechelewa angeweza hata kuzalia kwenye daladala,” alisema.

Kaimu Ofisa Uhusiano wa Manispaa ya Ilala, Davi Langa, alisema malalamiko mengi yanaweza kutatuliwa ndani ya uongozi wa hospitali au ngazi ya halmashauri kama wagonjwa watafuata utaratibu unaotakiwa kuyawasilisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles