24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Madaktari waeleza ugonjwa wa Mbowe

Pg 1NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kushindwa kuhitimisha maandamano ya kumsindikiza mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia chama chao kuchukua fomu ya kuwania urais baada ya kuugua ghafla, madaktari wameweka wazi kinachomsibu huku yeye akisema anaendelea vizuri.
Jana, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Tilizo Sanga, alisema Mbowe anasumbuliwa na maradhi ya Exhaustion ambayo kitaalamu yanajulikana kama Fatigue. Dk. Sanga ambaye ni mmoja wa madaktari bingwa wanane wa kitengo cha moyo kwenye hospitali hiyo wanaomuhudumia Mbowe,
alisema ugonjwa huo unatokana na kutokulala muda mrefu na kutokula.
“Mbowe alipokewa jana (juzi) baada ya kupewa rufaa akitokea katika Hospitali ya TMJ Mikocheni, na alipofika alipokewa akiwa anajisikia vibaya, hivyo alianza kufanyiwa uchunguzi na jopo la madaktari bingwa wanne wa moyo na baada ya kumaliza walimtaka apumzike hospitalini hapo kwa saa 48,” alisema Dk. Sanga.
Alisema baada ya madaktari hao kumpokea juzi na kumuhudumia, jana waliongezeka madakatari wengine wanne na kuendelea kumuhudumia kiongozi huyo. Dk. Sanga alielezea chanzo cha maradhi hayo kuwa kinatokana na uchovu unaochangiwa na mtu kufanya kazi kwa muda mrefu bila mapumziko hali inayosababisha kuishiwa nguvu na kupungukiwa maji mwilini kutokana na kula chakula kidogo.
Kwa upande wake, Mbowe alisema: “Nililazimika kufika hospitali ili kupata ‘medical attention’ baada ya kukabiliwa na kizunguzungu kikubwa, na nilipofika timu ya madaktari ilinitaka kupumzika kwa saa 48, nikisubiri majibu yaliyobainisha kwamba nilikuwa nasumbuliwa na tatizo la Exhaustion.
“Matatizo hayo yametokana na kufanya kazi kwa muda mrefu usiku na mchana, kwa kweli mwili wa binadamu una kipimo cha mwisho cha kuchukua adhabu kama hiyo. Hali ya mambo inayoendelea nchini humu ilichangia kunilazimisha kuji-overwork kwa kufanya kazi kwa muda wa saa 24 bila kupumzika,” alisema.
Mbowe alisema jambo analosubiri ni kumalizika kwa mapumziko ya muda aliopewa wa saa 48, lakini kutokana na kutaka kuondoa sintofahamu ya wananchi katika kujua afya yake, amechukua jukumu la kuzungumza na vyombo
vya habari na kuwaeleza kwamba afya yake inaendelea kuimarika.
“Napenda kuwahakikishiaWatanzania na waandishi wa habari kwamba niko salama na kwa kupitia kwenu Watanzania wataelewa niko salama na kuwatoa hofu iliyojitokeza kuhusu afya yangu, na nawashukuru sana wale wote waliokuja kunijulia hali na niwaombe radhi wale wanaonyimwa kuniona kwa sababu za kitabibu kwa sababu ninatakiwa kupatiwa ‘full rest’.
“Natambua suala la kuzungumza nanyi si sehemu ya ‘full rest’ ila nimeona nivunje masharti ili niuhabarishe umma kwa kupitia ninyi ili umma upate maendeleo ya afya yangu ambayo ni sahihi,” alisema.
Mbowe aliripotiwa kupatwa na tatizo hilo juzi alipokuwa kwenye maandamano ya kumsindikiza mgombea urais wa Ukawa, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa wakati wa kuchukua fomu ya uteuzi ofisi za Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC). Ukawa inaundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.

MBATIA
Naye Mwenyekiti wa Chama cha NCCR- Mageuzi, James Mbatia, akizungumza hospitalini hapo, aliwaomba Watanzania kumwombea dua na sala Mbowe na viongozi wa Ukawa ili waweze kuvuka salama katika kuhakikisha mama Tanzania inapata mabadiliko.
Mbatia alitoa shukrani kwa jopo la madaktari wanane waliomuhudumia Mbowe hadi anapata nafuu tangu alipofika Muhimbili juzi ambapo walionyesha moyo wa ukarimu kwa kuwapokea vizuri. “Maradhi haya si ya kwanza
kumpata Mbowe, bali yamekuwa yakiwapata watu wengine, ila tunachoomba ni Mwenyezi Mungu amwezeshe kupona na kurejea katika mapambano ambayo yanaendelea,” alisema.

VIONGOZI WENGINE
Baadhi ya viongozi waliofika kumjulia hali ni Lowassa, Mbatia, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, Mgombea mwenza wa Ukawa, Juma Duni Haji, Mbunge wa Arumeru
Mashariki, Joshua Nassari, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Naibu Katibu Mkuu Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles