25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Madaktari vijana wadaiwa kutongoza wagonjwa

 Nathael Limu- Sindiga

CHAMA Cha Mapinduzi Mkoa wa Singida, kimeibua tuhuma nzito kwa madaktari wa Hospitali ya Rufaa mkoani hapa, ikiwamo madai ya madaktari vijana kuwatongoza wagonjwa wasichana na wanawake, wanaofika hospitalini hapo kupata huduma ya tiba.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mjumbe wa Kamati ya Siasa CCM Mkoa wa Singida, Martin Lissu, alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa pamoja kati ya kamati ya siasa mkoa na viongozi wa hospitali hiyo. Alisema amepokea malalamiko mara kwa mara hasa kutoka kwa wasichana kwamba wanapoingia kwenye chumba cha daktari kijana, baadhi yao hutumia fursa hiyo kutongoza.

“Mbaya zaidi, baadhi yao huwa wanawambakizia magonjwa ambayo hawana. Lengo aweze kufanikisha lengo lake ovu la matamanio ya ngono.

“Aidha wanapoteza muda mwingi na kusababisha wagonjwa wengine kuchelewa kupata huduma. Vitendo hivyo vinasababisha baadhi ya wasichana kuikimbia hospitali, jamani tunakwenda wapi,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu CCM Mkoa wa Singida, Alexandrina Katabi, alisema kuwa inafika wakati hata wagonjwa wanapofika hospitalini hapo huambiwa hakuna dawa hali ya kuwa zipo.

“Dosari zipo nyingi, tunazoziona na tunazozishuhudia. Mfano hai ni kwamba kuna kipindi tulikuwa na maiti mochwari ya hapa, ilitulazimu kuchukua saa zaidi ya 12, kuipata.

“Mhudumu wa mochwari alitafutwa kwa simu na akafuatwa nyumbani, hakupatikana, ila alikuwa Ilongero. Kwa ujumla uongozi wa hapa unapaswa kusimama imara kuhakikisha wafanyakazi wa ngazi zote, wanabadilika haraka, vinginevyo hatua stahiki zitachukuliwa,” alisema Katabi.

Mmoja wa wajumbe wa bodi ya hospitali hiyo, Diana Chilolo, alisema kero zinazolalamikiwa nyingi wamezisikia, ambapo aliahidi bodi yao itafanyia kazi dosari hizo kwa wakati.

Alisema wao wanataka kuona hospitali hiyo inafanya kazi iliyotarajiwa na Serikali ya kutoa huduma kwa ubora kwa watu wote kwa mujibu wa sheria na pindi linapojitokeza jambo ni wajibu wao kukaa na kufuatilia na kisha kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.

Naye Katibu Mwenezi wa Mkoa, Ahmed Athumani aliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama ya kuangalia uwezekano wa daktari bingwa ambapo kwa sasa ni Sh 15,000 hadi 20,000.

Alidai kiwango hicho ni kikubwa na wananchi wengi hawana uwezo wa kumudu gharama hizo kutokana na tofauti ya kipato.

Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Juma Kilimba, alisema kuwa kwa mujibu wa ibara ya 189 ya Ilani ya uchaguzi, wanawajibika kukagua utekelezaji wa ilani hiyo ya uchaguzi kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya afya.

“Utekelezaji huu ni pamoja na kuona kama mnatoa huduma stahiki. Tuna uhakika serikali imetoa fedha kutosha kununulia vifaa tiba na madawa, kilichosalia ni ninyi kuwatendea wananchi haki wananchi,” alisema. 

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,522FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles