27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Madaktari, manesi, walimu wachuana mishahara

kairukiNa RACHEL MRISHO, DODOMA

SERIKALI imesema wafanyakazi wa sekta ya afya ndio wanaopokea viwango vikubwa vya mishahara wakifuatiwa na wale wa sekta ya elimu nchini.

Taarifa hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angela Kairuki, alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Zubeda Sakuru (Chadema).

Katika swali lake, Sakuru alitaka kujua Serikali inakabiliana vipi na changamoto za masilahi kwa watumishi katika sekta ya afya.

Sakuru alisema kuna matukio ya vifo visivyo vya lazima vinavyotokana na ukosefu wa motisha kwa madaktari na wauguzi, ambao wanalipwa viwango vidogo vya mishahara na hawalipwi posho zao kwa wakati.

Akijibu swali hilo, Kairuki alisema Serikali imeendelea na jitihada za kuboresha mishahara ya watumishi wake, ikiwamo wataalamu wa sekta ya afya kwa kuzingatia uwezo wa kifedha.

Alisema kwamba mishahara huzingatia ngazi ya elimu, ambapo ngazi ya astashahada kwa upande wa Serikali Kuu ni Sh 390,000, kada ya walimu Sh 419,000, wauguzi Sh 432,000 na madaktari ni Sh 432,000.

Kwa upande wa stashahada, Serikali Kuu ni Sh 525,000, walimu 530,000 wauguzi 680,000 na madaktari ni Sh 680,000.

Kairuki alisema ngazi ya shahada kwa upande wa Serikali Kuu ni Sh 710,000, walimu 716,000, wauguzi 980,000 na madaktari ni Sh 1,480,000.

Pamoja na hayo, alisema Serikali inaendelea na utafiti wa tathmini ya kazi na itakapokamilika, itapanga upya mishahara na motisha kwa watumishi wote wa umma ikiwamo sekta hiyo.

“Kati ya mwaka 2010/11 hadi mwaka 2016/17, vianzia vya mishahara kwa kada za wauguzi vimeongezeka kutoka shilingi 614,000 hadi 980,000 kwa mwezi kwa wahitimu wa shahada.

“Vimeongezeka pia kutoka shilingi 425,000 hadi shilingi 680,000 kwa wahitimu wa stashahada na shilingi 260,000 hadi shilingi 432,000 kwa wahitimu wa astashahada.

“Kwa kada ya madaktari na maofisa tabibu katika kipindi hicho, vimeongezeka kutoka shilingi 886,800 hadi shilingi 1,480,000 kwa wahitimu wa shahada na shilingi 425,000 hadi shilingi 680,000 kwa wahitimu wa stashahada na shilingi 260,000 hadi shilingi 432,000 kwa wahitimu wa astashahada.

“Pamoja na hayo, Serikali itaendelea kuboresha masilahi ya waatumishi kadiri uwezo wake wa kulipa utakavyoimarika,” alisema Kairuki.

Wakati huo huo, Serikali imewaagiza waajiri wote nchini kuhakikisha wanatenga fedha za uhamisho na za marekebisho ya mishahara kabla ya hatua yoyote kufanyika.

Agizo hilo lilitolewa bungeni jana na Waziri Kairuki wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Singida Mjini, Mussa Sima (CCM), aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kupandisha mishahara ya watumishi wa umma kwa kuwa kila mwaka inapofika Julai, hupandisha vyeo na mishahara kwa watumishi wa umma.

Awali katika swali la msingi, mbunge huyo aliuliza Serikali ina mpango gani wa kuyalipa madeni ya watumishi wa umma, vilevile alihoji mkakati wake wa kuhakikisha haina madeni tena.

Katika majibu hayo, Kairuki hakulitolea ufafanuzi swali la nyongeza, badala yake alijielekeza katika kujibu madeni ya watumishi wa umma.

Alisema ni kweli kulikuwa na malimbikizo, lakini tangu kuanzishwa kwa mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara, malimbikizo yamepungua.

Kairuki alisema ili kukabilina na changamoto ya malimbikizo ya madeni, ni vema waajiri wazingatie sheria na kanuni kwa kuhakikisha wanalipa fedha kwa wakati, zikiwamo za matibabu na posho, ambazo zimekuwa zikilalamikiwa.

“Serikali inatoa wito kwamba mtumishi yeyote asihamishwe kama hakuna fedha za uhamisho, pia na za marekebisho ya mishahara. Mambo haya yafanywe pale fedha zinapokuwapo,” alisema Kairuki

Sambamba na hilo, waziri huyo alieleza kwamba nafasi za kukaimu lazima zitolewe taarifa ili mtumishi anayekaimu nafasi husika aweze kulipwa stahiki yake kwa wakati.

Akizungumzia mpango wa Serikali wa kukabiliana na mlundikano wa madeni ya watumishi, Kairuki alieleza kuwa inaendelea kupokea na kuhakiki madai ya watumishi wa umma yanayohusu mishahara na kuyalipa kwa kadiri ya uwezo wake wa kifedha.

“Katika mwaka wa fedha 2014/2015 Serikali ililipa madai ya malimbikizo ya mshahara ya shilingi 55,293,372,627.37 ambayo yalilipwa kwa watumishi 55,688 waliokuwa na madai yaliyotokana na kupandishwa vyeo, ajira mpya na sababu nyinginezo.

“Kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Serikali imeendelea kulipa madai ya malimbikizo ya mshahara ya watumishi wa umma ambapo hadi kufikia Juni 2016 watumishi 31,032 walilipwa jumla ya Sh 28,929,095,373.89,” alisema Kairuki

Aliongeza kuwa madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi 7,871 yenye zaidi ya Sh bilioni 13.7 yamehakikiwa na kuingizwa kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara na sasa yanasubiri kulipwa.

Kairuki alisema madai ya watumishi 8,776 yenye zaidi ya Sh bilioni 15.5 yanaendelea kuhakikiwa ili yaingizwe kwenye mfumo kwa ajili ya kufanya malipo.

Waziri huyo alieleza kuwa katika shughuli za kila siku madeni huzalishwa, hivyo azma ya Serikali ni kuhakikisha yanalipwa mara yanapojitokeza.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles