Na MWANDISHI WETU –DAR ES SALAAM
MADAKTARI bingwa wa upasuaji wa nyonga na magoti kutoka India, wanatarajiwa kuwafanyia uchunguzi na upasuaji watu wenye matatizo hayo nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Hospitali ya Regency, uchunguzi wa magonjwa hayo utafanyika kuanzia tarehe 23, 24 na 25 mwezi huu katika hospitali hiyo Upanga jijini Dar es Salaam.
Ilisema ujio wa mtaalamu huyo utapunguza gharama za wagonjwa kwenda nje ya nchi kufuata tiba hiyo.
“Katika jitihada za kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda matibabu nje ya nchi na kuokoa fedha nyingi za kigeni ambazo zimekuwa zikitumika tumeona ni vyema kuita mara kwa mara mtaalamu huyu kufanya upasuaji hapa Dar es Salaam,” ilisema taarifa hiyo
IIisema ujio wa mtaalamu huyo umekuwa ukisaidia kuwapa ujuzi wataalamu wa ndani ili mwishowe wawe na utaalamu wa kufanya upasuaji wa aina hiyo wao wenyewe.
Aidha, ilisema mpango wa kuita madaktari hao bingwa wa magoti na nyonga umekuwa ukiratibiwa na hospitali ya Regency kwa kushirikiana na hospitali ya HCG Multi-Specialty iliyoko mji wa Ahmedabad nchini India.
“Tunatarajia mtaalamu huyo atafanya uchunguzi kuanzia tarehe 23, 24 na 25 Januari na wale watakaobainika kuwa na matatizo hayo watafanyiwa upasuaji.
“Hii ni fursa ya kipekee kwa watanzania wenye matatizo kama haya kuchangamkia fursa hii kwani badala ya kwenda nje na kutumia gharama kubwa kusafiri na wasaidizi wao kwenda nje ya nchi sasa wanafanyiwa upasuaji hapa hapa nchini,” ilisema taarifa hiyo