25.2 C
Dar es Salaam
Saturday, January 29, 2022

MADAI YA TUCTA YATUA KWA JPM

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli, amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) na kuwahakikishia kuwa Serikali itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano kati yake na wafanyakazi kwa manufaa ya taifa.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Tucta kutoa maazimio ya Baraza la Wafanyakazi, ikiwamo kudai haki za wafanyakazi kwa kuiburuza Serikali mahakamani ikiwa itashindwa kuzitoa.

Taarifa iliyotolewa jana na Ikulu, ilieleza kuwa Rais Magufuli alikutana na viongozi wa Tucta, Ikulu Dar es Salaam, ambako pamoja na mambo mengine, alisema kuwa Serikali itaimarisha ushirikiano na ipo tayari kupokea maoni na ushauri wowote utakaotolewa na vyama vya wafanyakazi wenye lengo la kuboresha masilahi ya wafanyakazi na kuongeza tija kazini.

Rais Magufuli alisema Serikali inatambua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi na itaendelea kuchukua hatua za kukabiliana nazo kama ambavyo imeanza kufanya.

“Nataka kuwahakikishia nyinyi viongozi wa Tucta na wafanyakazi wote kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inawapenda wafanyakazi na ipo tayari kuwapigania, jambo la msingi tutangulize masilahi ya Taifa, kawaambieni wafanyakazi wachape kazi na Serikali itawalinda,” alisema Rais Dk. Magufuli.

Kwa upande wao viongozi wa Tucta wakiongozwa na rais wao, Tumaini Nyamhokya, walimpongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali yake kujenga uchumi imara, kuimarisha utendaji kazi wa watumishi wa Serikali, kupambana na rushwa, kuondoa watumishi hewa na kulipa madeni ya watumishi.

Viongozi hao wameahidi kushirikiana na Serikali katika kusimamia haki na wajibu wa wafanyakazi na wameomba Serikali iendelee kufanyia kazi masuala mbalimbali ya wafanyakazi, ikiwamo kuwalipa stahili zao na kuboresha mazingira ya kazi.

Wiki iliyopita Tucta, walijipanga kuiburuza Serikali mahakamani kudai haki za wafanyakazi, ikiwamo kushindwa kuzingatia nyongeza ya mshahara kwa wafanyakazi wa umma.

Pamoja na hayo, shirikisho hilo lilisema kuwa wamechoshwa na Serikali kushindwa kutekeleza hoja zao haraka.

Kauli hiyo ilitolewa na Nyamhokya, alipokuwa akisoma maazimio manane ya kikao cha Baraza Kuu la shirikisho hilo.

Nyamhokya alisema tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani, haijafanya nyongeza yoyote ya mshahara kwa watumishi wake.

Kutokana na hali hiyo, alisema ni lazima Serikali izingatie nyongeza ya mshahara katika mwaka ujao wa fedha (2017/2018), kwani hivi sasa wafanyakazi wanaishi maisha magumu na yenye kudhalilisha.

Alisema kuwa Serikali inapaswa kuzingatia nyongeza hiyo ikizingatiwa kwa sasa kuna uwepo wa mfumuko wa bei unaofikia asilimia 5.5, kupanda kwa gharama za maisha na kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani.

 

KAGAME ATUMA UJUMBE

Wakati huo huo, Rais Magufuli amepokea barua yenye ujumbe wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame, iliyowasilishwa kwake na mjumbe maalumu ambaye ni Waziri wa Elimu wa Rwanda, Dk. Musafiri Malimba.

Pamoja na kupokea barua hiyo, Rais Magufuli na Dk. Malimba wamezungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda, ikiwamo katika sekta ya elimu, hususani maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Rais Magufuli ameipongeza Rwanda kwa kuamua lugha ya Kiswahili ianze kufundishwa katika shule zake na ameahidi kuwa Tanzania ipo tayari kutoa walimu wa kwenda kufundisha lugha hiyo.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
177,207FollowersFollow
532,000SubscribersSubscribe

Latest Articles