RAMADHAN HASSAN,DODOMA
MBUNGE wa Madaba,Joseph Mhagama (CCM) amesema Tanzania haitakuwa na mapinduzi ya Kilimo kama haitaweza kufikisha pembejeo katika maeneo ya vijijini.
Kauli hiyo ameitoa leo Mei 20 bungeni wakati akichangia mjadala wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, kwa mwaka wa fedha 2018-2019.
“Hatutakuwa na mapinduzi ya kilimo kama hatutakuwa na mapinduzi jinsi ya kufikisha pembejeo kwa wakulima wadogo.Wakulima wetu wapo vijijini na mbolea na viuatilifu vipo mjini tutafanikiwaje,”amehoji Mhagama.
Muhagama amesema katika maeneo ya vijijini kumekuwa na changamoto ya gharama za kufungua maduka ya kuuzia mbolea na viuatilifu hali ambayo imekuwa ikiwafanya wananchi washinde kufungua maduka.
“Mambo ni mengi kuna vyeti vya kuanzishia biashara ni gharama kubwa kabla hujafungua duka lazima uwe na laki sita mjasiriamali atakuja kuwekeza kwenye hii bishara kweli.
“Ushauri wangu zipitiwe hizi tozo na gharama ikiwezekana ziondolewe ili kumsaidia huyu mkuluma mdogo tusipofanya hivyo tutaendelea kuwaumiza wakulima,”amesema Mhagama.