27.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Machinga watahadharishwa kutowagombanisha viongozi wa Serikali

Na Clara Matimo, Mwanza

Wafanyabiashara wadogo (machinga) wametakiwa kuacha tabia ya kukiuka kwa makusudi maagizo ya Serikali na kuwagombanisha watumishi wa umma na waajiri wao.

Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hasani Kabeke, aliyeshika kipaza sauti akiwa pamoja na viongozi mbalimbali meza kuu akiomba dua baada ya kufuturu.

Wito huo umetolewa Aprili 26, 2022 jijini Mwanza na Sheikh wa Mkoa, Hasani Kabeke, katika hafla maalum ya futari iliyoandaliwa kwa makundi mbalimbali na Mkuu wa mkoa huo, Mhandisi Robert Gabriel, aliyeshirikiana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi(CCM)Taifa Mkoa wa Mara, Christopher Gachuma huku akiwataka machinga kufanya biashara kwenye maeneo waliyopangiwa na serikali

Kauli hiyo ya Sheikh Kabeke imekuja huku kukiwa na uwepo wa matukio ya baadhi ya machinga jijini hapa kukiuka maagizo yaliyotolewa na serikali yakuwataka kutopanga na kufanya biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa hali iliyosababisha vyombo vya ulinzi kuwaondoa kwa nguvu na kuzua taharuki.

“Machinga msiwe sababu ya kuwapotezea kazi viongozi wetu, mnapokaidi maagizo mliyopewa na serikali mnawasababishia viongozi wetu migongano na mabosi wao bila sababu ya msingi.

“Hata Quran inatutaka tufuate sheria za uongozi bila shuruti, huo ndiyo uislamu na ukristo pia hivyo hivyo maana ndani ya biblia Mwenyezi Mungu ameagiza hivyo hakuna dini inayotaka waumini wake wawe sababu ya migogoro na uvunjifu wa amani katika jamii,” amesema Sheikh Kabeke na kuongeza:

“Makundi yote yanawajibu wa kutii sheria bila shuruti wakiwemo machinga, hata sisi viongozi wa dini baadhi yetu ni machinga  na tumefuata maagizo na maelekezo ya serikali, kwanza utaratibu wa kupanga maeneo maalum kwa ajili ya machinga uliofanywa na serikali unafaa kupongezwa  wote ni mashahidi mji umependeza tofauti na awali ambapo baadhi ya nyumba za ibada zilikuwa haziingiliki machinga wamepanga bidhaa zao hadi mlangoni,”amesema Sheikh Kabeke.

Kwa upande wake Mhandisi Gabriel amesema lengo la kuandaa futari hiyo ni kumfuturisha mfungaji ili kudumisha amani, utulivu, maelewano, masikilizano na kuvumiliana baina ya wananchi na viongozi wao wa kada mbalimbali.

“Serikali haina dini lakini inategemea sana viongozi wa dini kufikisha ujumbe kwa wananchi wake kuhusu amani miongoni mwao hivyo naomba amani na mshikamano uendelee kutawala mkoani kwetu na nchi yetu kwa jumla baina ya waislamu na wakristo,”amesema Mhandisi Gabriel.

Naye, MNEC Christopher Gachuma amesema anajisikia furaha kupata nafasi kila mwaka kuandaa futari kwa ajili ya waislamu katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo alianza kufanya hivyo tangu mwaka 1995 lengo likiwa ni kumuenza rafiki yake aliyekuwa muislamu ambaye ameishatangulia mbele ya haki.

Hafla hiyo ya futari ilihudhuriwa na  viongozi mbalimbali wa serikali, madhehebu ya dini na wananchi wa kada tofauti  tofauti wakiwemo masheikh, maaskofu wachungaji, wakuu wa wilaya na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Ngusa Samike.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles