Machinga jalini usalama wenu kwanza fedha baadae

0
2006

 Na Frank Kagumisa (SAUT)

UKOSEFU wa ajira umewafanya watu  wengi kujihusisha na shughuli ndogo ndogo ili kujiingizia kipato.

Hakuna kulala, hivi ndivyo unavyoweza kusema hasa ukipita maeneo ya mijini, huko utashuhudia vijana wakichakarika asubuhi, mchana na usiku wakitafuta fedha. Changamoto iliyopo ni ukosefu wa maeneo ya kutosheleza idadi ya wafanyabiashara hao.

Katika maeneo mengi utakuwa watu wamepanga bidhaa zao pembezoni mwa barabara na wengine hutembeza kuuza kwenye magari yakiwa kwenye foleni.

Mara kadhaa tumeshuhudia mamlaka zinazohusika na masuala ya usafi wa miji, manispaa na hata ulinzi wakiwaondoa wafanyabiashara hao na wengine kufikishwa hadi mahakamani.

Hatua hiyo ililenga kusafisha miji katika maeneo husika lakini pia kuhamasisha wafanyabiashara hao kwenda katika maeneo yaliyopangwa kwa biashara.

Lakini yaliibuka malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara wengi wakidai kuonewa dhidi ya hatua zinazochukuliwa juu yao.

Akiwa ziarani Mwanza, Rais Dk. John Magufuli aliwahi kuagiza mamlaka kuacha kuwaondoa wafanyabiashara hao, agizo hilo lilipokewa kwa nderemo na vifijo na kundi hilo, wakaanza kurejea kwa kasi kule walikoondolewa.

Si lengo langu kupinga agizo la Rais Magufuli, bali kuwashauri wafanyabiashara hao kuhusu umuhimu wa kuzingatia usalama wao wanapokuwa katika shughuli zao.

Nimeeleza awali kwamba wengi wanafanya biashara zao pembezoni mwa barabara ambako kiusalama ni hatari kwani gari zinaweza kuacha njia na kuwafuata, kuwagonga kule walikopanga bidhaa zao.

Lakini pia kutokana na msongamano wa watu katika maeneo hayo, usalama kwa watumiaji wengine wa barabara huwa mdogo wapo ambao huibiwa pindi wanaponunua bidhaa.

Ni kweli wanahitaji fedha kwa ajili ya kujikimu kwa maisha yao, familia zao na hata kuchangia uchumi wa nchi, lakini wanapaswa kuzingatia pia suala la usalama wao na watu wengine wanaotumia barabara.

Mfano hai ni pale eneo la Ubungo ambako inajengwa barabara ya juu (fly-over), utaona mafundi wapo wanaendelea na ujenzi na wakati huo huo wafanyabiashara hao nao wanaendelea na shughuli zao.

Ni hatari hata kwa afya zao, kwani eneo hilo kutokana na shughuli za ujenzi huwa kuna vumbi jingi na hivyo kuwaweka katika hatari ya kupata magonjwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here