30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Machinga Complex chanzo cha wizi wa mapato Karume

Jamal Malinzi
Jamal Malinzi

Na MARTIN MAZUGWA,

WAHENGA walisema ukicheka na nyani utavuna mabua, ni msemo kama misemo mingine iliyowahi kusemwa, lakini ikiwa na maana kubwa kama itaweza kufafanuliwa kwa umakini na kutambua maana halisi ya kile inachomaanisha.

Hakuna nyumba isiyo na msingi na kama ipo na ajitokeze mjenzi wa nyumba hiyo ajisifu kwa ubunifu wake, ninachoamini mimi msingi na  ubora wa kitu unatokana na maandalizi yake ya awali ambayo ndiyo hutoa taswira halisi ya kitu.

Msingi wa Ligi Kuu unatokana na Ligi Daraja la Kwanza, kwani timu ili ipande ni lazima ipitie ligi hiyo ndipo ipande daraja, timu zinazoshiriki Ligi Kuu zimetoka huku chini na kuweza kufika hapo zilipo, ligi ya awali imeonyesha kusahauliwa kutokana na mambo ambayo yamekuwa yakifanyika katika viwanja mbalimbali.

Kilio kikubwa kwa timu zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ni suala la ukata na kukosekana kwa wadhamini, kitu kinachopelekea wachezaji kukosa mishahara pamoja na posho.

Timu nyingi zinazoshiriki ligi hii, zinategemea viingilio vya mashabiki wanaoingia uwanjani kwa ajili ya kuendesha baadhi ya mambo,  ikiwemo kutoa mishahara pamoja na kufanya usajili wa wachezaji wao  na benchi la ufundi.

Kitendo cha kupata mapato kidogo ya viingilio vya uwanjani, yanasababishwa na baadhi ya watu wasiopenda maendeleo ya mchezo wa soka hapa nchini, ikiwemo wafanyabiashara wa soko la Machinga Complex ambalo ni kikwazo kikubwa katika Uwanja wa Karume.

Madhara ya haya ni makubwa, kwani ni sababu ya  kutofanya vizuri kwa baadhi ya timu zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, hivi sasa mpira unahitaji gharama kubwa ili uweze kufanya vizuri.

Huwa siamini kama kweli Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),  limeshindwa kabisa kuwazuia wale wote wanaokaa katika jengo la biashara la Machinga Complex, kwani wamekuwa  wakiangalia mpira pasipokuwa na hofu ya aina yoyote ile na wasimamizi wa Ligi wakiwa kimya kana kwamba suala hili hawalioni.

Jambo hili ambalo ni zito limekuwa halipewi uzito unaostahili, kwani ikiwa suala hili halitachukuliwa hatua mapema litakuwa na athari kubwa kwa soka la nchi hii hapo baadaye.

Taratibu jambo hili limeanza kukua, watu wengi wamekuwa wakikaa juu ya jengo hilo huku mashabiki wachache na wapenda soka wakiingia uwanjani na kuzisapoti timu zao pindi zinapocheza.

Kama hali itaendelea kuwa hivi kila siku, haitokuwa ajabu kusikia baadhi ya timu zikishindwa kusafiri, kwani watu wengi wamekuwa wakiangalia michezo mingi pasipo kutoa hata senti tano, jambo linaloziumiza baadhi ya timu ambazo hazina udhamini na zinajiendesha zenyewe kwa kutegemea michango ya mashabiki na wanachama.

Ili kuweza kudhibiti suala hili, ulinzi unapaswa kuimarishwa katika soko hili, pindi michezo ya Ligi Daraja la Kwanza inapochezwa ili kuweza kudhibiti uhalifu huu ambao umeanza kukua kwa kasi kubwa, huku wimbi kubwa la watu  ambao wanakaa katika soko hilo  kuangalia mpira likiongezeka.

Mazoea hujenga tabia, imekuwa ni kama wafanyabiashara hawa wamepewa kibali cha kuangalia mpira bure pindi mechi mbalimbali za Ligi hiyo zinapochezwa kwenye Uwanja wa Karume.

Je, ni kweli TFF wameshindwa kudhibiti suala hili? Ni swali ambalo nimekuwa nikijiuliza kila siku na kushindwa kupata majibu sahihi, ambayo yataniridhisha kuwa shirikisho limeingia makubaliano na soko kuwa wafanyabiashara waangalie mpira bure.

Naomba ufafanuzi wa jambo hili mapema ili tujue kama wale wanaoangalia mpira wana ruhusa ya kufanya hivyo au wanafanya kimakosa na kama ni kosa kwa nini hawachukuliwi hatua.

Sitaki kuamini kama kweli shirikisho limekubali kuona timu zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, kila siku zikitembeza bakuli la kuomba msaada ilhali wanaweza wakatumia viingilio kutatua matatizo yao.

Mtanzania tunaomba TFF ichukue hatua za haraka kuhusu jambo hili, maana mficha maradhi kifo humuumbua, hatutaki tufike huko,  haitapendeza kuona baadhi ya timu zikishindwa kumudu gharama za uendeshaji kutokana na ukata.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles