MACHAFUKO YANUKIA DRC BAADA KUTANGAZWA HAKUNA UCHAGUZI

0
401

KINSHASA, DRC


UPINZANI umepanga kutumia nguvu ya umma baada ya Taume ya Uchaguzi nchini hapa kusema uchaguzi wa rais atakayechukua nafasi ya Rais Joseph Kabila hauna uwezekano wa kufanyika mwaka huu.

Hilo huenda likazua upya machafuko yaliyoshuhudiwa mwaka jana kwa vile bi ukiukaji wa makubaliano yaliyoyasitisha mwaka jana, ambayo yalimruhusu Kabila kuendelea kubaki madarakani hadi mwishoni mwa mwaka huu.

Kugoma kwa Kabila kuondoka madarakani mwishoni mwa muhula wake wa pili Desemba mwaka jana kuliibua machafuko yaliyoua makumi ya watu.

Upinzani haukuchukua muda kuibuka kulaani tangazo hilo la Rais wa Tume, Corneille Nangaa, ikisema huko ni ‘kutangaza vita.’

“Rasilimali tulizo nazo, zinatupa sababu zaidi za kuamini kuwa Desemba, haitawezekana kufanyika uchaguzi kama ilivyopangwa,” Nangaa alisema katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Ufaransa, TV5Monde.

Chini ya makubaliano yaliyofikiwa Desemba 31 mwaka jana kati ya wawakilishi wa Kabila na viongozi wa upinzani, Kabila, aliye madarakani tangu 2001, pia alizuiwa kujaribu kubadili katiba ili awanie urais kwa muhula wa tatu.

Hata hivyo, Kabila alisema uchaguzi utafanyika tu pale tume ya uchaguzi itakapomaliza kuorodhesha mamilioni ya wapiga kura.

Katika kuitikia kauli za Nangaa, kiongozi wa upinzani Felix Tshisekedi aliandika katika mtandao wa Twitter kuwa rais wa tume ametangaza vita kwa watu wa Kongo na ameonya watachukua hatua kali kushirikisha nguvu ya umma mitaani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here