29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

MABOSI ACACIA WAZIDI KUKUNA VICHWA MAKINIKIA

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Acacia, Brad Gordon

Na JUSTIN DAMIAN – DAR ES SALAAM

KAMPUNI ya kuchimba madini ya Acacia Mining Plc, imesema Mwenyekiti wa Barrick, Profesa John Thornton ambaye alifanya mazungumzo na Rais Dk. John Magufuli, Ikulu Dar es Salaam juzi, hakusema kama watalipa malimbikizo ya kodi.

Acacia ilitoa ufafanuzi huo jana katika mkutano wa wanahisa baada ya mwanahisa mmoja kutaka kujua kama ni kweli kampuni hiyo ilitoa ahadi ya kulipa malimbikizo ya kodi za nyuma ambazo haikulipa kwa Serikali ya Tanzania.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Acacia, Brad Gordon, aliwaambia wanahisa kupitia mkutano kwa njia ya simu kutokea makao makuu ya kampuni hiyo London, Uingereza jana kuwa mwenyekiti huyo hakuzungumza chochote kuhusu kulipa kodi.

“John Thornton hakusema chochote kuhusu kulipa kodi. Hata ukifuatilia mahojiano aliyofanya na vyombo vya habari Dar es Salaam, hakuna sehemu yoyote ile aliyozungumzi suala la kodi,” alisema Gordon.

Akiwa na mkuu wa kitengo cha fedha wa kampuni hiyo, Andrew Wray, Gordon alisema ripoti ya kamati ya pili iliyotolewa Jumatatu Juni 13, mwaka huu haikuwa nzuri kwa Acacia, lakini haikuwashangaza kwa kuwa walitegemea ingekuwa hivyo.

“Kwa sasa tunachokifanya ni kujiandaa kwa mazungumzo ambayo yatasababisha kupata mwafaka wa suala hili, huu pia ndio msimamo wa Rais wa Tanzania. Acacia inaona majadiliano ni njia bora kwa pande zote mbili ya kuweza kufikia mwafaka,” alisema.

Wakati Acacia wakisema hivyo, taarifa iliyotolewa juzi na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu na video ya Rais Magufuli ilieleza kwamba katika mazungumzo yao wamekubaliana kuunda timu mbili za majadiliano.

Alisema timu hizo zitahusisha Serikali ya Tanzania na wawakilishi wa Kampuni ya Barrick kutoka Canada na Marekani na watafanya majadiliano ambayo yatahusu namna ya kufikia mwafaka kwenye suala la kusafirisha mchanga wa madini (makinikia) nje ya nchi kwa faida ya pande zote mbili.

Kupitia taarifa hiyo, Rais Magufuli alisema timu hiyo itapitia mapendekezo yote na Profesa Thornton amekubali chochote ambacho kitakuwa kimekubalika watalipa.

“Akasema ni bahati mbaya wanatubu kwa haya yaliyotokea, nikamwuliza jina lako ni nani akasema ni John na mimi nikamwambia langu ni John kwa hiyo hapo tutaishi kwenye makubaliano.

“Kwa hiyo amesema kwa wiki moja au mbili tutakapowahitaji waje waingie kwenye mazungumzo na ametoa mfano kuwa amehusika hivyo hivyo katika nchi ya Dominica, ambako nako walikuwa wanachimba dhahabu, viongozi wa kule wakasema wanaibiwa ikabidi waingie kwenye mazungumzo watengeneze mkataba mwingine.

“Pia akaniambia kwamba walifanya hivyo Saudi Arabia, nako walikuwa wanadhulumiwa Serikali ya kule ikawa wazi na baada ya makubaliano sasa wana hisa asilimia 50 kwa 50.

“Hivyo akasema yaliyofanyika Dominica na Saudi Arabia hayana ugumu kufanyika Tanzania,” alisema Rais Magufuli akielezea mazungumzo yake na Profesa Thornton.

Mwenyekiti huyo wa Barrick alikuja nchini siku chache baada ya ripoti ya Kamati ya pili iliyoundwa na Rais Magufuli kusema kwamba Kampuni ya Acacia ni hewa kwa sababu haina usajili wowote nchini.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa iliyosambazwa juzi, timu hizo zitakutana baada ya wiki moja hadi mbili kuanzia sasa.

Katika taarifa hiyo, Msigwa alisema pamoja na Profesa Thornton kukubali kulipa fedha zinazodaiwa, pia amekubali kushirikiana na Tanzania kujenga mtambo wa kuchenjua dhahabu (smelter) hapa nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles