30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mabilioni yateketea katika bomoabomoa

bomoaNA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

KAZI  inayoendelea ya kubomoa nyumba zilizojengwa katika maeneo ya yasiyoruhusiwa kisheria, yakiwemo ya mabondeni nchini kote, yataigharimu Serikali kutumia zaidi ya Sh bilioni moja, MTANZANIA imebaini.

Tayari Serikali imetumia Sh milioni 108.3 hadi jana katika jiji la Dar es Salaam kwa kipindi cha siku kumi, tangu kazi ya bomoabomoa ilipoanza katika maeneo ya mabondeni.

Baadhi ya maofisa kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wale wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), waliliambia gazeti hili kuwa, hadi kumalizika kwa kazi hiyo Serikali itakuwa imetumia zaidi ya Sh bilioni moja nchi nzima.

Serikali hutumia Sh milioni mbili kwa siku, kwa ajili ya kulipia magari maalumu ya ubomoaji maarufu kama Tingatinga.

“Fedha nyingine zimeelekezwa kwa wafanyakazi wanaoweka alama ya X ambao wamekuwa wakibadilika kulingana na kazi inavyokuwa kubwa, ambapo idadi yao huanzia 50 hadi 80 na hulipwa Sh 50,000 kwa siku,” kilisema chanzo chetu cha habari.

MTANZANIA ilipotaka kupata ukweli kuhusu gharama za malipo ya wafanyakazi wanaoweka alama ya X kwenye majengo yaliyojengwa katika maeneo hatarishi ya Gongo la Mboto na Pugu, mmoja wa maofisa hao ambaye hakutaka jina lake litajwe, alikiri Serikali kulipa kiasi hicho cha fedha.

Wafanyakazi wengine wanaolipwa kwenye kazi hiyo ni askari polisi ambao idadi yao inakuwa kati ya 30 na 90 kulingana na maeneo yenye vurugu na yasiyokuwa na vurugu.

Mtanzania limeshuhudia wafanyakazi hao wakilipwa posho zao na mwakilishi wa NEMC, katika vituo vya Polisi vya Stakishari na Ukonga jijini Dar es Salaam, baada ya kumaliza kazi.

Taarifa hizo zilieleza kuwa, magari hayo ambayo yamefanyakazi kwa siku saba yametumia zaidi ya Sh milioni 54, huku mengine yakiwa hayajafanyakazi ya kubomoa nyumba.

Hata hivyo baadhi ya maofisa hao walishangaa kuona kiwango kikubwa cha fedha kikitumika kwa kazi hiyo. “Fedha hizi ni nyingi zingeweza kutengwa kwa ajili ya kujenga nyumba za bei nafuu na kuhamisha kaya zaidi ya 8,000,”  alisema mfanyakazi huyo.

MCHANGANUO

Mchanganuo wa gharama zilizotumiwa katika siku ya kwanza Serikali ilitumia Sh milioni 4.5 kwa ajili ya kuwalipa askari 90 ambao kila mmoja alilipwa Sh 50, 000.

Wafanyakazi wengine 82 walilipwa Sh milioni 4.1 kwa siku hiyo hiyo, huku magari ya Tingatinga manne yakigharimu Sh milioni nane na kufikia jumla ya Sh milioni 16.6.

Siku ya pili gharama zilizotumiwa askari walikuwa 60 waliolipwa Sh milioni tatu, wafanyakazi 74 walilipwa Sh milioni 3.7 na gharama za magari manne ilikuwa Sh milioni  nane, ambazo jumla yake ilikuwa ni Sh milioni 14.7.

Gharama hizo zilikuwa zikipanda na kushuka kulingana na idadi ya wafanyakazi na gharama nyingine za uendeshaji.

Ukijumlisha gharama zote zilizotumika katika kazi hiyo ya bomoabomoa na uwekaji wa alama ya X kwa siku 10 iligharimu Sh milioni 108.3 kwa jijini la Dar es Salaam pekee.

Alama X yaendelea

Akizungumza baada ya kumaliza uwekaji wa alama katika Manispaa ya Ilala, Ofisa Mipango Miji wa manispaa hiyo, Alfred Mbyopyo, alisema Mto Msimbazi umeharibiwa vibaya kutokana na shughuli za uchimbaji mchanga na kilimo unaosababisha mmomonyoko wa udongo katika kingo za mto.

Hadi jana nyumba ambazo zilikuwa zimewekewa alama ya X kwa maeneo mbalimbali jijini zilikuwa 16,000 na zile zilizobomolewa zimefikia 700.

KAULI YA SERIKALI

Akizungumzia fedha zinazotumiwa kwenye bomoabomoa inayoendelea, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, alisema anachojua ni kwamba fedha za bajeti huwa hazitumiwi zote nyingine hubaki kwa kazi za dharura.

Alisema ni ngumu kuelezea moja kwa moja fedha hizo zimetolewa katika mfuko gani kwa sababu kazi yenyewe inashirikisha wizara zaidi ya nne.

“Kazi hii tunashirikiana na wizara nne ambazo ni Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na  Wizara Maji na Umwagiliaji” alisema Mabula.

USHAURI

Hivi karibuni katika mahafali ya Chuo Kikuu cha Ardhi, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Idris Mshoro alisema nchi inakabiliwa na changamoto nyingi za usimamizi wa mipango miji.

Alisema mfano, ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya tathmini ya shughuli za Mipango Miji Tanzania ya Desemba 2014 inaainisha kwamba miji 96, kati ya miji 148 iliyokaguliwa yaani asilimia 65 haikuwa na mpango kabambe wa kuendeleza miji hiyo tangu ilipoanzishwa.

Ili kukabiliana na changamoto hizo, Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) kimetayarisha wataalamu katika maeneo hayo ili kuhakikisha changamoto hizo zinatatuliwa na kumalizwa.

Habari hii imeandaliwa na Shabani Matutu, Florian Masinde, Tunu Nassor na Grace Shitundu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles