22.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

Mabalozi wa Kodi waendelea kuhamasisha ulipaji kodi

Na Mwandishi Wetu, Namanga

Mabalozi wa Kodi walioteuliwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba wako katika mikoa ya Kaskazini ambayo ni Arusha, Kilimanjaro na Tanga kwa ajili ya kuhamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari ili kuongeza mapato ya Serikali.

Mabalozi hao wamepata fursa ya kutembelea Kituo cha Huduma kwa Pamoja cha mpakani Namanga mkoani Arusha na kukutana na baadhi ya wadau na walipakodi ambapo wamewahimiza kuendelea kulipa kodi kwa hiari na wakati.

Wakizungumza wakati wa ziara hiyo Mabalozi hao wa kodi, wameipongeza Serikali kwa kuwa na Vituo vya Huduma kwa Pamoja mipakani kwani vimeondoa kero zilizokuwepo kipindi cha nyuma na kusifu ushirikiano uliopo katika ya TRA na wafanyabiashara ambao umesaidia Mkoa wa Arusha kuvuka malengo ukusanyaji mapato.

“Katika kituo hiki cha Namanga, nimejifunza mambo mengi, moja wapo ni namna nchi hizi mbili za Tanzania na Kenya zilivyoondoa urasimu uliokuwepo kipindi cha nyuma.

“Nikiwa kama Balozi, nitatumia elimu hii niliyoipata kutoka TRA kuwahamasisha wananchi kujenga tabia ya kulipa kodi kwa wakati kwa maendeleo ya nchi yetu,” alisema Kumwembe mmoja wa mabalozi hao.

Kwa upande wake Balozi Zulfa Omari, ambae ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba, Zanzibar akizungumza wakati wa kikao kati ya wafanyabiashara wa Arusha na mabalozi hao, alisema kuwa ni nadra sana kukuta wafanyabiashara wakiizungumzia vizuri TRA lakini amefarijika kuona walipakodi wa Arusha wakiipongeza TRA kwa kuboresha huduma zao.

“Kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi kulikuwa na mambo mengi niliyokuwa nikiyasikia kuhusu TRA na yalikuwa yakiniumiza sana lakini hapa Arusha nimesikia kitu cha faraja kwamba TRA inazungumzwa vizuri mbele yetu kitu ambacho si kitu cha kawaida maana wafanyabiashara mara nyingi huwa hawaizungumzii vizuri TRA,” alisema Balozi Zulfa.

Balozi mwingine ni Subira Khamis Mgalu Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani ambae alisema kuwa kupitia ziara hii amejifunza taratibu mbalimbali zinazotumika wakati wa uingizaji wa mizigo kutoka ndani na nje ya nchi kupitia Kituo cha Namanga.

“Kama Balozi nimefahamu kwa kina jinsi mifumo inavyofanya kazi katika kituo hiki cha Namanga ambayo huisaidia Serikali kukusanya mapato stahiki kutoka vyanzo mbalimbali.

Kwa upande wa walipakodi na wadau ambao tumekutana nao Arusha Mjini, naweza kusema kuwa, usemi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan umedhihilika wazi kuwa, kodi inaweza kukusanywa bila kutumia mabavu kwa sababu Mkoa huu wa Arusha umevuka malengo bila kuwasumbua walipakodi wake,” amesema.

Balozi Mgalu amewasisitiza walipakodi hao kuongeza ushirikiano kwa TRA ili kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kuwaahidi kwamba, changamoto zote walizozitoa wamezipokea na watazifanyia kazi.

Kazi wanazozifanya Mabalozi hao wa Kodi katika ziara yao ya kikazi kwenye mikoa hiyo ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga ni pamoja na kutembelea viwanda, kutembelea vituo vya huduma kwa pamoja mipakani na kukutana na wafanyabiashara kwa ajili kuwahamasisha kulipa kodi kwa hiari na wakati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,717FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles