31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mabaharia nchini wajivunia walivyojitoa kwa taifa wakati wa Uviko-19

Na Nyemo Malecela, Kagera

Mabaharia nchini wamejivunia jinsi walivyotoa rehani maisha yao katika kipindi cha Uviko-19 ili kuhakikisha wanaendelea kufanya kazi usiku na mchana kwa ajili ya kupandisha kiwango cha uchumi wa Tanzania na Dunia kwa ujumla.

Mabaharia hao wameeleza hisia zao Juni 29, 2022 ikiwa ni siku chache tangu yalipofanyika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mabaharia yakiwa ni ya 12 tangu kuanzishwa kwake wakati kitaifa mwaka huu yakihadhimishwa katika uwanja wa Mayunga mjini Bukoba mkoani Kagera.

Katika kilele cha maadhimisho hayo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Profesa Faustine Kamuzora kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbalawa amesema katika kipindi hicho mataifa mengi yaliingia karantini na kuzuia baadhi ya usafiri lakini mabaharia waliendelea kusafirisha mizigo ili nchi na dunia visikose mahitaji muhimu.

Profesa Kamuzora amesema asilimia 90 ya biashara zote duniani zinabebwa na meli wakati huo huo ukiwa ni usafiri wenye gharama ndogo ya kusafirisha bidhaa ukilinganisha na njia nyingine za usafirishaji kitaifa na kimataifa.

Ameongeza kuwa mpaka sasa duniani kuna mabaharia 1,600,000 wakati Tanzania ikiwa na mabaharia 5,300 huku wanwake wakiwa ni asilimia 1 pekee.

“Kupitia maadhimisho haya, mabaharia hawa hupata ujasiri wa kueleza changamoto wanazokumbana nazo katika kazi zao ili ziweze kufanyiwa kazi kwa lengo la kuboresha maisha na ustawi wao wa leo na baadae ukizingatia umuhimu wa kada hii katika kukuza uchumu wa Taifa na Dunia kwa ujumla.

“Kada ya ubaharia imeendelea kuzalisha wafanyakazi wengi wanaokidhi viwango vya kimataifa wanaoweza kuaminiwa duniani kote na kuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Tanzania,” amesema Profesa Kamuzora.

Upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Mawakala wa Meli Tanzania (TASAC), Kapteni Musa Mandia amesema shirika hilo kwa kushirikiana na wadau wengine wanaohusika na usafiri na usafirishaji kwa njia ya maji wameamua kufanya mahadhimisho hayo mkoa wa Kagera ili kuwaelimisha wananchi kuwa njia bora na ya urahisi kwa gharama nafuu ni kupitia njia ya meli.

Amesema wamekusudia kuhakikisha wananchi wanapata elimu itakayowasaidia kuwa salama wao na vyombo vyao vya usafiri kwa kuzingatia sheria na taratibu kwa kuwa mkoa wa Kagera una eneo kubwa la maji na visiwa visivyopungua 39, hivyo huduma hiyo inatumika kwa kiwango kikubwa.

Kepteni Mandia amesema elimu walivyotoa kwenye mahadhimisho hayo itawasaidia wananchi wa Mkoa wa Kagera na mikoa jirani ya Kanda ya ziwa kuzingatia umuhimu na usafiri kwa njia ya maji kwani ndio nyepesi ya usafirishaji kwa kutolea mfano kuwa usafirishaji wa kutumia barabara unaigharimi serikali fedha nyingi katika kutunza miundombinu ya barabara.

Ameongeza kuwa wameweza kutembelea maeneo ya mito na maziwa ili kuyajua zaidi, kuona miundombinu yake ikoje, usalama ukoje katika maeneo hayo pamoja na kuwakumbusha wananchi kuwa kuna mmamlaka zinazosimamia sekta hiyo ili kama wana tatizo linalohitaji uamuzi wa kiserikali waweze kupata msaada.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles