KATIBU Mkuu wa Klabu ya Soka ya Yanga, Baraka Deusdedit, amesema kwamba mkutano mkuu wa wanachama wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika Agosti 6 mwaka huu, utakuwa wa kujipanga zaidi kama ambavyo mahasimu wao Simba walivyoamua kubadilika na kutumia mfumo wa hisa badala ya kadi.
Uamuzi huo wa Yanga huenda ukafuata nyayo za Simba ambao wanakaribia kumpa rasmi mfanyabiashara maarufu nchini Mohamed Dewji ‘Mo’, umiliki wa asilimia 51 za hisa na kumfanya aweke Sh bilioni 20.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Deusdedit alisema wanachama wa klabu hiyo wanatakiwa kuungana na kujipanga wakati wa mkutano huo unaodaiwa kuwa wa dharura.
“Mwenyekiti ndio anafahamu zaidi dhamira ya mkutano huu, lakini si mbaya kwa kuwa wenzetu wamejipanga na sisi tunatakiwa kujipanga zaidi.
“Katika mkutano huo, kama ikitakiwa kufanya mabadiliko pia litakuwa jambo zuri ili kuendana na kasi iliyopo ya uendeshaji wa klabu,” alisema Deusdedits.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya klabu hiyo, zinadai kwamba mkutano huo utajadili ajenda tano ikiwamo ripoti ya mkutano uliopita, maendeleo ya klabu, udhamini wa kampuni ya Quality Group, ujenzi wa uwanja na mambo mengine.