Mabadiliko makubwa bima ya afya

0
1988

Faraja Masinde -Dar es salaam

MABADILIKO makubwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF). Hii ndiyo kauli ambayo unaweza kuisema, wakati leo mfuko huo unatarajia kuzindua vifurushi vipya ya bima ya afya vilivyofanyiwa mabadiliko makubwa lengo likiwa ni kuwafikia Watanzania walio wengi.

Wakati uzinduzi huo unatarajia kufanyika leo, huduma za kitaalamu za matibabu ya figo, moyo na saratani hazipo katika vifurushi vipya, pia wanachama watasubiri kwa siku 30 tangu tarehe ya kulipa mchango kabla ya kunufaika na huduma.

Pia baadhi ya huduma zitakuwa na kipindi cha kusubiri na kutakuwapo na uchangiaji wa baadhi ya huduma.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Bernard Konga alivitaja vifurushi vinavyotarajiwa kuzinduliwa kuwa ni Najali Afya, Wekeza Afya na Timiza Afya.

Akizungumzia vifurushi hivyo, Konga alisema wanachama watanufaika na huduma za matibabu kuanzia ngazi ya zahanati hadi Hospitali ya Rufaa ya Taifa katika vituo zaidi ya 7,500 nchi nzima, ikiwa ni vya Serikali, binafsi na vya madhehebu ya dini.

 “Mwanachama atakwenda ngazi ya hospitali ya kanda ya mkoa na Hospitali ya Rufaa ya Taifa kwa utaratibu wa rufaa, vifurushi vyote vya Najali Afya, Wekeza Afya na Timiza Afya vimezingatia upana wa huduma kwa mwananchi, ikiwa ni kuanzia gharama za kumwona daktari, vipimo, dawa, kulazwa, upasuaji mkubwa na mdogo, matibabu ya kinywa na meno na huduma nyingine.

“Ukubwa wa kitita cha mafao utazingatia aina ya kufurushi ambacho mtu atachagua. Kupitia utaratibu huu mwanachama atalipa mara moja ambapo tunaangalia utaratibu wa mtu kulipa kwa kudunduliza na pale fedha hizo zinapotimia ataweza kupatiwa bima yake,” alisema Konga.

Aidha, alifafanua kuwa mfuko huo unaamini kuwa kuja kwa mfumo huo wa bima kutaimarisha upatikanaji wa bima kwa wananchi wengi kutoka sekta isiyo rasmi kutokana na kuibuka kwa magonjwa mengi na yanayohitaji gharama kubwa jambo ambalo bima hiyo itaweza kusaidia kutokana na wananchi wengi zaidi kujiunga.

 “Hivyo hii ina maana  hata kwa wale ambao kulipia gharama za matibabu ilikuwa changamoto, basi kwa sasa wataweza kumudu, kwani hata Serikali ilikuwa ikitutaka kuja na mpango wa matibabu ya gharama nafuu kwa wananchi.

“Kwani kwa sasa tuna mkataba na vituo zaidi ya 7,000 vikiwamo vya Serikali, mashirika ya dini pamoja na vya binafsi, hivyo mbali na hivyo  mtu atakuwa na uhakika wa kupata matibabu hadi hospitali ya taifa tofauti na ambavyo imekuwa ikipotoshwa na baadhi ya watu.

 “Lakini pia tumetafuta mbinu rahisi zaidi ya kuhakikisha kuwa wananchi wanajiandikisha kirahisi ikiwamo kutoka kwenda kuwatafuta wnanachi huko waliko, lakini kama hiyo haitoshi tuko mbioni kuanza kutumia mfumo wa mtandaoni kwa kuwa mambo mengi kwa sasa yanafanyika huko,” alisema Konga.

Aidha, Konga alisema kuwa kwa utaratibu huo wa sasa mtu anao uwezo wa kuwaongeza ndugu zake mbali na wazazi wake kwa maana ya mjomba, shangazi na wengine tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

 “Tumeangalia pia kundi la watu wenye umri zaidi ya miaka 60, nao wataweza kunufaika kwani inawezekana kwamba kuna wengine hawana wazazi wamebakiwa na wajomba zao au shangazi, hivyo kwa vifurushi hivi nao wataweza kujumuishwa moja kwa moja.

 “Mpango huu wa vifurushi vya bima ya afya unatoa uwanja mpana wa wananchi kujiunga na bima ya afya kwa kujipimia kulingana na mahitaji ya huduma, ukubwa wa familia na umri.

“Lakini ikumbukwe kuwa kifurushi cha Najali utalazwa kwa siku 60, Wekeza siku 90 na Timiza siku 120, ukija kwenye vipimo vya maabara na uchunguzi Najali kuna vipimo 162, wekeza 127 na Timiza 223, ikiwamo vipimo muhimu vya moyo, ultra sound na vipimo vya kibingwa,” alisema Konga.

Alisema mtu mmoja kuanzia miaka 18 hadi 35 atachangia Sh 192,000 kwa kifurushi cha Najali, Sh 384,000 kwa kifurushi cha Wekeza na Sh 516,000 kwa kifurushi cha Timiza.

“Kwa mtu wa kuanzia umri wa miaka 36 hadi 59, atachangia Sh 240,000 kwa kifurushi cha Najali, Sh 444,000 kwa kifurushi cha Wekeza na Sh 612,000 kwa kifurushi cha Timiza.

“Lakini kwa mchangiaji wa miaka 60 na kuendelea, atachagia Sh 360,000 kwa Najali, Sh 660,000 kwa Wekeza na Sh 984,000 kwa Timiza.

“Kwa mmoja mwenye watoto wanne mwenye miaka 18-35 atachangia Sh 636,000 kwa kifurushi cha Najali, Sh 1,092,000 kwa Wekeza na Sh 1,548,000 kwa Timiza.

“Hivyo, kutokana na maboresho haya, wananchi wana fursa ya kukabiliana na gharama za matibabu ambazo zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku na wakati mwingine kushindwa kuzimudu na kuangukia katika janga la umasikini au kifo,” alisema Konga.

Akizungumzia gharama hizo, Konga alisema kuwa kiwango hicho ni nafuu zaidi ikilinganishwa na gharama za matibabu kwa mtu ambaye hana bima ya afya.

“Kwanza tujue tusiangalie gharama ya fedha bali tuangalie unapata nini, kwani kwa Sh 192,000 ni dhahiri kabisa kuwa ni kiwango nafuu, lakini kuhusu wategemezi ni kwamba sasa hivi unaweza kumkatia bima yeyote, awe jirani yako na au yeyote unayeona kwamba anafaa kuwa na bima,” alisema Konga.

Alisema mtu anaweza kujisajili ofisi za mfuko ambazo ziko katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar, huku akiwataka wananchi hususan wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi leo katika viwanja vya Mnazi mmoja kwenye uzinduzi huo.

Katika hatua nyingine, Konga alisema kati ya Watanzania takribani milioni 50 ni milioni 4.6 pekee ndio wenye bima ya afya ambao ni sawa na asilimia 8.

Konga alisema kiwango hicho cha ukosefu wa bima ya afya kwa Watanzania kinatokana na wengi kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu masulaa ya bima jambo alilosema kuwa ni moja ya mikakati yao inayofuata kuhakikisha kuwa Watanzania wengi zaidi wanaelimishwa.

 “Kiwango cha Watanzania wenye bima ni milioni 4.6 ambacho ni sawa na asilimia 8, hii ikiwa na maana kwamba kati ya Watanzania 100 ni Watanzania nane tu ndio wenye bima ya afya.

 “Hata hivyo tumebaini kuwa hii inatokana na uelewa mdogo kwa wananchi juu ya umuhimu wa bima, jambo ambalo tumepanga kulifanyia kazi kwa maana ya kutoka na kwenda kwa wananchi wenyewe, kwani mpango wetu ni kuhakikisha kuwa hadi kufikia juni 2020, tuwe tumefika asilimia 30 hadi 50 ya Watanzania wenye bima ya matibabu,” alisema Konga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here