23 C
Dar es Salaam
Tuesday, August 16, 2022

Maaskofu watoa ujumbe mzito Krismasi

ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

Maaskofu wa makanisa mawili makubwa nchini, Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wametoa salamu za Sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya wa 2020 huku wakisisitiza ujumbe wa amani na upendo, ambayo msingi wa matunda ya haki.

Katika ujumbe huo wa Krismasi mwaka huu, maaskofu hao, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Thadeus Ruwa’ichi alitaka kuombewa kwaTaifa kuelekea Uchaguzi mkuu wa 2020, wakati Mkuu wa KKKT, Askofu Dk. Gideon Shoo akitaka kuponywa kwA majeraha yaliyotokana na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 24, mwaka huu.

Katika salamu zake, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Ruwa’ichi alisema wakati Taifa lilisherehekea kuzaliwa kwa Masia, Yesu Kristo, Watanzania wanatakiwa kuhimiza na kuombea haki, amani na upendo kuelekea Uchaguzi Mkuu mwakani.

Akizungumza na MTAZNANIA jana, Askofu Ruwa’ichi alisema ujumbe mkuu wa Sikukuu ya kuzaliwa Kristo, yaani Krismasi kama ulivyosambazwa na malaika wakati wa kutangaza kuzaliwa kwake ulikuwa ‘Amani na upendo’ duniani, mambo ambayo msingi wake ni uwepo wa haki.

Alisema wakati Watanzanuia wakimaliza mwaka huu salama, suala la muhimu ni kuhakikisha kila mmoja anavuka salama kwa kuangalia umuhimu wa mapatano, ambapo kwa wale waliokoseana wanatakiwa kuangalia namna ya kuombeana na kila mmoja kumjali mwenzake.

“Mambo haya ni muhimu na tunavuka mwaka na kuingia mwaka 2020, ambao tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu kama Taifa. Suala la muhimu ni kuliombea Taifa, tuhakikishe tunafuata misingi ya haki, nina uhakika tutavuka salama.

“Ninachowasihi watanzania, tusikiuke sheria, kila mmoja awe mtulivu. Kanuni zipo, asiwepo wa kupenda kupata madaraka kwa nguvu, tufuate kanuni na kusimamia haki. Nchi yetu ni nzuri na tukiweka mbele upendo tutavuka salama,” alisema Askofu Ruwa’ichi

Alisema ni jukumu la watanzania na watu wenye mapenzi mema kuombea Taifa na kuombea amani duniani na kwamba ni vyema kuchukuliana kwa upole, kwa kila mmoja kumjali na kumuombea mwenzake, hata pale anapopungukiwa kidogo.

Alisema wakati Wakristo wanaposherehekea kuzaliwa kwa Kristo, wajue kuwa Mwenyezi Mungu amewanuia mema hivyo ni vyema kuhakikisha wanatumia nyakati zao vizuri kwa kukumbuka uwepo wa Mungu, kufuata maagizo na mafundisho yake.

Alisisitiza kuwa maisha yaliyo bora ni yake yanayoheshimu na kulinda amani na kujenga upendo, katika misingi ya kusimamia haki, ili kujenga furaha kuanzia katika ngazi ya familia.

“Lakini ili kuwa na mafanikio na kushuhudia uwepo wa Mungu, yote haya, ya haki, amani na upendo yanatakwia kuanzia kwa mtu mmoja mmoja, kuonyesha juhudi katika kutafuta amani. Hii amani ikiwepo ndiyo inayotupatia furaha kuanzia kwa mtu mmoja, familia na hatimaye Taifa,” alisema.

Askofu Ruwa’ichi alisema ni vyema kutumia nyenzo zote tulizo nazo kuhakikisha kwua tunamfurahisha Mwenyezi Mungu na iwapo kuna mahala inaonekana kuna upuinguvu, nyenzo zilizopo zitumike kuhakikisha amani, upendo na furaha ambavyo msingi wake ni upatikanaji wa haki vinakuwepo.

ASKOFU SHOO

Katika salamu zake za Krismasi kwa Kanisa, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),Dk Gideon Shoo, alisema pamoja na kuuona mkono wa Mungu ukitenda kazi, kwa neema ya Mungu kwamba tumevushwa katika mengi magumu hadi kufikia kipindi cha majira haya na wakati huu wa mwaka.

Alisema katika mwaka huu tunaoelekea kuukamilisha sasa, ni wazi kwamba haukuwa mtelemko na raha tu, bali tumekutana na hali mchanganyiko, akishuhudia baraka nyingi za Mungu, lakini pia magumu na changamoto nyingi za kimaisha.

Askofu Dk Shoo alisema wengine wamepata wakati mgumu hata jinsi ya kulipa gharama za elimu ya watoto wao pamoja na kuwapatia mahitaji mengine muhimu kutokana na changamoto za kiuchumi.

“Lakini zaidi, mwaka huu pia tumeona uchaguzi wa Serikali za Mitaa ukifanyika. Kama kawaida ilivyo kwa nchi nyingi za Afrika uchaguzi huu haukupita bila changamoto. Tumeshuhudia sintofahamu kadhaa katika mchakato mzima jambo lililosababisha tukaingia katika uchaguzi huo bila kuwa na muafaka wa pamoja kwa wadau mbalimbali muhimu, vikiwemo vyama vya siasa na taasisi nyingine.

“Katika hali kama hii na mazingira kama haya ni wazi kwamba kila mmoja wetu angependa kusikia habari njema ya furaha kuu!,” alisema

Alisema mwaka huu amechagua neno kutoka Injili ya Luka, ambapo malaika alitangaza habari njema ya furaha kuu, ambayo hakika ni ya furaha kuu maana ni ya kweli na haina ubaguzi, ambayo ni kwa watu wote.

“Habari ya kuzaliwa kwa Mwokozi wetu Yesu Kristo ni habari njema na ya furaha kuu kwa wote, yaani matajiri na maskini, yatima na wajane, wasomi na wasio wasomi. Tangazo la malaika linatutaka wote kusahau changamoto na magumu yote tuliyokutana nayo mwaka huu na kumtazama Yesu Kristo Mwokozi wetu anayetuletea furaha kuu mioyoni mwetu na maishani mwetu kwa ujumla.

“Furaha kuu ya kwanza tunayoipokea katika Neno hili, ni kwamba Mungu anatupenda na ndiyo maana amemtuma mwanae wa pekee aje kutukumboa toka dhambini. Yaani hii ni furaha ya kweli kwetu sisi, kwamba sasa hatupotei tena, nuru imekuja ulimwenguni na kupitia hiyo nuru yaani Yesu Kristo tunaahidiwa uzima wa milele baada ya kusafishwa dhambi zetu.

“Hivyo wapendwa, katika kusherehekea Siku Kuu za Krismasi mwaka huu nawaalika mpokee habari njema ya furaha kuu, mwokozi wetu Yesu amezaliwa kwa ajili ya wote.

“Anakuja kuleta nuru mahali penye giza, haki pasipo na haki, matumaini mapya mahali tulipokata tamaa, amani mahali penye vita na furaha mahali penye huzuni. Kwa kuwa habari hii njema haina ubaguzi na sisi tusiimiliki peke yetu, tuwatangazie wengine pia kwa furaha na upendo mkuu ili nao washiriki furaha kuu pamoja nasi,” alisema Askofu Dk Shoo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,800FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles