22.7 C
Dar es Salaam
Sunday, June 4, 2023

Contact us: [email protected]

MAANDAMANO KUTIKISA UKUTA MIRERANI

Na MASYAGA MATINYI – SIMANJIRO


WAKATI Rais Dk. John Magufuli  akitarajiwa kuzindua rasmi ukuta wa Mirerani wiki hii, maandamano na mabango yameandaliwa kumpokea.

Lengo la maandamano na mabango hayo ni kutaka wamiliki wa migodi kuwalipa mishahara wafanyakazi wao wanaozama migodini, suala ambalo liliibuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti.

Agizo la kulipa mishahara hilo lilitolewa na Mnyeti, Februari 25, mwaka huu alipozungumza na wamiliki wa migodi   na wachimbaji mjini Mirerani.

Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka wamiliki wa migodi   kuwalipa mishahara wafanyakazi wao kuanzia mwezi uliopita (Machi), na wote watakaoshindwa  wafungashe na kuondoka eneo hilo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Iddi Kondo, ambaye alijitambulisha kama Mwenyekiti wa Chama cha Wazamiaji Migodini Tanzania (CHAWAMITA), alisema wamejipanga kufikisha kilio chao kwa Rais.

Kondo ambaye alikiri kuwa chama chao bado hakijasajiliwa, alisema suala la mishahara ni kilio chao cha muda mrefu, na kudai lengo lao kubwa ni kulipa kodi serikalini kama ilivyo kwa wafanyakazi wa sekta nyingine.

Waratibu wengine wa ‘maandamano’ hayo ambao pia walizungumza kwa nyakati tofauti, ni Jafari Matimba na Emmanuel Makaranga, ambao walidai wamefikia hatua hiyo kutokana na baadhi ya wenye migodi kukiuka makubaliano   unapotokea uzalishaji migodini.

“Ni kweli huwa tuna makubaliano ya kupewa asilimia 10 ya uzalishaji   mgodi unapotoa mawe, lakini kuna wamiliki wengine hukiuka makubaliano   mawe yanapotoka, hivyo kilichobaki tulipwe mishahara,” alisema Makaranga.

Wakati hali ikiwa hivyo, imebainika pasipo shaka kuwa wengi wanaopanga kubeba mabango si wafanyakazi kwenye migodi kama wanavyodai. Hata Mwenyekiti wao Kondo, amedai kufanya kazi katika migodi miwili tofauti.

Uchunguzi zaidi umebaini   wengi wanaopanga kuandamana maarufu kwa majina ya “murere au wanachuchu” (wasiofanyakazi migodini), wanatumiwa na baadhi ya wachimbaji wakubwa kwa malengo ya  biashara.

KAULI YA RPC

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Augustino Senga, alisema Jeshi la Polisi lina taarifa za mpango huo  na linazifanyia kazi.

“Taarifa tunazo na tunazifanyia kazi kuhakikisha ziara ya Rais inafanyika na kukamilika kama ilivyokusudiwa kwa amani… kule machimboni kama ujuavyo kuna mambo mengi.

“Ni kweli kuna wachimbaji ambao wanafanya kazi kwa makubaliano, na hawa hawadai mishahara  na kuna kundi jingine ambalo linadai mishahara, ambamo tunaambiwa wengi si wafanyakazi wa migodini  lakini tunazifanyia kazi hizi taarifa,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, wamiliki wa migodi kupitia chama chao cha Manyara Region Miners Association (MAREMA) wamefanya mikutano kadhaa Mirerani, ambako pamoja na mambo mengine, kwa pamoja, walisema suala la ulipaji wa mishahara haliwezekani kutokana na mazingira ya uchimbaji na biashara ya madini ya tanzanite.

Walisema kwa muda mrefu wamekuwa na utaratibu au mikataba na wafanyakazi wao ambao wanawaita wabia, ambao   mgodi unapozalisha madini, mmiliki huchukua asilimia 90 na wabia huchukua asilimia 10.

WANA APOLO

Wafanyakazi wa migodini (maarufu kama wana-apolo) ambao walizungumza, walisema hawapo tayari kuingia kwenye mkataba wa mshahara  kwa sababu hauwezi kuwanufaisha kwa lolote lile.

Kwa niaba ya wenzake, Amir Mgoo, anayefanya kazi katika mgodi wa mchimbaji Money Yusuf tangu mwaka 1994, alisema kazi wanayofanya ni makubaliano kati yao na wamiliki wa migodi, na kila anayekwenda pale huwa na malengo yake, hata kama itachukua muda mrefu kufikiwa malengo husika.

“Kaka huku hakuna masuala ya ajira au mishahara, ndiyo sababu hata siku moja huwezi kusikia matangazo ya ajira, huku watu tumekuja kutafuta maisha, hatukuja kutafuta Sh 250,000 kwa mwezi.

“Huku tunapiga kazi usiku na mchana, siku mgodi ukitoa mawe, nachukua changu na kutengeneza maisha, lakini nikisema nilipwe mshahara, hata nikifanya kazi kwa miaka 100, nitakufa masikini, kwa hiyo watuache. Ila kama wapo wanaotaka mishahara, kama wapo, basi wazungumze na mabosi,” alisema.

Katibu wa Chama cha Wachimbaji Mkoa wa Mannyara (MAREMA), Abou Madiwa, amesema wamiliki wa migodi wenye leseni ndogo zijulikanazo kama Primary Mining Licence (PML) au wachimbaji wadogo, kwa uhalisia wa mambo hawawezi  kulipa mishahara.

“Kwanza hatuna mitaji, na hata Serikali yetu kwa maana ya Wizara ya Madini ni shuhuda katika hili.

“Kwa miaka mingi tumekuwa tukiomba iangalie utaratibu wa kutupatia mitaji na utaalamu (teknolojia), haya yote yanadhihirisha uduni wetu.

“Mifano ni mingi, unaweza kukuta mchimbaji mdogo anajinyima kiasi hata cha kuuza mali zake kama mashamba  aweze kuhudumia mgodi.

“Wakati mwingine mtu anapambana kwa zaidi ya miaka 10 bila kupata hata jiwe moja. Sasa mmiliki kama huyu anatoa wapi fedha za kulipa mishahara wafanyakazi?

“Ndiyo maana wale tunaofanya nao kazi kwenye migodi yetu huwa hatupendi kuwaita wafanyakazi, badala yake tunawaita wabia, kwa sababu kinachofanyika pale ni mjumuisho wa nguvu za kila mmoja.

“Mimi mwenye mgodi natafuta fedha kuhudumia mgodi kuhakikisha chakula, maji, dizeli na mashine vinapatikana, na wabia wangine wanachangia nguvu kazi, siku tukizalisha basi tunagawana kwa mujibu wa makubaliano, na makubaliano haya yanafahamika mpaka Ofisi ya Madini ya Kanda.

Ujenzi wa ukuta huo umekamilika katika eneo lote lenye urefu wa kilometa 24.5 na hatua iliyofikiwa sasa ni kukamilisha mambo madogo madogo yanayolenga kuimarisha ulinzi na ukuta huo.

Ukuta huo umejengwa kwa gharama ya  Sh bilioni 5.6.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,283FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles