30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi yafikia asilimia 95

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Serikali imesema maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi yamefika zaidi ya asilimia 95 hivyo ni vyema kuendelea kushirikiana kwa pamoja kwa kuzingatia muda uliobaki ili kulifikia lengo lililopo.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu), Dk. John Jingu akitoa utambulisho wa washiriki wa mkutano huo.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene katika Mkutano Maalum wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alipokutana na sekta binafsi kwa lengo la kutambua mchango wao katika kuelekea siku hiyo ikiwemo ya rasilimali fedha, huduma na vifaa kwa ajili ya zoezi la Sensa ya watu na makazi ya Mwaka 2022.

Amesema kuwa, Serikali inatambua mchango wa sekta binafsi hivyo ni vyema kwa kila mdau kushirikia katika zoezi hili  kwa kadri awezavyo kwa kuchangia  rasilimali fedha, huduma na vifaa vitakavyosaidia kufanikisha zoezi la sensa.

“Karibu kila mdau ameshiriki katika maandalizi ya sensa kupitia taasisi ya sekta binafsi (TPSF) na tumekutana hapa ili kuonesha mshikamano wetu na kutambua michango yenu ninawapongeza sana,” amesema Simbachawene.

Naye katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Dk. John Jingu amesema serikali imeshirikiana sekta binafsi  katika maandalizi ya kuelekea siku ya sensa kwa namna mbalimbali ikiwemo, kugharamia matangazo yanayotoka kwenye vyombo vya habari.

“Kampuni za simu zilisaidia kutoa ujumbe mfupi wa kuhamasisha wananchi na kuelimisha wananchi juu ya zoezi la sensa ya watu na makazi na baadhi kuahidi kuchangia fedha na vifaa mbalimbali ili kufanikisha zoezi la sensa ya watu na makazi,” amesisitiza Dk. Jingu

Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Anne Makinda akitoa neno la shukrani wakati wa mkutano huo.

Naye Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Spika Mstaafu Anne Makinda ameshukuru sekta binfasi kwa mchango wao katika kuwezesha maandalizi ya kuelekea siku ya sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu.

“Tumejipanga kusimamia matumizi yote tunayopewa na kuhakikisha tunapata matunda tunayotegemea,” amesema Makinda.

Matukio katika picha wadau mbalimbali wa sekta binafsi wakiwa katika mkutano uliohusu uchangiaji wa rasilimali kwa ajili ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 uliofanyika katika kituo cha Mikutano cha kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles