Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Serikali imesema maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi yamefika zaidi ya asilimia 95 hivyo ni vyema kuendelea kushirikiana kwa pamoja kwa kuzingatia muda uliobaki ili kulifikia lengo lililopo.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene katika Mkutano Maalum wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alipokutana na sekta binafsi kwa lengo la kutambua mchango wao katika kuelekea siku hiyo ikiwemo ya rasilimali fedha, huduma na vifaa kwa ajili ya zoezi la Sensa ya watu na makazi ya Mwaka 2022.
Amesema kuwa, Serikali inatambua mchango wa sekta binafsi hivyo ni vyema kwa kila mdau kushirikia katika zoezi hili kwa kadri awezavyo kwa kuchangia rasilimali fedha, huduma na vifaa vitakavyosaidia kufanikisha zoezi la sensa.
“Karibu kila mdau ameshiriki katika maandalizi ya sensa kupitia taasisi ya sekta binafsi (TPSF) na tumekutana hapa ili kuonesha mshikamano wetu na kutambua michango yenu ninawapongeza sana,” amesema Simbachawene.
Naye katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Dk. John Jingu amesema serikali imeshirikiana sekta binafsi katika maandalizi ya kuelekea siku ya sensa kwa namna mbalimbali ikiwemo, kugharamia matangazo yanayotoka kwenye vyombo vya habari.
“Kampuni za simu zilisaidia kutoa ujumbe mfupi wa kuhamasisha wananchi na kuelimisha wananchi juu ya zoezi la sensa ya watu na makazi na baadhi kuahidi kuchangia fedha na vifaa mbalimbali ili kufanikisha zoezi la sensa ya watu na makazi,” amesisitiza Dk. Jingu
Naye Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Spika Mstaafu Anne Makinda ameshukuru sekta binfasi kwa mchango wao katika kuwezesha maandalizi ya kuelekea siku ya sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu.
“Tumejipanga kusimamia matumizi yote tunayopewa na kuhakikisha tunapata matunda tunayotegemea,” amesema Makinda.