25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Maambukizi ya Covid-19 yaongezeka Afrika

 ADDIS ABABA, ETHIOPIA

MAAMBUKIZI ya ugonjwa wa Covid-19 au corona barani Afrika yanaongezeka kwa kasi na hadi kufikia Jumapili, waliokuwa wameabukizwa ugonjwa huo barani humo walikuwa ni 828,214.

Kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa Barani Africa (Africa-CDC) hadi sasa waliofariki kutokana na Covid-19 barani Afrika ni 17,509 katika nchi 54 barani humo.

Eneo la Kusini mwa Afrika ndilo ambalo limeathiriwa vibaya zaidi likiwa na visa 452,000 vya maambukizi ya Covid-19 likifuatiwa na eneo la Kaskazini mwa Afrika lenye kesi, 147,500 huku eneo la Magharibi mwa Afrika likirekodi kesi, 118,400, Afrika Mashariki kesi 65,000, na eneo la Kati mwa Afrika ni la mwisho likiwa na kesi 45,300.

Wakati huo huo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema zaidi ya wahudumu wa afya 10,000 wameambukizwa virusi vya corona barani Afrika.

Hata hivyo, idadi kamili ya watu walioambukizwa barani Afrika huenda ikawa ni ya juu zaidi tofauti na inavyoripotiwa kutokana na uhaba wa zoezi la kuwapima watu na kutokuwepo upimaji na data kamili.

Kwa ujumla takwimu zinaonyesha kuwa, idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona kote duniani imepindukia milioni 16.2 huku zaidi ya watu laki 6.48 wakiwa wameshaaga dunia hadi sasa kufuatia kuugua Covid-19.

Marekani imeendelea kuwa mhanga mkuu wa virusi vya corona ulimwenguni ambapo hadi sasa zaidi ya watu milioni nne wameambukizwa virusi hivyo nchini humo huku karibu watu 150,000 wakiwa wameshafariki dunia.

Brazil ni ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya maambukizi ya corona ambapo hadi sasa imesajili kesi karibu milioni 2.5 ambapo India inafuata katika orodha hiyo kwa kuwa na maambukizo karibu milioni 1.5 ya virusi vya corona.

Kwa mujibu wa takwimu za shirika la habari la AFP, zaidi ya nusu ya maambukizi hayo duniani yameripotiwa katika bara la Amerika na nchi za Carribean.

WHO pia lilisema maambukizi yanaendelea kuenea kwa kasi duniani kote.

Katika hatua nyingine, watalii raia wa Uingereza wanaorudi nchini mwao kutoka Hispania wamekasirishwa na uamuzi wa ghafla wa serikali yao kuwalazimisha kukaa karantini kwa muda wa siku 14.

Uamuzi wa Uingereza kuiondoa Uhispania katika orodha ya nchi salama ulitangazwa juzi Jumamosi, na kuwaacha njia panda wasafiri wanaoingia Uingereza.

Utawala wa Waziri Mkuu, Boris Johnson umekosolewa vikali kwa uamuzi huo ambao umechukuliwa baada ya idadi ya maambukizi ya virusi vya Corona kupanda nchini Uhispania.

Hispania ilikuwa kwenye orodha ya nchi salama, hatua hiyo ikimaanisha kuwa sio lazima kwa wasafiri wanaotokea nchini humo na kuingia Uingereza kukaa karantini.

Hata hivyo kufuatia ongezeko la maambukizi ya Covid-19 nchini humo, imelazimu baadhi ya miji kama vile Barcelona kuweka tena sheria za kuwalazimu watu kuvaa barakoa na kuwataka watu kusalia majumbani.

Huko Korea Kaskazini, Kiongozi wa nchi hiyo, Kim Jong Un ametangaza hali ya dharura pamoja na kuweka vizuizi katika mji wa mpakani wa Kaesong baada ya mtu mmoja kudhaniwa kuwa na virusi vya corona.

Chombo cha habari cha serikali KCNA kimeripoti kuwa mtu huyo alivuka mpaka kwa njia isiyo halali akitokea Korea Kusini.

Shirika la habari la serikali limeripoti kuwa mtu huyo anayedhaniwa kuwa ameambukizwa virusi vya corona aliiasi Korea Kaskazini miaka mitatu iliyopita na kukimbilia Korea Kusini.

Taarifa zilisema kwamba alivuka mpaka wa Kaesong kinyume cha sheria Julai 19, 2020 na kuingia nchini Korea Kaskazini akiwa na dalili za virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

Iwapo mtu huyo atapimwa na kuthibitishwa kuwa na virusi hivyo, atakuwa ni wa kwanza kuwa na maambukizi ya virusi vya corona kwenye ardhi ya Korea Kaskazini.

Kim Jong Un ameitisha mkutano wa dharura kujadili kadhia hiyo kutokana na wasiwasi kwamba huenda maambukizi ya virusi vya corona yakawa yameingia nchini mwake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles