Anna Potinus
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi saba duniani ambazo zimefikia malengo ya mkakati wa kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu (TB) kufikia mwaka 2020 na kwamba katika mwaka 2018 maambukizi mapya yamepungua kwa kasi ya asilimi 4.6.
Ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Novemba 7, alipokuwa akifungua mkutano wa mawaziri wa afya nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo amesema kuwa vifi vinavyotokana na ugonjwa huo vimepungua kwa asilimia 27.
“Vifo vinavyotokana na TB vimepungua kutoka vifo 55,000 kwa mwaka 2015 hadi 39,000 kwa mwaka 2018 ambayo ni sawa na asilimia 27 aidha utoaji wa taarifa za wenye TB umeongezeka kwa asilimi 20.6 katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2018 hii inatokana na kuongezeka kwa kiwango cha utambuzi wa ugonjwa huu kutoka asilimia 39 mwaka 2015 lakini kimekua hadi asilimi 53 mwaka 2018.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye kiwango cha chini cha usugu wa dawa za TB kwa kuwa na asilimia 0.3 ya usugu kwa wenye maambukizi mapya na asilimia 13 kwa wagonjwa waliotibiwa, hadi kufikia Septemba mwaka huu vituo 103 nchini vinatoa huduma ya tiba kwa wagonjwa wenye TB sugu ikilinganishwa na kituo kimoja mwaka 2015.
“Waheshimiwa mawaziri mtakapojadili kuhusu virusi vya ukimwi naomba mtambue kuwa Tanzania imefanikiwa kupunguza maambukizi mapya kwa kiwango cha asilimia 20.6 kutoka mwaka 2015 hadi 2018 kwa walio na umri zaidi ya miaka 15 na asilimia 31.3 kwa walio chini ya umri wa miaka 15,” amesema Makamu wa rais.
Aidha ameongeza kuwa Tanzania imeweka mikakati ya kuhakikisha wanafikia malengo yake kwa kufanyia marekebisho sheria ya kuruhusu watu kutumia vifaa vya kujipima wenyewe kwani kwa kufanya hivyo kutapelekea watu wengi kuamua kujipima wenyewe kwanza lakini baada ya kufanya hivyo watatakiwa kwenda vitu vya afya kuthibitisha.