MWANDIUSHI WETU – DODOMA
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema maambukizi ya kifua kikuu (TB) yamepungua nchini kutoka wagonjwa 164,000 mwaka 2015 hadi kufikia 142,000 mwaka 2018.
Ummy alisema hayo juzi wakati akikabidhi hadubini 57 zitakazotumika kufanya vipimo vya ugonjwa wa kifua kikuu ambazo zitasambazwa hospitali na vituo vya afya mkoani hapa.
“Leo nimeanza zoezi la kukabidhi hadubini 941 zilizonunuliwa na Serikali kwa ufadhili Taasisi ya Global Fund zenye thamani ya Sh bilioni 3.3 ambapo leo (jana) nitamkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma hadubini 7 za Wilaya ya Chamwino zitakazosambazwa katika vituo vya afya mbalimbali,” alisema Ummy.
Pamoja na hayo, Ummy alitumia muda huo kueleza mafanikio yaliyofikiwa na Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma ikiwa ni pamoja na kupungua maambukizi mapya kwa asilimia 18, lengo likiwa ni asilimia 20 na vifo vimepungua kwa asilimia 27 lengo likiwa ni asilimia 35.
Aidha alisema ugunduzi wa kifua kikuu unaendelea kuimarika ambapo idadi ya wagonjwa waliogundulika na kuwekwa kwenye matibabu imeongezeka kutoka 62,180 mwaka 2015 hadi kufikia 82,140 mwaka jana.
Kwa upande wa vituo vya ugunduzi wa tiba, Ummy alisema katika kipindi cha miaka mitatu vituo vimeongezeka kutoka 662 mwaka 2016 hadi kufikia 1,201 mwaka jana.
Katika kipindi cha miaka mitatu idadi ya wagonjwa waliogundulika kuwa na kifua kikuu imepungua kutoka 164,000 mwaka 2015 hadi 142,000 mwaka 2018.