26.8 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

Maambukizi homa ya ini yaongezeka

AVELINE KITOMARY -DAR ES SALAAM

MAAMBUKIZI ya ugonjwa wa homa ya ini (Hepatitis B) yameongezeka nchini, huku ikielezwa kuwa wananchi wengi bado hawana uelewa juu ya ugonjwa huo.

 Hayo yalibainishwa katika kongamano la madaktari na wauguzi lililofanyika Hospiatali ya Taifa ya Muhimbili jana.

 Daktari bingwa wa homa ya ini, Dk. John Rwegasha, alisema utafiti unaonesha kiwango cha homa hiyo kimeongeza na vyanzo vikuu vya kasi hiyo ni kujamiiana na maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

“Takwimu zilizotolewa na Shirika la Utafiti la Taifa zinaonesha maambukizi ya homa ya ugonjwa wa ini yamefikia asilimia 4.5, huku jamii ikiwa haina uelewa wa kutosha kuhusu ugonjwa huo,” alisema Dk. Rwegasha.

Alisema virusi vya ugonjwa huo vinaweza kukaa ndani ya mwili kwa muda mrefu, hivyo endapo mgonjwa atachelewa kutibiwa, unaweza kuwa sugu na kusababisha kifo.

“Hepatitis B na C zote zina madhara, ni ugonjwa sugu ambao unaweza kukaa ndani ya mwili zaidi ya miaka 20, ukichelewa kuutibu kuna madhara makubwa, hata kusababisha kifo,” alisema Dk. Rwegasha.

Alisema licha ya chanjo kupatikana hospitali zote, lakini bado watu hawajitokezi kupata huduma hiyo hali inayosababisha madhara kuongeza.

“Huduma ya chanjo ipo kwa hospitali zote, lakini bado watu hawajitokezi kwa wingi, nafikiri hii ni kutokana na uelewa mdogo kuhusu ugonjwa huo.

“Hata hivyo kwa sasa Shirika la Afya Duniani  (WHO) linapendekeza chanjo itolewe kwa watoto mapema ili kudhibiti maambukizi au mama mjamzito kama ana maambukizi anaweza kutumia dawa ili asiweze kumwambukiza mtoto,” alieleza Dk. Rwegasha.

Alisema Serikali kupitia Wizara ya Afya, ina mpango wa kuwekeza kwenye vipimo na utoaji wa dawa kwa ugonjwa huo kwani vipimo kwa sasa ni changamoto kwa hospitali nyingi.

“Ingawa kuna dawa na chanjo, changamoto ni vipimo bado havijaweza kufika katika hospitali zote na bei ya vipimo kwa hospitali za binafsi ni kubwa, kipimo tu ni Sh 500,000 hadi kupona unaweza kufikia hata Sh milioni 2,” alisema.

Dk. Rwegasha alitoa wito kwa jamii kujitokeza kupata chanjo ya ugonjwa huo ili kudhibiti maambukizi  mapya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles