30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif, Zitto watua kwa kishindo Z’bar

Na FREDY AZZAH   -ZANZIBAR

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ameanza ziara visiwani Zanzibar ikiwa ni mara ya kwanza tangu ajiunge na ACT-Wazalendo, huku Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe, akisema baadhi ya waliokuwa viongozi waandamizi wa Serikali ya CCM wamewapongeza na sasa wanawakaribisha waunganishe nguvu.

Zitto aliyasema hayo jana mjini Unguja wakati wa hafla ya kumkaribisha Maalim Seif, iliyofanyika katika ofisi za ACT-Wazalendo Vuga, ambazo awali zilikuwa za CUF.

Katika hafla hiyo, Maalim Seif ambaye leo atafanya ziara visiwani Pemba ambako ndiko kwenye ngome yake, hakutaka kuzungumza zaidi ya kusalimia wafuasi wake kwa salamu ya ACT, huku akisema kwa siku mbili zilizopita alizungumza sana.

Akizungumza na waandishi wa habari, Zitto alisema chama chao hakina ugomvi na dola bali kinataka demokrasia, haki ya kukosoa na kupongeza pale inapobidi.

Alisema kwa sasa haki hizo zimeminywa na uwepo wao pamoja na wageni waliowapokea kutoka CUF, ni zao la ukandamizaji unaofanywa dhidi ya haki za watu kufanya siasa.

“Wito kwa watu wote ambao wameshawishika na safari hii, tayari tumepokea simu na ujumbe mbalimbali kutoka kwa watu ambao wengine walikuwa wakubwa kwenye Serikali ya CCM, wameridhika na hili.

“Wamechoshwa na siasa za kuburuzwa, wanataka kuona uchumi wa nchi unaimarika, wanaona kuna matumaini kwa tunayofanya, sasa tunapoendelea tunawakaribisha,” alisema Zitto.

Alisema chama chao hakibagui watu kutokana na vyama vyao wala itikadi na kwamba wote wanakaribishwa kufanya nao kazi.

Zitto pia alisema kuna wafanyabiashara ambao wanavutiwa na chama hicho, lakini wanaogopa kujiunga nao hadharani, hivyo kuwataka wafanye kimyakimya.

Aliwataka wafuasi hao kutokata tamaa kwa yaliyotokea ndani ya chama chao cha awali na badala yake yaliyowakuta yawe chachu ya kusonga mbele.

“Wazanzibar hii si mara ya kwanza kuanza upya, yaliyopita yatupe ujasiri wa kusonga mbele siyo kutufanya tuwe wanyonge,” alisema Zitto.

Waandishi wa habari walipotaka kujua kama dhima ya ACT kuhusu Zanzibar ni sawa na ile ya CUF, alisema tangu awali chama chake kwenye masuala ya Zanzibar kilikuwa hakitofautiani na vingine vya upinzani.

Alisema moja ya masuala hayo ni mfumo wa Muungano ambao wao wanaamini katika Tume ya Jaji Warioba iliyokuja ma mfumo wa Serikali tatu.

“Lazima tuwe na Muungano wenye usawa, tunataka Zanzibar ichukue nafasi yake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini pia Tume ya Jaji Warioba ni sehemu muhimu ya kuanzia,” alisema Zitto.

Baada ya mkutano huo, viongozi hao waligawa kadi za chama kwa wanachama wapya ambao wengi walikuwa CUF.

WARUSHIWA MCHELE

Katika kile kilichoelezwa kuwa ni utaratibu wa kizanzibar, Maalim Seif alipoingia katika eneo la Vuga, wakinamama walimlaki kwa vigelegele huku wakimrushia mchele.

“Kurusha mchele ni kama mila, unamrushia mtu aliye kwenye moyo wako, kwa mfano hata kwenye harusi bibi harusi akipendeza ndugu wanamrushia mchele ili kumwepusha na husda ama jicho baya,” alisema mmoja wa wanachama hao.

Pia Zitto alipofika hapo na kulakiwa na Maalim Seif aliyefika eneo hilo dakika 40 kabla, naye alipokewa kwa kurushiwa mchele.

WAFUNDISHWA SALAMU YA ACT

Moja ya kazi kubwa aliyokuwa nayo mshereheshaji wa shughuli hiyo kabla ya viongozi kufika, ni kuwafundisha wafuasi hao salamu ya ACT.

Wengi walionekana kutojua kuitikia salamu ya ACT, ambapo badala ya kuitikia ‘Taifa kwanza’ wengi walikuwa wakisema ‘Wazalendo’.

WAOMBA MSAADA

Katika hatua nyingine, chama hicho kimeanza kampeni ya kuchangisha fedha ili kiweze kuendelea na ziara zake na kujenga chama.

“Wakati chama chetu kikiwa kinaendelea kukaribisha wanachama, viongozi na wanachama waandamizi watakuwa na ziara katika mikoa kadhaa nchini, tunaomba michango yenu ya hali na mali, kufanikisha safari hii ya kuhamasisha wananchi kuelekea makubwa ya kisiasa na kiuchumi,” alisema.

Hiyo ni ziara ya kwanza ya Maalim Seif tangu atangaze kujiunga na ACT-Wazalendo hasa baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kumpa ushindi Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba kwa kukubaliana na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kumtambua kiongozi huyo.

Hatua hiyo ya Maalim Seif kutangaza kujiunga na ACT-Wazalendo iliamsha ari kwa baadhi ya waliokuwa wanachama wa CUF kutangaza kuungana nae huku ofisi zikibadilishwa rangi na bendera kushushwa na kupandishwa za chama chao kipya.

Pia baadhi ya wanachama waliokuwa CUF waliamua kuachana na chama hicho kwa kuchoma bendera na sare hadharani ikiwa ni hatua ya kugomea kuwa chini ya Profesa Ibrahim Lipumba.

Kutokana na matukio hayo, Mwenyekiti wa CUF Profesa Lipumba alitoka hadharani na kuonya watu wanaochoma bendera za chama hicho kwa kusema kuwa wanafanya makosa ya jinai kwa mujibu wa sheria.

Tamko hilo la Lipumba pia lilifanya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Thobias Sedoyeka kusema kuwa pamoja na baadhi ya wafuasi wa CUF kushusha bendera na kupandisha za Chama cha ACT- Wazalendo, wajue kwamba wanavunja sheria za nchi.

Alisema licha ya shughuli hiyo kuendelea katika maeneo mbalimbali, lakini alitahadharisha wafuasi hao watekeleze shughuli zao hizo kwa kufuata sheria za nchi pamoja na utaratibu na kanuni za uendeshaji wa vyama vya siasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles