23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif: Wema wangu umeniponza

Na FREDY AZZAH-ZANZIBAR

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema walianza kutafuta chama mbadala miezi minne kabla mahakama haijatangaza kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kama mwenyekiti halali wa chama hicho.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Maalim Seif, ambaye wiki hii amejiunga na Chama cha ACT- Wazalendo, kinachoongozwa na mwanasiasa kijana, Zitto Kabwe, amesema tangu awali waliona kila dalili kwamba mgogoro ndani ya chama hicho umepandikizwa na dola.

Maalim Seif, ambaye amekuwa CUF kwa miaka 27 tangu aliposhiriki kukiasisi chama hicho mara tu baada ya kutoka gerezani alikokaa takribani miaka mitatu (1989-1991), amesema kutokana na hali hiyo, waliamua kufungua kesi mahakamani wakiamini watapata haki, lakini waliona baadhi ya mambo yaliyokuwa yakifanyika wakajua kabisa dola ipo kazini.

“Katika chama cha siasa wakati wote lazima ufikirie mbadala, tulikuwa na mgogoro tangu mwanzo, tulijua umepandikizwa na dola, tukaamua kwenda mahakamani tukiamini mahakama itatenda haki.

 “Wakati tunaendelea tukaona dola wanaunga mkono upande wa pili, kwa mfano msajili aliandika barua ya kuzuia kabisa ruzuku mpaka mgogoro umalizike, lakini upande wa pili akawa anawapa ruzuku.

“Pia upande wa pili wanapanga kufanya mkutano mkuu, mimi kwa chama ninachokijua, taratibu za mkutano mkuu huitishwa bila baraza kuu, ndilo linapanga ratiba, kuchukua fomu na uchaguzi, lakini tukaona Ofisi ya Msajili inabariki yote haya, tukaona hapa kuna jambo.

“Suala jingine ni kesi kupigwa danadana, kesi iliyoamuliwa  Machi 18, mwaka huu ilifunguliwa 2016, yote haya yakawa yanatoa taswira kwamba kuna mkakati.

“Kwa hiyo tangu mwanzo tulikuwa na wasiwasi, lakini tukaamua kupambana, kwa hiyo naweza kusema tangu miezi minne iliyopita ndio tukaanza ‘serious’ kujadili hili la kuhama, mwisho uongozi wa Baraza Kuu la Taifa wakasema ikifika hakuna budi kuhama, Baraza Kuu linakabariki,” anasema Maalimu Seif, ambaye kabla ya kuunda CUF alitimuliwa CCM yeye na wenzake 17.

Akifafanua zaidi kwanini waliamua kwenda ACT na si chama kingine, amesema: “Wakati tunafikiria chama kingine, tuliona bora tupite kwenye baadhi ya vyama, tuwasikilize wako tayari kiasi gani kutupokea kama tukiamua kufanya hivyo, tulipita vyama vyote vinavyounda Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) na ambavyo havikuwa huko, ingawa nao walishapeleka maombi ya kujiunga.

“Katika kufanya hilo, tuliangalia katiba ya vyama hivyo, ‘flexibility ya katiba hizo, sera zao, itikadi na uongozi uliopo, taswira yake ikoje kwa umma na tunaweza kufanya nao kazi kwa namna gani.

“Vyama vyote vilitukaribisha, vyote ni vizuri, lakini hata kati ya vizuri pia kinachagulika kimoja. Na hata ukivipa alama basi ACT- Wazalendo wanachukua nafasi kubwa.

“Baada ya timu yetu kutembelea na kuomba, baadaye walirudi wote kuwashukuru hata kabla hatujachagua ACT,” anasema Maalim Seif.

Kosa gani la kisiasa analijutia

Maalim Seif, ambaye amekuwa kwenye mikiki mikiki ya siasa  za upinzani kwa takribani miaka 27 kabla ya kutimuliwa CCM na wenzake, amesema kwenye maisha yake ya siasa, jambo analojutia ni kumwamini kila mtu aliyekuwa anakwenda kwake na wengine sasa ndio wamewafikisha walipo leo.

“Kosa kubwa ni kumwamini kila mtu, wakati mwingine mtu anakuja wenzako wanakwambia si mtu mzuri, mimi nasema acha athibitishe mwenyewe kwamba ni mzuri ama la wakati mwingine ndio hawa wametufikisha huku,” anasema.

Sijafuata vyeo

Kutokana na aina ya siasa anazozifanya na ambazo kimsingi zimemvika taswira ya kitaasisi, Maalim Seif anasema yeye ndani ya ACT-Wazalendo hajafuata vyeo na kwamba hata akiwa mwanachama wa kawaida atafanya kazi yake vyema.

“Kwanza nitapata muda wa kupumzika na kujipanga, hata pengine nikibaki tu kuwa mshauri naweza pia fanya vizuri tu na kuwa na ushawishi, kwa hiyo kikubwa huku sisi tumetafuta jukwaa la kufanyia siasa na si vyeo,” anasema.

Ameeleza kuwa, jukwaa hilo linawasaidia kudai haki na kusimamia anachoamini na kwamba kama angetaka cheo zaidi asingetoka serikalini.

“Lakini niliona si vyema kusaliti wenzangu katika kudai haki, hilo ndilo kubwa kwangu,” anasema Maalim Seif.

Tofauti ya Zitto na wengine

Kuhusu tofauti anayoiona yeye kati ya Zitto na viongozi wengine wa upinzani, amesema wote ni wazuri, ingawa Zitto na chama chake pamoja na uchanga wao wanajua kujenga hoja.

 “Naona wote ni wazuri, pamoja na udogo wao na uchanga wao wewe mwenyewe ni shahidi jinsi wanavyoibua mambo mazito kwenye nchi hii, Zitto si mropokaji, anafanya kwanza utafiti akipata uhakika anasema, hata kama anajua wenye nguvu na mamlaka hawapendi na hiyo kaambukiza wengine wanaomfuata,” anaeleza Maalim Seif.

Aidha, anasema anaamini ACT-Wazalendo hakutakuwa na majungu wala makundi kama alikotoka na kwamba wao wanawaheshimu hata walioshiriki kuanzisha chama hicho na baadaye kuamua kujiunga na CCM.

“Kabla ya kwenda sisi kuna watu walikuwa waanzilishi, wakaamua kuacha jahazi na kwenda chama kinachotawala, jambo ambalo ni zuri, kwasababu ukiona hapa kuna sehemu nyingine nzuri ni jambo zuri sana.”

Lowassa hakuniaga, sikumuaga

Katika hatua nyingine, Maalim Seif, ambaye alipeperusha bendera ya Ukawa Zanzibar wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, huku Edward Lowassa, akipeperusha bendera hiyo Zanzibar, anasema alipochukua uamuzi wa kwenda ACT hakumuaga mwenzake huyo ambaye alihamia CCM kwasababu na yeye hakuagwa.

“Sisi tumetangaza juzi kuhama, mwenzangu huyo mzee mwenzangu nilisoma tu kwenye magazeti kwamba kahama, kwa hiyo sikuona sababu na mimi wakati wa kuondoka nimwambie.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles