Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, amesema si aibu kwa nchi kupata msaada kutoka nje kuchunguza tukio la kushambuliwa kwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Aidha, amesema anaunga mkono kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, kwamba vyombo vya ndani vinaweza kufanya hivyo na kuongeza kuwa ni muhimu wananchi waambiwe kinachoendelea.
“Nadhani ni vizuri wananchi wakaona matokeo yake kwa sababu hatujaambiwa hasa nini kinaendelea, si vibaya kupata msaada toka nje, hiki ndicho kinatokea duniani huko,” amesema Maalim Seif wakati akihojiwa na Radio Deustche Welle (DW) ya Ujerumani, leo.
Hata hivyo, Maalim Seif ambaye jana alimtembelea Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu hospitalini Nairobi kumjulia hali, amesema waliomshambulia kwa risasi hawajawamrudisha nyuma katika kuwatetea wanyonge.
“Anaendelea vizuri licha ya kupigwa risasi zote hizo vile vile yuko timamu, anazungumza vizuri yuko makini na anajua anachokisema, mimi nimepata moyo sana baada ya kuzungumza naye.
“Sidhani kama Watanzania tumefikia hapo, lazima kama taifa lazima tuzungumze katika mjadala wa kitaifa tujue tumekosea wapi na wapi turekebishe,” amesema Maalim Seif.