30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MAALIM SEIF, SERIKALI WALAANI KUPIGWA WAANDISHI

NA MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


SIKU chache baada ya kutokea kwa vurugu zilizosabisha kujeruhiwa kwa waandishi wa habari katika mkutano wa Chama cha Wananchi (CUF), Serikali pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, wamelaani tukio hilo.

Mbali na vyombo hivyo, pia Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amelaani tukio hilo.

Kutokana na hali hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dk. Hassan Abbasi, alisema uandishi wa habari ni taaluma adhimu na nadhifu inayopaswa kuheshimiwa, kuenziwa, kulindwa na kutoingizwa katika migogoro ya pande zinazofarakana katika jamii.

“Serikali imepokea kwa masikitiko taarifa za kushambuliwa na kujeruhiwa baadhi ya waandishi wa habari katika mvutano uliotokea Dar es Salaam kati ya wafuasi wa pande mbili zinazokinzana za CUF.

“Tumechukua muda kidogo kulifuatilia suala hili na kubaini licha ya baadhi ya waandishi kujeruhiwa na kuripoti polisi, wapo ambao vifaa vyao vya kazi vililengwa katika shambulizi hilo,” alisema Dk. Abbasi.

Aliainisha baadhi ya vifungu vya sheria vinavyomlinda mwanahabari katika kazi yake kama vile kifungu cha 7 (1) (a) cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016, ambacho kinaainisha uhuru wa wanahabari katika kukusanya habari kwa muktadha wa kuwapo katika maeneo ya matukio kama hakuna sababu nyingine za kuzuiwa.

Alisema pia misingi ya uhuru huo wa kitaaluma imesisitizwa katika Ibara za 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na  Ibara ya 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 ambao nchi yetu imeuridhia, hivyo wananchi wanatakiwa kuheshimu hilo.

 

MAALIM SEIF

Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema kitendo cha kuwavamia, kuwashambulia na kuwajeruhi waandishi wa habari kwa kutumia silaha za jadi na moto, si cha kiungwana na hakiashirii nia njema, uvumilivu na uendeshaji wa siasa za kistaarabu hapa nchini.

Alilitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua stahiki za kisheria kwa kuwakamata wahusika wote na kuwafikisha                                       mahakamani haraka iwezekanavyo.

“Tukio hilo linapaswa kulaaniwa na kila mpenda haki, amani na ustawi wa demokrasia nchini na utawala wa sheria.

“Jeshi la Polisi lina wajibu wa kuwakamata mvamizi aliyewatolea bastola waandishi wa habari na wanachama waliokuwepo ukumbini wakati huo na wasisubiri hadi yatokee maafa makubwa zaidi,” alisema Maalim Seif.

 

JAJI MUTUNGI

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amelaani vurugu zinazodaiwa kufanywa na wafuasi wa pande hizo mbili za CUF zinazokinzana na kusababisha baadhi ya waandishi wa habari kushambuliwa na kujeruhiwa wiki iliyopita.

Jaji Mutungi alisema kama mgogoro huo utaendelea, hatasita kuchukua hatua stahiki za kisheria kwa chama hicho.

Katika taarifa yake iliyotumwa kwa vyombo mbalimbali vya habari jana, Jaji Mutungi alisema kuwapo kwa shauri mahakamani si fursa ya kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani, kwani jambo hilo linaleta sura mbaya kwa jamii.

“Suala la mgogoro wa uongozi CUF lipo mahakamani, lakini nikiwa msimamizi wa Sheria ya Vyama vya Siasa na kutambuliwa na jamii kuwa ni mlezi wa vyama vya siasa,  ninalaani vurugu hizo, ambazo zilionekana kuvunja amani na utulivu na watu kuumizwa tofauti na tunu zetu za taifa za amani na utulivu.

“Nawaasa wanachama wa CUF pamoja na tofauti walizonazo tuheshimu utawala wa sheria,” alisema Jaji Mutungi.

Aliviasa vyama vya siasa kuelewa kuwa havipo juu ya sheria, hivyo vinapaswa kuheshimu na kufuata sheria za nchi, ikiwamo kutunza amani na utulivu uliopo.

Msajili huyo pia aliviomba vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza tukio hilo ili wahusika wafahamike na kuchukuliwa hatua za kisheria.

 

CUF, POLISI WATETA

Viongozi wa CUF, jana walikutana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, kujadili kuvamiwa na kupigwa kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho mwishoni mwa wiki iliyopita.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamishna Sirro,  alisema kitendo hicho ni kinyume na sheria na kwamba kinapaswa kulaaniwa na wahusika waweze kuchukulia hatua za kisheria.

Alisema kinachofanyika ndani ya chama hicho ni mgawanyiko wa viongozi ambapo kuna CUF A na B na kila upande una kiongozi wake wanaomtii, jambo ambalo limesababisha wengine kujichukulia sheria mkononi kinyume na sheria na kuanza kufanya vurugu, kupiga na kujeruhi wananchi.

“Hatuwezi kuvumilia vitendo vinavyofanywa na wanachama wa CUF kwa sababu ni kinyume na sheria na kwamba kinapaswa kukemewa, kulaaniwa pamoja na kuwachukulia hatua watu wanaodaiwa kufanya hivyo,” alisema Sirro.

Aliongeza kuwa kwa sasa bado wanafanya upelelezi kuhusu tukio hilo na kwamba tayari watu watatu wanaodaiwa kuhusika wamekamatwa na kuendelea kuhojiwa.

Alisema kutokana na hali hiyo, watu waliobaki wataendelea kutafutwa ili wakamatwe na kufikishwa kwenye mikono ya sheria kwa hatua zaidi mara baada ya kukamilika kwa upelelezi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi upande wa CUF Maalim Seif, Julius Mtatiro, alisema tukio hilo ni la 12 tangu kuanza kwa matukio ya uvamizi kwa baadhi ya wanachama wanaomtii Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.

 “Tunajua kabisa Profesa Lipumba na genge lake wanalindwa na CCM, ndiyo maana polisi wanashindwa kuchukua hatua, kutokana na hali hiyo, tumewaambia itafika kipindi tutachoka, tutaanza kuruhusu walinzi wetu wajihami na matukio kama hayo,” alisema Mtatiro.

Alisema upande unaomtii Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif una jumla ya wabunge 40, huku upande wa Lipumba una wabunge 10, hivyo basi kama wakiamua kuendeleza ugomvi huo itakuwa hatari zaidi, kutokana na hali hiyo aliitaka polisi kulishughulikia suala hilo.

 

POLISI MAGOMENI

Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Kinondoni, Juma Nkumbi, jana alishikiliwa katika Kituo cha Polisi Magomeni.

Mwanasheria wa chama hicho, Hashim Mziray, aliliambia MTANZANIA kuwa walifika polisi kuitikia wito walioambiwa wanatakiwa kwenda kwa ajili ya kufungua kesi ya kuvamiwa.

Alisema baada ya kufika kituoni hapo, polisi walimwambia Nkumbi kuwa kunahitajika kufunguliwa majalada ya kesi mawili ambalo moja ni Nkumbi kushtakiwa na wale waliovamia mkutano na jingine ni yeye kushtaki waliovamia mkutano.

Hata hivyo, wakili huyo alisema ameshangaa kuona jalada moja limefunguliwa la Nkumbi kushtakiwa na waliovamia mkutano, huku yeye kushtaki waliovamiwa alielezwa kuwa bado wanaendelea na uchunguzi.

Hata hivyo, Mziray alisema Nkumbi aliachiwa kwa dhamana ya mdhamini mmoja na kiongozi mmoja wa Serikali ya mtaa anakoishi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles