28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Maalim Seif Rasmi ACT

*Ahitimisha miaka 26 ya uongozi CUF, asema alifanya mazungumzo na vyama 10 akachagua ACT

Na NORA DAMIAN

-DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amehitimisha miaka 26 ndani ya chama hicho baada ya kutangaza kujiunga na Chama cha ACT – Wazalendo.

Maalim alitangaza uamuzi huo jana saa chache baada ya Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam kutoa uamuzi wa kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa ni mwenyekiti halali wa CUF.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za za wabunge wa CUF Magomeni, alisema hana nia tena ya kuendeleza mabishano badala yake ataendeleza mapambano ya siasa.    

Katika mkutano huo, Maalim Seif aliongozana na Nassor Ahmed Mazrui ambaye awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF – Zanzibar na Joram Bashange (aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bara).

“Sasa imetosha mapambano ya siasa lazima yaendelee, tumetafakari kwa kina mwelekeo wetu na tumeona njia sahihi ni kutafuta jukwaa jingine ambalo ni ACT – Wazalendo.

“Wana – CUF waliokuwa wakituunga mkono nawaarifu kwamba mimi na wenzangu tumejiunga na ACT – Wazalendo na tunawaomba na wao wajiunge nasi  kuendeleza kazi tuliyokuwa tukiifanya CUF,” alisema Maalim Seif.

Alisema alitumia muda mrefu kuijenga CUF lakini anamshukuru Mungu kwa yote na anaendelea na safari.

“Nyumba ukiizoea kuhama kuna taabu, lakini kumbuka tunazaa watoto wetu tunawapenda, Mwenyezi Mungu anawachukua. Namshukuru Mwenyezi Mungu naendelea na safari.

“Ni kama tufe na mizigo yetu au mizigo tuitupe, hivyo tumeamua mizigo kuitupa…mizigo ya CUF tumeitupa,” alisema.

Aliwashukuru wananchi wote waliojitolea kwa kuwaazima nyumba zao kutumika kama ofisi za chama na kuwaomba waendelee kuwaunga mkono zitumike kwa jukwaa jipya la ACT – Wazalendo.

“Malumbano hatuna haja nayo, kama wamekwenda kuchukua ofisi wakachukue, lakini ofisi nyingine za CUF ni za watu binafsi, sasa mwenye jengo ana hiyari kama atabaki huko au atakuja kwetu,” alisema.

Alisema pia yuko tayari kushirikiana na vyama vyote makini hata kama ni Ukawa watashirikiana nao.

Maalim Seif alisema mapambano ya kujenga demokrasia na kusimamisha utawala wa haki unaoheshimu sheria si kazi ya lelemama na wataendelea kuikamilisha.

“Hatua tunayochukua leo (jana) ni kuandika historia mpya ya mabadiliko ya siasa Tanzania, kote Zanzibar na Bara. Umma haujawahi kushindwa popote duniani, hatuna wasiwasi kwamba umma wa Watanzania nao utashinda.

“Kwa wana – CUF wanaotuunga mkono wakati ni huu, wakati ni sasa. Shusha tanga, pandisha tanga, safari iendelee,” alisema Maalim Seif.

KWA NINI ACT?

Maalim Seif alisema awali  walitembelea baadhi ya vyama na kuwaeleza nia ya kutaka kuhama lakini walichambua na kuona masharti ya ACT – Wazalendo si magumu.

“Kabla ya kuchukua uamuzi huu, tulitembelea baadhi ya vyama   kuwaambia ikitokea tukahama kama watakuwa tayari kutukaribisha na kwa masharti gani.

“Vyama 10 tulivitembelea na kila mmoja alionyesha yuko tayari lakini kwenye masharti tukachambua tukaona ACT – Wazalendo, kwa kweli masharti yao si magumu.

“Tulisoma katiba yao na kuona inatufaa, hivyo tukaamua kwenda huko… Wanaosema nimekinunua ACT ni fikra za watu wajinga waliofilisika… mimi hata milioni moja sina,” alisema Maalim Seif.

Kuhusu nyadhifa katika chama hicho, alisema kama atapewa ataangalia akubali au laa lakini yuko tayari hata kuwa mwanachama wa kawaida.

“Sisi nyadhifa kwetu ‘it’s doesn’t matter’ tunakwenda hivi hivi, mahala ambako tuna hakika mapambano yetu yataendelea ni ACT – Wazalendo na niko tayari kuwa mwanachama wa kawaida,” alisema.

UAMUZI WA MAHAKAMA

Maalim Seif alisema uamuzi wa mahakama ni mwendelezo wa mpango aliodai umesukwa na dola kwa lengo la kuihujumu na kuidhoofisha CUF ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuhujumu demokrasia nchini.

“Dalili ya mwisho tulisema kwamba kuahirishwa kusomwa uamuzi wa kesi hii kutoka Februari 22 hadi leo (jana), kulikuwa na lengo la kutoa nafasi kwa upande unaobebwa kuandikisha tena bodi yao ya wadhamini na kufanya mkutano mkuu feki ili wakati uamuzi unatolewa iwe wametuingiza katika mgogoro mwingine.

“Labda lengo ni kutufanya tuendelee kupanda na kushuka mahakamani huku tukishindwa kufanya shughuli za siasa. Sasa imetosha, mapambano ya siasa lazima yaendelee,” alisema.

HATIMA WABUNGE 28

Kuhusu wabunge 28 waliokuwa wakimuunga mkono, Maalim alisema wamewaachia uhuru waamue wenyewe kama watahama sasa au baadaye.

“Wabunge ni wanachama wa CUF na wengi walituunga mkono lakini tumewaachia uhuru waamue kama watahama sasa au baadaye,” alisema.

Kati ya wabunge hao 28, 22 wanatoka Zanzibar na wanne Bara na mmoja wa Viti Maalumu ambao wamekuwa wakimuunga mkono Maalim Seif.

Hali ilivyo Zanzibar

Saa chache baada ya Mahakama kuridhia Profesa Lipumba kuwa ni mwenyekiti halali CUF, baadhi ya wanachama visiwani Zanzibar walianza kuhamisha vifaa katika Ofisi za Makao Makuu ya CUF Mtendeni mjini Unguja. Baadhi ya vitu hivyo ni samani za ofisi.

Pia kwenye baadhi ya maeneo, wafuasi wa Maalim walianza kushusha bendera za CUF na kupandisha za ACT huku zilizokuwa ofisi ndogo za chama hicho zikipakwa rangi za ACT.

Miongoni mwa matawi ambayo yameanza kubadilishwa rangi ni ofisi ya Jimbo la Chakechake na kuonekana kuwa na rangi zenye mfano wa Chama cha ACT- Wazalendo.

Maalum Seif ni nani

Maalim Seif alizaliwa katika Kijiji cha Nyali, kisiwani Pemba Oktoba 22, 1943.

Nyota ya siasa ya Maalim Seif inaonekana kuanza kung’ara   baada ya kumaliza shahada yake ya kwanza ya siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kurudi nyumbani.

Aliteuliwa kuwa msaidizi maalumu wa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe.

Muda mfupi baada ya uteuzi huo, Maalimu Seif aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu Zanzibar  baada ya Baraza la mawaziri kuvunjwa.

Baada ya hapo, Maalim aliweza kushika nyadhifa mbalimbali kwa nyakati tofauti, ikiwamo nafasi ya waziri kiongozi ambayo ni sawa na wadhifa wa waziri mkuu.

Mwaka 1977 – 1988 alikuwa Mjumbe wa Kamati kuu ya CCM lakini pia mwaka 1977 – 1987 alikuwa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM huku mwaka 1982 – 1987 aliteuliwa kuongoza Idara ya Uchumi na Mipango ya Chama cha Mapinduzi.

Maalim Seif ni miongoni mwa waanzilishi wa CUF iliyotokana na Kamati Huru ya Mageuzi (Kamahuru) baada ya yeye na wenzake kufukuzwa ndani ya CCM mwaka 1988.

Baadaye vuguvugu la Kamahuru lilianzisha Chama cha Zanzibar United Front (ZUF). Miongoni mwa waanzilishi mbali na Maalim Seif, walikuwa ni   Shaaban Mloo, Khamis Machano, Hamad Rashid na Juma Haji Duni.

Baada ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi, ZUF iliungana na Chama cha Civic Movement kilichoanzishwa na mwanasiasa mkongwe James Mapalala na kuunda Civic United Front (CUF) mwaka 1993.

Mapalala ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa kwanza wa CUF na Makamu wake akiwa Maalim Seif Sharif.

Hata hivyo, mwaka 1994 Mapalala aliondolewa kwenye nafasi ya uenyekiti, ambako mwenyewe anadai kuwa alifanyiwa mizengwe na kufukuzwa kwenye chama hicho huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni udini.

Baada ya kuondoka nafasi yake ilichukuliwa na Musobi Mageni na mwaka 1999 Profesa Ibrahim Lipumba alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa CUF nafasi anayoitumikia hadi leo – huku Maalim Seif akichaguliwa kuwa Katibu Mkuu

Mbio za urais

Maalim Seif  ameshiriki mbio za urais za Zanzibar mara tano bila mafanikio.

Uchaguzi Mkuu wa kwanza alioshiriki ni ule wa mwaka 1995 akigombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF  ambako alitangazwa kupata asilimia 49.76 ya kura zote dhidi ya Rais Salmin Amour “Komandoo” aliyekuwa na asilimia 50.24.

Katika uchaguzi wa mwaka 2000 Maalim Seif alitangazwa kupata asilimia 32.96 ya kura zote dhidi ya asilimia 67.04 za Amani Karume wa CCM.

Kwenye uchaguzi wa mwaka 2005, Maalim Seif aliangushwa kwa mara nyingine na Rais Amani Karume wa CCM.  Safari hiyo akitangaziwa kupata asilimia 46.07 dhidi ya 53.18 za Karume.

CUF ilikataa matokeo hayo na ikatangaza kutomtambua Karume kama Rais wa Zanzibar.

Maalim Seif alitupa karata ya nne ya kusaka urais wa Zanzibar mwaka 2010.

Alipambana na Dk. Ali Mohamed Shein ambako Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ilitangaza kuwa Dk Shein alimzidi Maalim Seif kwa kura 4471.

Maalim Seif alipata asilimia 49.1 dhidi ya asilimia 50.1 za Shein.

Hata hivyo, uchaguzi wa mwaka huo pia ulionekana kuwa na kasoro nyingi.

Mwaka 2015 Maalim Seif aligombea tena dhidi ya Dk. Shein na  kujitangaza kuwa alishinda uchaguzi huo kabla ya ZEC   kuufuta uchaguzi huo na kutangaza uchaguzi wa marudio   ambao CUF iliususa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,455FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles