27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MAALIM SEIF: NIPO TAYARI KWA MARIDHIANO

Na ASHA BANI


ALIYEKUWA mgombea urais Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema yupo tayari kufanya tena maridhiano endapo pande zote mbili zitakubali kwamba Zanzibar kuna matatizo.

Maalim Seif aliyasema hayo jana katika kipindi cha Funguka kinachorushwa na Televisheni ya AZAM na kuongozwa na mtangazaji nguli nchini, Tido Mhando.

Alisema maridhiano yaliyofanyika akiwa na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume,  yalikuwa na manufaa makubwa kwa kuwa Zanzibar ilikuwa na amani na utulivu.

Maalim Seif alisema CUF iliamua kukaa na Karume baada ya kuona uchaguzi ulikuwa unakaribia kufanyika hivyo ikaamua kufanya kikao cha muafaka wa maridhiano na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iliyozaa matunda.

Alisema baada ya kufanyika maridhiano na kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais alikuwa na nafasi kubwa ya kumshauri Rais mambo mbalimbali.

 “Hata kulipokuwa na SUK (Serikali ya Umoja wa Kitaifa),  mambo yalikuwa mazuri na maelewano na hata ilikuwa ikitokea mtu akifika ofisini anashindwa kufahamu CUF ni nani na CCM ni nani,’’ alisema Maalim Seif.

Alisema  hata sasa kama kuna nia njema ya kufanyika mazungumzo yafanyike kwa sababu  kwa sasa Zanzibar kuna matatizo na uhasama unazidi kupamba moto.

Maalim Seif pia alizungumzia suala la kufutwa  Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka 2015 na marudio yake Machi 20 mwaka jana.

Alisema yeye alishinda kwa kura nyingi na hivyo kama uchaguzi ungekuwa huru na haki yeye ndiyo alistahili kutangazwa kuwa Rais wa Zanzibar na si vinginevyo.

Alisistiza kwamba hatambui uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka jana  kwa kuwa hakushiriki na wala hakuwa na sababu ya kushiriki kwa kuwa mshindi alishapatikana Oktoba 25, mwaka juzi.

“Nisingeweza kukubali kurudia uchaguzi ule kwa kuwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC) alifuta matokeo yale ili CCM kwa njia zozote zile ishinde kwenye uchaguzi wa marudio.

“Hawakuweka mpira  uwanjani urudiwe eti kwa sababu washindwe  si kweli, hivyo wangetumia mbinu zozote ili washinde ,’’alisema Maalim Seif.

Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alisema ni kosa kukaa kimya wakati bado suala   la uchaguzi linafanyiwa kazi ili ufumbuzi upatikane.

Alisema  hilo  ni kama bomu ambalo likiripuka  hali itakuwa mbaya.

Mtangazaji alimuuliza MaalimSeif kama hakuona kuwa ni kosa kujitangazia   ushindi?

Alisema alifanya hivyo baada ya kuona kwamba ZEC ilikuwa anataka kumtangaza Dk. Shein (Ali Mohamed Rais wa Zanzibar) kuwa ni mshindi  huku hakushinda.

Hata hivyo alisema kama waliona amefanya makosa basi wangemkamata na kumpeleka mahakamani.

Alisema bado ana matarajio ya kuwa Rais wa Zanzibar katika   muda mfupi ujao.

Kuhusu uchaguzi wa 2020, alisema  ataangalia hali ya siasa ijayo.

 Mgogoro ndani ya CUF

Akizungumzia mgogoro ndani ya chama hicho, alisema  unachangiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.

Alisema Profesa Ibrahimu Lipumba aliamua kuondoka yeye mwenyewe.  “Lakini cha kushangaza baada ya miezi 10 akarudi sijui ni kwa misingi gani?” alihoji.

Alisema Katiba iko wazi kwa mtu anayejiuzuru, ni kwamba anaandika barua kwa Katibu Mkuu na Katibu anapeleka barua kwenye Mkutano Mkuu.

Alipoulizwa mbona alipokabdhiwa barua hakuitisha mkutano wa kumridhia Lipumba kujiuzulu, alisema hawakuweza kuitisha mkutano ghafla kwa kuwa chama hicho ni kidogo na hakikuwa na fedha.

‘’Lakini tuliitisha Mkutano Mkuu akajadiliwa, cha kushangaza yeye anang’ang’ania kuwa ni mwenyekiti, hii inashangaza haiwezekani katika hili!’’ alisema.

Alisema hata Msajili anafahamu kurudi kwa Lipumba ni lazima akubaliwe na Mkutano Mkuu.

Hata hivyo, alisema katiba ya chama haisemi mtu anayeondoka akae na baadaye aamue kurudi kwa sababu  hawafahamu kama ana nia njema na chama au la ikizingatiwa  pia alikiacha chama  katika kipindi kigumu cha uchaguzi mkuu.

Seif alisema kutokana na Msajili wa Vyama vya Siasa kuendelea kumtambua Profesa Lipumba licha ya kujiuzuru yeye mwenyewe, CUF kimeamua kwenda mahakamani  kuweza kupata tafsiri ya sheria.

“Mgogoro huu ulipandikizwa kwa wazi kabisa na Lipumba wakati anajiuzuru  tulimfuata na viongozi mbalimbali, wa dini wa chama wazee na vijana asitoke lakini alikataa kuendelea kubaki kwenye nafasi hiyo,’’ alisema.

Maalim Seif alisema kwa kufanya hivyo imeonekana kuwa Lipumba hakuwa na msimamo kwa kuwa yeye ndiye aliyewaletea aliyekuwa mgombea urais akiwakilisha Ukawa, Edward Lowassa, huku akisema kuwa kila alipokuwa akipita vijiweni, Lowassa alikuwa akitajwa tajwa sana na wananchi.

Alisema  yeye na wenyeviti wenzake wa   Ukawa walimtangaza Lowassa, hivyo Lipumba kubadili msimamo kulionyesha dhahiri kwamba tayari kulikuwa na nguvu nyuma yake iliyokuwa ikimshawishi  na hata baada ya kujiuzuru iliendelea kufanya hivyo.

Maalim  alisema baada ya Lipumba kukaa pembeni CUF kilipata mafanikio makubwa kwa vile kilipata viti vya ubunge 10 upande wa Bara na halmashauri nne ambazo ziliundwa na chama hicho  peke yake.

Alisema  hata katika uchaguzi mdogo wa marudio wa hivi karibuni, Lipumba alisimamisha wagombea katika kata 11 lakini hakuambulia kiti hata kimoja zaidi ya wagombea kupata kura 10 ,11,12.

Alipoulizwa hatima ya CUF kwa sasa,   alisema hiyo si mara ya kwanza kwa vile  kuna migogoro mikubwa ilipita huko awali ukiwamo wa Hamad Rashid Mohamed lakini ulikwisha.

Kuhusu kama ana mpango wa kuunda chama kingine, alisema ni hisia za watu tu na kwamba hana mpango huo.

Alisema  yeye ni mmoja wa waanzilishi wa CUF akiunda chama kingine ataonekana kuwa ni msaliti.

“Siwezi kuunda chama kingine nikaachana na CUF, mimi ni CUF kindakindaki na nitaendelea kuwa CUF kindakindaki  ndani ya chama ,’’alisema.

Alisema CUF kimeamua  kupeleka mahakamani  mgogoro huo na hata kama mahakama itampa Lipumba ushindi  watakata rufaa ingawa hawatarajii hilo.

Maalim Seif  alikiri kwamba bila vyama vya upinzani kuungana ni vigumu kukiondoa  CCM madarakani na ndiyo sababu ya kufanya hivyo.

Mgogoro wa ruzuku

Alimshangaa Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kutoa ruzuku kwa Profesa Lipumba   kupitia akaunti nyingine ambayo si ya chama makao makuu.

Alisema Msajili aliwaandikia barua kusema kuwa  ruzuku isingetolewa kutokana na chama hicho kuwa na mgogoro, lakini  baada ya muda wakashangaa imepitishiwa katika akaunti ya wilaya ya Temeke.

Kuhusu kushindwa uchaguzi wa marudio, Dimani alisema siyo kwamba wameshindwa bali   Dimani ni jimbo la CCM  na hata hivyo kama   demokrasi CCM ingetumika isingeshinda.

 

Maisha baada ya kustaafu

  Maalim Seif alisema licha ya kustaafu anapata haki zake zote kisheria siyo kuomba.

Haki hizo ni pamoja na gari, walinzi na posho kila mwezi ingawa alisema matibabu anajigharamia mwenyewe   kwa kuwa akiomba ananyanyaswa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles