26.1 C
Dar es Salaam
Friday, December 9, 2022

Contact us: [email protected]

Maalim Seif: Nikichaguliwa, wakulima wa karafuu, viungo watauza popote duniani

Mwandishi Wetu -Pemba

MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema endapo atapata ridhaa ya kuongoza, atahakikisha wakulima wa viungo na karafuu wanakuwa huru kuuza mazao yao sehemu yoyote wanayotaka duniani.

Maalim Seif aliyaeleza hayo katika Kijiji cha Konde, Wilaya ya Micheweni, ikiwa ni mwendelezo wa kampeni kupitia chama hicho katika Kisiwa cha Pemba.

Alisema kazi ya Serikali yake itakuwa ni kukusanya kodi ndogo ili kuwafanya wakulima wapate faida kubwa, waweze kuendeleza kazi yao hiyo kwa maendeleo ya nchi.

“Katika Serikali ya CCM imekuwa ikichukua faida kubwa kulikoni wakulima wenyewe, lakini Serikali ambayo nitaiongoza, nitahakikisha inachukua kodi ndogo na kuwafanyia mazingira ya kukuza kilimo chao,” alieleza  Maalim Seif.

Alisema kazi kubwa ya Serikali yake ni kuwapatia mbinu na mazinggira wakulima wa karafuu pamoja na bidhaa za viungo  ili iwe ni njia ya kukuza uchumi wa Wazanzibar.

“Tunataka kuwalea wakulima wetu wa bidhaa za viungo ili waweze kuitangaza Zanzibar katika masoko ya ulimwengu ili baadae wafanyabiashara za viungo waje Zanzibar kununua wenyewe,” alisema Maalim Seif.

Alisema katika Serikali ya CCM wakulima wa bidhaa za viungo wanaonekana kuchoka sana kutokana na kuandamwa na kodi kubwa za kila sehemu.

Maalim Seif alisema katika utawala wake atawashauri wakulima wa bidhaa za viungo kujikita zaidi kwenye bidhaa za viungo ambavyo vitaleta tija za haraka kwao na Serikali kwa ujumla.

Pia alisema kazi nyengine ya kufanya ni kuhakikisha Zanzibar inakuwa na mifugo bora na soko la uhakika.

Alisema atahakikisha huduma zote za mifugo zinapatikana ili kile kinachozalishwa kinakuwa bora katika masoko yote.

“Tutahakikisha viwanda vya madawa na vyakula vina vyakula vya mifugo yote vinapatikana hapahapa kwetu ili iwe rahisi wafugaji kuwahudumia mifugo yao,” alieleza Maalim Seif.

Alisema wafugaji wengi wa kuku Visiwani Zanzibar wameacha kufanya kazi hiyo kutokana na upatikanaji na  ughali wa madawa na vyakula.

Akizungumza mbele ya mgombea huyo, mfugaji wa kuku katika Kijiji cha Mtambile Mkoa wa Kusini, Pemba, Humud Muhammed Said, alisema kama ingalikuwa chakula cha kuku kinatengenezwa Zanzibar hata tija ingaliongezeka.

Alisema kwa mfano kwa siku yeye anahitaji matumizi ya gunia mbili na nusu ambayo moja ni Sh 55,000.

“Angalia kwa mwezi nitahitaji ngapi, kwa maana hiyo hatuwezi kupata faida nzuri kutokana na ughali wa vyakula… kama yangalikuwa yanazalishwa Zanzibar bei hiyo haiwezi kufikia,” alieleza Said.

Alisema ukiachana na vyakula, kuna madawa ambayo nayo wanaagizia nje ambayo mara nyingine yanachelewa sana.

Kufuatia malalamiko hayo, Maalim Seif alisema katika utawala wake atafanya mapinduzi katika sekta ya mifugo na kilimo cha viungo na karafuu kwa ujumla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,735FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles