Anna Potinus, Dar es Salaam
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, amesema hawakufanya uamuzi wa kuhamia Chama cha ACT Wazalendo kwa lengo la kukiteka chama hicho bali kukiongezea nguvu.
Maalim Seif amesema hayo leo Jumanne Machi 19, baada ya kukabidhiwa kadi ya chama cha ACT-Wazalendo iliyolipiwa ada ya miaka 10 katika Ofisi za Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es salaam ambapo amewataka wanachama wasifanye malumbano na wapinzani wao kwani kwa kufanya hivyo wanawapa nafasi.
“Mtachokozwa hasa katika mitandao ya kijamii lakini msikubali kujibizana nao kwani nguvu zao ni pale mnapojibizana nao tusiwape nafasi zao bali tutawale mitandao kwa fikra na mawazo ya jinsi tutakavyosonga mbele,” amesema.
“Sisi leo rasmi ni wanachama wa ACT-Wazalendo, tena mmenipa heshima kuniambia nichukue kadi namba moja ninawashukuru sana na tunaamini mmetupokea kwa moyo mmoja sasa tukafanye kazi ili tuwakomboe wananchi,” amesema.
Aidha amesema kuwa hakuna mahali popote duniani ambapo umma ukitaka jambo likashindikana na kazi yao kubwa ni kwa sasa ni kuwakusanya Watanzania na wakishakuwa na jeshi kubwa malengo yao yatatimia.