23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MAALIM SEIF: HAKUNA WA KUNITOA CUF

Na ASHA BANI – dar es salaam


KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema hakuna mtu yeyote wa kumwondoa katika nafasi yake aliyonayo ndani ya chama hicho.

Kauli hiyo ameitoa baada ya Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, kutangaza kumwondoa Maalim Seif katika nafasi yake ya ukatibu mkuu.

Profesa Lipumba alidai kuwa amefikia uamuzi huo kutokana na Maalim Seif  kukaidi wito wake na kutofika ofisini kwa miezi kadhaa.  

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Maalim Seif alisema ameshangazwa na kitendo cha Lipumba kutangaza kumng’oa katika nafasi hiyo ilhali yeye si mwenyekiti halali wa chama hicho.

“Sijashindwa kazi, mimi ni Katibu Mkuu hadi nisimamishwe na Baraza Kuu na yeye Lipumba kama ni mwenyekiti, alitakiwa lazima ahalalishwe na Baraza Kuu halali la chama.

“Tangu lini mwenyekiti akampangia kazi katibu mkuu, na hata angekuwa mwenyekiti halali, haruhusiwi kunipangia kazi mimi, yeye ni msemaji mkuu wa chama kwa mujibu wa katiba, hana mamlaka hayo,” alisema Maalim Seif.

Alisema mgogoro uliopo ndani ya chama hicho utamalizwa na mahakama ambayo ni chombo cha kutenda haki.

Maalim Seif alisema yuko tayari kwa jambo lolote na kuwa hatajali kufa akiwa katika mapambano ya kuikomboa CUF na Watanzania, kwani anaamini kuwa akifa atawaacha kina Maalim Seif wengine wenye misimamo kama yake.

“Binafsi nimetumia umri wangu wote kupigania demokrasia na haki za binadamu Zanzibar na Tanzania kwa ujumla na wananchi ni mashahidi wa hilo, nimepatishwa tabu na kupangiwa maovu mengi na walio nyuma ya mipango wakadhani wataweza kunitisha au kunikatisha tamaa, wameshindwa,” alisema Maalim Seif.

Alisema wengi waliomwingiza katika njama ovu wameondoka kwa vifo, hivyo hata waliokuwapo wataondoka na kumwacha na ushindi kwa nguvu za Mungu.

Maalim Seif alisema kwa hapa alipofikia sasa hakuna tena wa kumtisha wala kumkatisha tamaa, na kwamba ushindi wao uko karibu kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.

Kiongozi huyo alisema CUF inapita katika kipindi kigumu, akidai kuwa hali hiyo inasababishwa na hujuma zinazofanywa na dola kwa kumtumia Profesa Lipumba aliyemtaja kuwa kibaraka.

Alitaja hujuma hizo kuwa ni pamoja na kitendo cha dola kumtumia Lipumba kuendesha ‘genge la wahuni’ na kuvamia ofisi za CUF Buguruni.

Nyingine alisema ni kumzuia kushindwa kufanya shughuli zake kisiasa Tanzania Bara pamoja na kunyimwa ruzuku za chama Sh milioni 369 na kupewa Profesa Lipumba kinyume na utaratibu kwa mujibu wa katiba yao ya chama.

Maalim Seif alitaja njama nyingine ni kumtumia Mwenyekiti wa Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha katika kuufuta Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambao alidai kuwa alikuwa ameshinda.

“Njama nyingine ni Bunge kupokea wagombea ‘feki’ waliopitishwa na Baraza Kuu ‘feki’  kwa kumchagua Mohamed Habib Mnyaa kama mwakilishi wa CUF katika Bunge la Afrika Mashariki mtu ambaye hajapitishwa na chama, wala jina lake halijawakilishwa katika ofisi za katibu wa Bunge na katibu mkuu wa chama hicho,” alisema Malim Seif.

Aliongeza kudai kuwa hayo yote yanafanywa na dola kupitia mamlaka mbalimbali, ikiwa ni pamoja na msajili wa vyama vya siasa, polisi, hazina na kwa sasa Bunge kwa lengo la kuisambaratisha CUF.

“Siyo siri tena sasa kwamba kile kinachoitwa ‘mgogoro’ ndani ya CUF si chochote, bali ni hujuma zilizopangwa na zinazoendeshwa na dola kupitia njama ovu na mbinu chafu kwa lengo la kuua upinzani na mkakati wa kunyamazisha kila sauti inayowakosoa watawala.

“Watawala walioingia madarakani wameonekana kuwa na hofu ya kuendelea kubaki madarakani kutokana na mwamko ulioonyeshwa na Watanzania kuanzia Uchaguzi Mkuu wa 2015,’’ alisema Maalim Seif.

Alisema katika kuthibitisha hofu ya watawala, ni vyema kukumbuka matukio yaliyopata kutokea tangu washike madaraka.

Aliyataja baadhi ya matukio hayo kuwa ni pamoja na kupiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa nchi nzima.

Mengine alisema ni kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya mikutano ya Bunge kwa kuwaziba macho na masikio Watanzania wasisikie mijadala inayoendelea kutoka kwa wawakilishi wao.

Alisema pia kuminya bajeti za shughuli za Bunge, hasa kamati ili zisiweze kufuatilia ahadi mbalimbali walizozitoa kwenye kampeni kupitia mipango ya bajeti.

“Lakini pia kuwakamata na kuwabughudhi, kuwalaza na kuwafungulia mashtaka wabunge wa upinzani na wale wanaoonekana kuwa mwiba mkali kwa watawala, ili kuwatisha na kuwanyamazisha wale waliokuwa wakikosoa utawala.

“Mfano mwingine ni kuzipa mahakama maagizo hadharani ya jinsi ya kuamua kesi mbalimbali hata kufikia kusema hadharani kuwa Serikali itawapa fedha wanazozihitaji kwa ajili ya uendeshaji wa mahakama.

“Kuwakamata, kuwaweka ndani na kuwafungulia mashtaka watumiaji wa mitandano ya kijamii, wengi wao wakiwa vijana wanaotoa maoni yao kwa ajili ya kukosoa watawala.

“Kuwatisha waandishi wa habari na vyombo vyao hadharani, kuwatisha na kuwakamata wasanii wanaotumia vipaji vyao katika kuwakosoa watawala na kuwazindua Watanzania juu ya mwenendo wa Serikali,’’ alisema Maalim Seif.

Aliongeza kuwa matukio mengine ni pamoja na kutisha jumuiya za kiraia zinazojishughulisha na masuala ya haki za binadamu sheria na utawala bora kwa lengo la kuyanyamazisha ili zisitimize wajibu wao kwa jamii.

Pia, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuendelea kujipa mamlaka wasiyokuwa nayo kisheria ya kuita watu polisi kutoa amri wakamatwe na kuwekwa ndani.

 

HUJUMA ZA RITA

Akizungumzia kusajiliwa kwa wajumbe katika Bodi ya Wadhamini ya CUF, Maalim Seif aliitupia lawama dola kwa kutumia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), akidai kuwa kuna shinikizo kubwa la kumtaka Ofisa Mtendaji Mkuu kusajili wajumbe ‘feki’ wa bodi hiyo, kwa kutumia majina yaliyowasilishwa na Lipumba kwa kile alichoeleza lengo la kuhujumu majina halali waliyoyapeleka.

Alisema kuwa kimsingi bodi ya wadhamini ilikwishasajiliwa tokea mwaka 1993 kwa kufuata taratibu zote zilizoelekezwa na sheria ya wadhamini na hati ya usajili wanayo.

Maalim Seif alisema kilichokuwa kinafanyika kwa kipindi hiki ni kuweka sawa kumbukumbu za bodi hiyo kwa kuwalipia wadhamini na kuingiza kwenye kumbukumbu mabadiliko ya wajumbe kadiri yanavyofanyika kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

Alisema wanafahamu kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa amekuwa akiwasiliana na RITA ili kutia shinikizo wajumbe ‘feki’ waweze kusajiliwa jambo ambalo alisema hawatalivumilia.

MTANZANIA ilipomtafuta Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Emmy Hudson kuzungumzia madai hayo ya Maalim Seif, alisema hayana ukweli wowote kwa kuwa hata maombi yaliyowasilishwa bado hayajapitiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles