32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif: CCM wanatafuta kura Zanzibar kama ngedere

Seif_Sharif_HamadNa Jonas Mushi, Dar es Salaam

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharrif Hamad amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinasaka kura za kumpa ushindi mgombea wao wa urais Zanzibar mithili ya msako wa ngedere.

Akizungumza na MTANZANIA katika Hoteli ya Serena jana,  ambako  yupo kwa mapumziko ya matibabu, Maalim Seif alisema CCM inataka kushika madaraka kwa kutumia kila aina ya nguvu.

Alisema kinachofanyika Zanzibar  si uchaguzi bali ni kumtangaza Rais Dk. Mohamed Ali Shein kuwa rais wa Zanzibar baada ya kufuta matokeo halali ya uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana ambayo yalimpa ushindi.

Alisema ili kutimiza azma ya kumtangaza Dk. Shein, CCM wamelazimika kutafuta kura kwa kuwabana watumishi wote   nje ya Zanzibar kurudi visiwani humo kupiga kura na kwamba anayekaidi agizo atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe.

“Kinachofanyika si uchaguzi, bali ni kumtangaza Dk. Shein kuwa rais…CCM wanasaka kura utafikiri  wanasaka ngedere porini…watumishi wote waliopo nje ya Zanzibar wamelazimishwa kurudi  wapige kura.

“Sasa tunasubiri tu Rais atangazwe na kuapishwa.  Hata wakimtangaza Dk. Shein mshindi atakuwa ni Rais wa Jecha (Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salim Jecha) na CCM.

“Ukweli ni kwamba Wazanzibari wanajua rais wa mioyo yao, ni Maalim Seif na hawawezi kufuta hilo,”alisema.

Alisema anasikitika Zanzibar kurudi katika siasa za uhasama na chuki ambazo walizimaliza mwaka 2010 baada ya kuwa na maridhiano na kuunda serikali ya umoja wa  taifa.

“Mimi nasikitika CCM imeturudisha nyuma kwenye siasa za uhasama, chuki na uonevu. Mwaka 2010 tulifanya maridhiano mazuri tukamaliza haya mambo, sasa yamejirudia… hali ni mbaya wakuulizwa hatma ya Zanzibar ni CCM kwa sababu wao ndiyo wameamua tuwe hapa tulipo,” alisema.

Akizungumzia kutekwa kwa mwakilishi wa kituo cha redio cha Sauti ya Ujerumani (Deutsche Welle), Salma Said pamoja na matukio ya kukamatwa wafuasi wa chama hicho,Maalim Seif alisema pengine wangeshiriki uchaguzi hali ingekuwa mbaya zaidi tofauti na ilivyo sasa.

“Tulitazamia yatatokea haya na tukatangaza hatuingii kwenye uchaguzi huu kwa sababu si halali,wafuasi wetu wanakamatwa na wanateswa, sasa tungesema tuingie hali ingekuaje?” alihoji.

Alisema anashangazwa na hatua ya vyombo vya dola kumkamata Salma na kumpeleka kusikojulikana  kwa sababu  kufanya hivyo ni kuvunja misingi ya utawala bora.

Alipoulizwa kuhusu matumizi makubwa ya fedha akiwa hotelini hapo na kwamba alipewa nyumba na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) akaikataa, Maalim Seif alisema hajawahi kupewa nyumba  na yeye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar hivyo ana stahiki zake.

“Sijawahi kupewa nyumba nikaikataa. Kama kuna mtu ana ushahidi athibitishe nilipewa nyumba wapi na lini ajitokeze… kama Makamu wa Kwanza wa Rais nina stahiki zangu, sasa kwa nini ninapopewa inakuwa ‘issue’ na si wengine.

“Najua kuna ajenda ya kumchafua Maalim Seif inafanywa na baadhi ya waandishi wa habari wakishirikiana na CCM, niko safi na wananchi wananijua,” alisema.

Akizungumzia afya yake alisema: “Afya yangu ni nzuri, nipo hapa (hotelini) kwa sababu madaktari wamesema nipumzike, nashangaa vyombo vya habari vimeona Maalim Seif tu ndiye anayeumwa na si viongozi wengine.”

Alisema anasubiri ruhusa ya madaktari na kwamba siku yoyote atakayoruhusiwa atarudi Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles