MAALIM SEIF AUNGWA MKONO, PROF. LIPUMBA AGOMEWA

0
630

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM


BAADHI ya wenyeviti wa Serikali za mitaa wa Chama cha Wananchi (CUF), Mkoa wa Dar es Salaam, wamemuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad  huku wakigomea uamuzi wa kuitwa kuhojiwa na Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Profesa Ibrahim Lipumba.

Kutokana na hali hiyo wamesema kuwa kiongozi huyo hana sifa ya kufanyakazi wala kuwahoji kwani alishapoteza sifa ya kukiongoza chama hicho kwa mujibu wa katiba ya CUF.

Licha ya hali hiyo viongozi hao pia wameunga mkono tamko la Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Pwani, Saed Kubenea la kushirikiana katika operesheni yao inayojulikana kwa jina la ‘Ondoa Msaliti Buguruni’(OMB) iliyotangazwa kuanza hivi karibuni.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kwa niaba ya wenyeviti hao, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mtambani Manispaa ya Kinondoni,  Bakari Kasubi alisema Profesa Lipumba hana sifa ya kuwaita kwani alishafukuzwa uanachama ndani ya chama hicho.

“Tunasikia eti wanaojiita viongozi wa chama walipora mamlaka isiyo yao wanaandaa utaratibu wa kuwaita baadhi ya wawakilishi wa chama, madiwani, wabunge na viongozi wa serikali za mitaa kwa kile kinachoitwa kwenda kuhojiwa na kamati ‘feki’ ya maadili ya chama, hatuwezi kuhojiwa na watu hao,’’ alisema Kasubi.

Alisema wao wenyeviti wanaunga mkono juhudi na mwelekeo uliochukuliwa na chama chao kutokana na maamuzi ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa  na msimamo wa chama uliotolewa na Katibu Mkuu wao Maalim Seif Sharif Hamad.

Alisema wenyeviti wanaungana kupinga maamuzi ya RITA mbele ya Mahakama Kuu kwa kufungua kesi ambayo kwa mujibu wa kifungu cha 26 kwa kukiuka taratibu za sheria ya wadhamini na kesi nyingine zinazohusiana na hujuma ambazo walitaja kuwa ni fedha za ruzuku.

“Tunapingana kwa nguvu zote njama na mipango ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi kwa kushindwa kuheshimu hadhi na nafasi yake mbele ya jamii na kujiingiza katika vitendo vya hovyo  vyenye muelekeo wa kutaka kuiharibia mustakabali wa CUF  na kuwaathiri wadau mbalimbali walioshiriki katika kuasisi na kuijenga kwa takribani miongo miwili na nusu sasa,’’alisema Kasubi.

Alisema wanampinga Profesa Lipumba kwa kukubali kutumiwa na CCM kwa masilahi yao binafsi na kushindwa kuthamini mchango wa CUF katika kujenga demokrasia nchini.

“Lipumba leo amekuwa mtu wa kuweweseka ameshindwa kutumia taaluma yake kwa masilahi ya taifa, kila kukicha anatafuta msaada kwa vyombo vya dola ili kufanikisha dhamira yake, ameshindwa kukemea vitendo viovu  vinavyoendelea kufanywa na wafuasi wake wanapohudhuria mahakamani, kushambulia waandishi wa habari kauli za kashfa na kejeli dhidi ya viongozi ,’’alisema .

Aliongeza kuwa wito wao kwa wanachama na viongozi wa CUF kujiandaa vyema kukabiliana na mfumo kandamizi wa demokrasia nchini na kuwashughulikia wale waliowaita vibaraka wanaotumika katika kuharibu demokarsia na kukivuruga chama hicho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here