
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
UJUMBE wa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ukiongozwa na maofisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Vyama vya Kiliberali Duniani (Liberal International (LI)) ulianza ziara ya Ulaya kwa kutembelea makao makuu ya LI mjini London, Uingereza juzi.
Ujumbe wa CUF ulieleza wasiwasi wake kuhusu ongezeko la vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu visiwani Zanzibar tangu kufanyika uchaguzi wa marudio ambao CUF waliususa, Machi 2016.
Vitendo hivyo ni pamoja na kamata kamata bila kufungua kesi na kuminywa uhuru wa kutoa maoni.
Akiwaeleza wawakilishi wa LI namna CUF wanavyoendesha harakati za upinzani kwa njia ya demokrasia na amani ingawa waliporwa ushindi na serikali ya Tanzania Oktoba 2015, Seif Sharif Hamad alisema:
“Kinachotokea leo (juzi) hii ni ukandamizaji; serikali inahakikisha CUF hawafanyi kazi”.
Katibu Mkuu wa CUF alitoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa kutambua na kuzuia uwezekano wa kutokea machafuko kutokana na kuminywa demokrasia katika eneo hilo ambalo tayari hali ni tete.
Katibu Mkuu wa LI, Emil Kirjas alieleza kuwaunga mkono wenzao wa Tanzania akisema kwamba, “hamko pekee yenu katika harakati hizi.”
Aliongeza: “Sote katika jumuiya ya vyama vya kiliberali duniani tutafanya kila linalowezekana na kwa kadiri ya uwezo wetu kuhakikisha maisha yenu yanalindwa na matakwa ya walio wengi visiwani Zanzibar mwishowe yanaheshimiwa na Chama cha Wananchi, chini ya Maalim Seif, kinaunda serikali ya maendeleo na ustawi wa Zanzibar.”
CUF ni mwanachama wa LI tangu mwaka 1994, umoja ulionzishwa mwaka 1947 ukiundwa na vyama zaidi ya 100 vya kiliberali duniani. Umoja huo pia unajumuisha marais na mawaziri wakuu wanane (8) wa nchi mbalimbali.