22.5 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Maalim Seif atua Mahakama ya ICC

maalim seif

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

ALIYEKUWA mgombea urais visiwani Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, leo amewasili Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuwashtaki viongozi anaodai wanaminya demokrasia visiwani humo.

Taarifa za Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa chama hicho kuwasili katika mahakama hiyo mjini The Hegue, zilibainishwa mjini Dar es Salaam jana na Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Mazrui    alipozungumza na waandishi wa habari.

“Maalim Seif alipeleka maombi Mahakama ya ICC, kajibiwa ndiyo  maana  kesho (leo) anafika mahakamani kuelezea jinsi demokrasia inavyominywa Zanzibar.

“Amepeleka vielelezo vingi, vikiwamo vya uvunjaji  wa haki za binadamu, baada ya maelezo mawakili wataendelea na utaratibu wa kimahakama,”alisema Mazrui.

Katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu, baada ya ule wa mwaka jana kufutwa, Maalim Seif hakushiriki kwa madai kuwa haukuwa halali.

Alisema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana uliofutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha, kwa madai kulikuwa na kasoro nyingi, licha ya waangalizi wa kimataifa kusema ulikuwa huru na haki.

Katika uchaguzi wa marudio, mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohamed Shein aliibuka mshindi kwa kupata kura  299,982 ambazo ni  sawa na asilimia 91.4, akifuatiwa na na mgombea wa Chama cha ADC, Hamad Rashid Mohamed aliyepata kura 9,734 ambazo ni  sawa na asiilimia 3.

IGP

Kuhusu kauli ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu kuwa  jeshi hilo litamkamata na kumfikisha mahakamani Maalim Seif, Mazrui alisema ni jambo ambalo haliwezekani.

Alisema hofu ya IGP Mangu, inatokana na kuona kuna kila dalili za viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na yeye mwenyewe kufikishwa mahakamani.

“Tunasema azma ya kuwafikisha mahakamani vinara wote wa uminyaji wa demokrasia na uvunjaji wa haki za binadamu iko pale pale.

“Ameamua kutumia mkakati wa kutaka kumkamata kiongozi kama njia ya kujipapatua ili kuhakikisha lengo la CUF halifanikiwi,”alisema.

Alisema hakuna asiyejua Maalim Seif ni kipenzi cha Wazanzibari na ndiye anayeshinda uchaguzi mkuu wote Zanzibar.

Alisema  jaribio lolote  la kumkamata na kumdhalilisha kwa kumweka ndani ni kulazimisha au kutaka kuitumbukiza Zanzibar na Tanzania katika machafuko ambayo kiongozi huyo hapendi kuona yanatokea.

“CUF inamtaka IGP Mangu kufahamu, Maalim Seif na viongozi wote hawatatishwa wala kurudishwa nyuma au kunyamazishwa kwa aina yoyote ya vitisho katika kudai haki ya ushindi Zanzibar kutokana na uamuzi uliofanywa Oktoba 25, mwaka jana,”alisema.

Alisema mpango wa kuishawishi dunia kuwachukulia hatua wahusika wote wa ukiukwaji wa haki za binadamu na uminywaji wa demokrasia uko pale pale hautasitishwa kwa vitisho.

“Kama vitisho vikiendelea, CUF tutakwenda kumtembelea IGP Mangu ofisini kwake,”alisema.

Alisema wanashangazwa kuona mpaka sasa IGP Mangu,ameshindwa kumchukulia hatua za kumwajibisha Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai (DDCI), Salum Msangi dhidi ya kauli za vitisho na kibabe alizotoa kuhusiana na mawakili wanaofika vituo vya  polisi kuwawakilisha na kuwatetea wananchi waliokamatwa kwa tuhuma mbalimbali.

Mwishoni mwa Juni, mwaka huu wabunge wa Ukawa walimtaka Rais Dk. John Magufuli kutoa tamko juu ya uvunjifu wa haki za binadamu Zanzibar na kwamba wana mpango wa kumpeleka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), wakidai yanayotokea visiwani humo yana baraka zake.
Wabunge hao walimtaka pia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba kwenda Zanzibar kujionea hali halisi badala ya kupata taarifa kutoka kwa wasaidizi wake.

Mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia alisema hali ya kiusalama inazidi kuwa mbaya Pemba na Unguja kutokana na baadhi ya wananchi kupigwa na vikosi alivyodai ni vya usalama.

MNYIKA

Wakati huo huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC), Dk. Liberat Mfumukeko,wamefunguliwa kesi ya kikatiba katika Mahakama ya Afrika Mashariki .

Kesi hiyo, imefunguliwa jana ambapo mlalamikaji wa kwanza, ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe,Mbunge wa Kibamba, John Mnyika  na mlalamikaji wa tatu akiwa ni Chama cha  Chadema.

Akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kufungua kesi hiyo,Wakili wa Chadema, John Mallya alisema  kesi hiyo ya kikatiba ni ya kupinga uvunjifu wa vifungu vya mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo.

Alisema mkataba huo, unataka nchi ambazo ni wajumbe wa jumuiya hiyo kuheshimu masuala ya kidemokrasia,vyama vingi na uhuru wa watu kukusanyika.

“Nimeagizwa na wateja wangu  Mbowe, Mnyika na Chadema,kuwafungulia kesi na nimeshaiwasilisha mahakamani na tuna imani itapangiwa majaji na hivi karibuni itaanza kusikilizwa”alisema na kuongeza

“Sababu za msingi za kufungua kesi hii, ni zuio ambalo  polisi wameliweka na Rais Magufuli amekuwa akilirudia mara kwa mara kwamba vyama vya siasa havipaswi kufanya shughuli za siasa wakati huu hasa mikutano ya hadhara hadi mwaka 2020,” alisema.

Kwa upande wake, Mnyika ambaye ni mlalamikaji wa pili katika kesi hiyo, alisema Katiba ya Tanzania na Sheria zingekuwa zinaruhusu Rais aliyeko madarakani kushitakiwa, kesi hiyo wangemshtaki Rais Magufuli moja kwa moja.

“Sheri zetu zingekuwa zinaruhusu kumshitaki Rais,leo tungemburuza

Magufuli moja kwa moja, tutasimamia hoja mahakamani na tumeleta vielelezo  mbalimbali, ikiwemo barua ya zuio la Polisi,mikutano ambayo imezuiwa ikiwamo wa Kahama…tunaamini vitakuwa ushahidi wa namna ambavyo Serikali ya Tanzania kupitia Polisi kukiuka mkataba wa Jumuiya

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles