25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 29, 2021

Maalim Seif ataka mashirika ya kimataifa kusitisha riba za mikopo

Na NORA DAMIAN

-DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, ameyaomba mashirika na taasisi za fedha duniani kusaidia nchi zinazoendelea kwakusimamisha kwa mwaka mmoja malipo ya madeni ili fedha zinazookolewa zitumike kukabili virusi vya corona.

Pia ameshauri watu wote ndani walio katika hatari ya ugonjwa wa corona, wapimwe kuzuia kusambaa kwa maambukizi. 

Akizungumza jana, alisema iwapo mashirika ya kimataifa yatakubali, fedha zitakazookolewa zitasaidia kujenga mfumo wa afya utakaosaidia watu masikini na kurejesha hali ya uchumi katika hali ya kawaida. 

“Mataifa mengi hasa ya Afrika yanatumia fedha nyingi kuhudumia madeni yao hasa ya nje. Iwapo taasisi kama Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF)na nchi zilizoendelea zitasimamisha kutaka kulipwa riba ya madeni haya, nchi zetu zinazoendelea zitapata nafuu na kupata fedha za kusaidia kukabiliana na virusi vya corona,” alisema Maalim Seif.

Maalim Seif pia alishauri Serikali zote kuchukua hatua za dharura za kupunguza makali ya kiuchumi kwa wananchi. 

“Kila mmoja wetu anayejiita kiongozi ana wajibu wa kumlinda mwananchi maskini anayeteseka na kadhia hii.

“Ipo haja kubwa ya kujipanga, kwamba iwapo tutafikia kipindi cha kuwataka watu wabaki majumbani je, tutawasaidia vipi kujikimu kwa angalau mahitaji yao ya msingi hasa chakula?” alihoji.

Kwa mujibu wa Maalim Seif, kwa Zanzibar theluthi moja ya pato la taifa inategemea utalii na asilimia 80 ya mapato ya fedha za kigeni yanatoka kwenye sekta hiyo ambayo sasa imeathiriwa na corona.

Alisema watu wengi hasa vijana waliokuwa wanategemea kuongoza watalii ili kupata vipato vyao kwa sasa hawana shughuli ya kufanya. 

“Wafanyakazi wa hoteli na migahawa wapo nyumbani hawana kazi, wasafirishaji kuanzia madereva wa taxi,  daladala na hata marubani wa ndege za watalii sasa wapo nyumbani kwa sababu shughuli zimesimama,” alisema.

Alisema licha ya kuwapo mipango ya kupunguza msongamano wa wafanyakazi katika ofisi za Serikali, alihoji iwapo kuna sera ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) ya kuwashawisha watu kubaki majumbani na kuepuka misongamano au mikusanyiko isiyo na ulazima.

“Nchi kubwa duniani zinapoteza maelfu ya raia wao kutokana na kuzidiwa uwezo kwa mifumo yao ya afya na hospitali, ikiwa hali ni hivyo kwa nchi hizo tajiri zenye fedha itakuwaje ugonjwa huu ukifikia katika nchi kama yetu?” alihoji. 

UPIMAJI KWA JAMII

Maalim Seif alisema kufunga mipaka ya bandari na uwanja wa ndege ni hatua moja lakini kuna haja ya kuanza kufanya upimaji kwa jamii.   

“Kwa wenzetu mashirika yote ya kimataifa ya afya watusaidie Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika kuanzisha mifumo bora na ya haraka ya kuwapima wale walio katika hatari ya ugonjwa wa corona. 

“Mifano ya nchi za wenzetu waliofanikiwa kwa kiasi kikubwa hadi sasa kukabiliana na corona imeonyesha upimaji katika jamii ni msingi mkubwa wa kupambana na adui huyu corona,” alisema Maalim Seif.

Pia aliwaasa wananchi kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu kwa kuepuka mikusanyiko na kupunguza watu wanaokutana nao.

“Nawaomba sana msipuuze ushauri wa watalaamu wa kukaa umbali wa angalau mita mbili kutoka mtu na mtu. 

“Hata kama corona haitokuathiri wewe, ukishindwa kufuata ushauri wa wataalamu utakuwa ndani ya hatari ya kuwadhuru wenzako, marafiki, ndugu, jamaa, wazee, watoto, mke, au mume.

“Jiulize, utakwenda kusema nini mbele ya muumba wako pale itakapodhihirika kuwa wewe ndiye uliyekuwa chanzo cha madhila na misiba ya wenzako? Tuchukue tahadhari na tufuate tunayoelekezwa,” alisema.

Aliwasihi wananchi kufuata maelekezo ya wataalamu ili kuzuia nchi kupata maambukizo makubwa kwani uwezo wa kuyakabili ni mdogo, hivyo ufumbuzi ni kujikinga. 

“Kama kila Mzanzibari na kila Mtanzania atafuata maelekezo ya wataalamu wa afya kwa usahihi tutapunguza maambukizo kwa kiasi kikubwa na kuushinda ugonjwa huu. 

“Tukifanya uzembe hospitali zetu ambazo hali yake tunaijua wenyewe hazitakuwa na uwezo wa kukabiliana na wingi wa wagonjwa na hivyo, watu wetu wengi watapoteza maisha yao,” alisema. 

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,301FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles