31.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Maalim Seif amtafakari Lipumba kwa saa 10 kikaoni

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ameitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji ya Taifa ili kutafakari kusudio la Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini na kudai amevunja amri ya Mahakama Kuu kwa kuitisha Mkutano Mkuu wa Uchaguzi.

Maalim Seif ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya Taifa kwa mujibu wa Katiba ya chama chao, imeelezwa aliitisha kikao hicho kwa dharura na kujadili hatua hiyo ya Lipumba kwa muda wa saa 10.

Taarifa iliyotolewa jana na Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma upande wa Maalim Seif,  Mbarala Maharagande, ilieleza kwamba kikao hicho kilifanyika Ofisi ya CUF Vuga mjini Unguja visiwani Zanzibar, kuanzia saa tisa alasiri na kumalizika saa 7 usiku.

Alisema lengo la kikao hicho ni kujadili kile kilichoelezwa na upande wa Profesa Lipumba, kuvunja amri ya mahakama iliyotoa zuio la kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Taifa uliopangwa kufanyika Machi 14 na 15.

Kikao hicho cha Maalim Seif kilitanguliwa na tamko lililotolewa juzi na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, upande wa Maalim Seif, Joran Bashange, kuhusu kusikitishwa na taarifa walizozipata za kuandaliwa kwa mkutano huo huku kukiwa tayari na zuio la mahakama.

Katika tamko lake, Bashange alidai kwamba sasa wanawaachia wanachama na wafuasi wao ili waweze kukihami chama na hujuma za aina yoyote zinazotaka kufanywa ikiwamo kutaka kumng’oa Maalim Seif katika nafasi yake ya Katibu Mkuu.

Hata hivyo kauli hiyo ya Bashange ilionekana kupuuzwa na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma wa upande wa Lipumba, Abdul Kambaya, ambaye alisema mkutano huo uko palepale na maandalizi yanaendelea na hakuna wa kupingana na zuio la mahakama lililowataka wasifanye.

TAARIFA YA MAHARAGANDE

Katika taarifa yake Maharagande alieleza kuwa mahakama ilitoa zuio siku ya Februari 28, mwaka huu mbele ya Jaji Stephen Magoiga ya kuzuia kuandaa na kusitisha Mkutano Mkuu wa CUF Taifa.

“Amri ya zuio inasomeka ifuatavyo kwa tafsiri kwamba wamezuiwa wamekatazwa washtakiwa au wajibu maombi ambao iliwataja ni pamoja na Profesa Ibrahim Lipumba, Mashaka Ngole, Magdalena Sakaya, Abdul Kambaya, Jafari Mneke na Thomas Malima.

“Wengine ni Salma Masoud, Haroub Masoud, Haroub  Shamis, Khalifa Suleiman Khalifa, Mohamed Habib Mnyaa, Nassor Seif Amour, Thiney Juma Mohamed, Rukia Kassim Ahmed, Kapasha Kapasha na Maftaha Nachuma,’’ ilieleza sehemu ya taarifa ya Maharagande.

Alisema kuwa hukumu imefafanua na kuweka bayana kuwa mawakala wao na mtu yeyote anayefanya kazi kwa niaba yao wamezuiwa kuitisha Mkutano Mkuu ‘feki’ kwa jina la CUF -Chama cha Wananchi.

Maharagande alisema katika kutafakari suala hilo Kamati ya Utendaji imezingatia taarifa ya Naibu Katibu wa Mkuu Tanzania Bara, Bashange kupitia mkutano wa waandishi wa habari kwamba taarifa zote na nakala ya hukumu zimepelekwa kwa Jeshi la Polisi na kukabidhiwa IGP Sirro, Kituo Kikuu cha Polisi, RPC Ilala, OCD Buguruni na mamlaka nyingine za Serikali.

Pia alieleza kuwa kamati tendaji imetoa wito kwa wanachama wa CUF, viongozi na wapenda demokrasia, amani na ustawi mwema wa taifa kushiriki na kuhakikisha  amri ya katazo la Mahakama Kuu linatekelezwa na mkutano upande wa Profesa Lipumba haufanyiki.

“CUF ni taasisi imara na yenye viongozi makini, tumetafakari vyema na tumejipanga vyema kwa hali zote,’’ alisema Maharagande katika taarifa hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,625FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles