29.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 30, 2024

Contact us: [email protected]

MAALIM SEIF AMKINGIA KIFUA JPM

*UVCCM  yasema hajakosea uteuzi wa Mghwira

*Zitto atuliza wanachama ACT Wazalendo


Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amemkingia kifua Rais Dk. John Magufuli kwa uamuzi wake wa kumteua Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Maalim Seif alisema Rais Magufuli hajakosea kwa uteuzi huo kwa kuwa hapangiwi nani amweke wapi na nani asimweke.

“Uteuzi ni haki yake, wala hatuingilii maamuzi yake kwa sababu kuteua au kutoteua ni yeye na kuteua ACT na kuacha vyama vingine huenda yeye mwenyewe ana yake moyoni na kwamba hajaamua kufanya hivyo.

“Mimi sikuingia katika moyo wake na kwa kufanya hivyo si jambo geni kwa kuwa wapo waliopita waliwapa wapinzani ubunge, lakini pia ni Rais wa kwanza kuingiza mtu wa chama kingine kwenye serikali katika utendaji…si jambo baya kwa maana linaweza jenga upya Serikali,’’ alisema.

Alisema Rais Magufuli ametumia mfumo ambao pia hutumiwa na nchi za Bara la Ulaya na Marekani, ambapo Rais Mstaafu wa Marekani, Barack Obama naye aliutumia.

“Siwezi kushangaa kwani inaweza ikatokea siku akamteua Naibu Katibu Mkuu wangu, Joran Bashange kuwa Waziri wa Nishati na Madini,” alisema Maalim Seif huku waandishi na maofisa wa chama hicho wakiangua kicheko.

Katika hatua nyinginje Katibu Mkuu huyo wa CUF, alizindua ofisi mpya ya chama hicho iliyopo Magomeni Mapipa Mtaa wa Idrisa Kata ya Mzimuni, jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo ya Maalim Seif kuzindua ofisi hiyo ya wabunge wa chama hicho ambayo pia naye ataitumia kwa majukumu yake, jambo lililotafsiriwa ni kama kuepusha shari kwa kutokwenda katika ofisi za CUF Buguruni ambazo kwa sasa zinatumiwa na Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.

Tangu kuanza kwa mgogoro ndani ya CUF, Maalim Seif na wabunge wanaomuunga mkono hawajawahi kukanyaga katika ofisi hizo licha ya kila mara kutoa tishio la kwenda kufanya usafi na kujikuta wakikwama kutokana na amri ya Jeshi la Polisi.

“Wamenikaribisha kuja kupokea jengo kwa niaba ya chama tumelibariki lakini niwapongeze kwa moyo wao wa kujitolea  hasa wabunge wa CUF kwa kipindi hiki kwani wamekuwa wanachama wazalendo, kutokana na michango mbalimbali ambayo huwa wanachangishana.

 “Nyie wote mnafahamu Msajili wa Vyama vya Siasa  kazuia ruzuku kwa muda mrefu lakini chama kinakwenda bila ruzuku, kinaendelea kuendesha shughuli zake pamoja na  michango ya wanachama  lakini wabunge wamekuwa wakijitolea kiasi cha kwamba nawaonea huruma wakati mwingine,’’ alisema Maalim Seif.

Mtoto wa Karume atua CUF

Jana Katibu Mkuu huyo wa CUF, alimkabidhi kadi ya chama hicho, mtoto wa kwanza wa Rais wa Sita wa Zanzibar, Ahsa Amani Karume.

UVCCM

Nao Umoja wa  Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM),  umesema hatua ya Rais Dk. Magufuli kumteua Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ni kitendo cha kijasiri na cha kizalendo kwa sababu  hakuna alipokosea.

Pamoja na hali hiyo, umoja huo umesema uteuzi wa nafasi ya RC Mghwira, ni wazi ataisimamia na kuongoza kwa hekima, busara na uzalendo kwa masilahi ya Taifa.

Kauli hiyo, imetolewa  Dar es Salaam jana na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka.

Alisema uteuzi huo, usiibue nongwa na kuonekana kuna jambo limekosewa.

Pamoja na hali hiyo Shaka, alisema Katiba ya nchi hairuhusu mgombea binafsi na kwamba kila mgombea urais, udiwani au ubunge hutokana na chama cha siasa ila anaposhinda urais huwa na mamlaka ya kuteua mtu yeyote ili mradi awe Mtanzania bila ubia.

Alisema Rais Dk. Magufuli, ana haki na wajibu wa kumteua mtu yeyote atakayeona anafaa kushika nafasi atakayomteua ilimradi aliyeteuliwa awe ana hisia za uchapakazi, mpenda umoja na mzalendo.

Shaka alisema katiba ya CCM imetamka ikiwa kutakuwa na mkuu wa mkoa anayetokana na CCM atashiriki vikao vya Kamati ya Siasa ya Mkoa wakati wa vikao lakini kwa suala la Mghwira lipo tofauti kwani anatokana na chama kingine na ikiwa ataona kuna haja ya kujiunga na CCM basi naye atapata fursa ya kushiriki vikao hivyo.

“Ila kwa sasa hasa baada ya kuripoti katika eneo lake la kazi hatoweza kuhudhuria vikao vya Kamati ya Siasa ya Mkoa kwa kuwa si mwana CCM ila kama ataona kuna haja ya kujiunga na CCM hazuiwi na atakuwa na haki ya kuhudhuria vikao vyote.

“Kwa hili Rais Dk. Magufuli anabaki kuwa nembo ya demokrasia ya kweli nchini kwetu kwa kushirikisha wapinzani kwenye nafasi nyeti za utendaji.

“Viongozi wa Serikali wakiteuliwa hula viapo vya utii ambavyo vimeandikwa kisheria katika medani za uendeshaji Serikali, mteule wa Rais hali kiapo cha kisiasa bali huapa kiapo cha kutumikia nchi na watu wake kwa mujibu wa sheria za nchi na Katiba,” alisema Shaka.

Zitto

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ametoa tamko kuhusu uteuzi wa mwenyekiti wao huku akiwataka wanachama wake kuwa watulivu.

“Nimekuwa naulizwa Sana kuhusu uteuzi wa Mwenyekiti wa Chama chetu kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro. Nimekuwa kimya Kwa sababu tumepokea taarifa za uteuzi kutoka katika vyombo vya Habari Mwenyekiti yuko nje ya nchi na kutokana na tofauti za masaa bado hatujawasiliana nae. Tutatoa tamko kamili atakapokuwa amerejea nchini,” alisema Zitto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles