23.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif alazwa Dar

MAALIM+SEIF+PHOTONa Sarah Mosi, Zanzibar

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amelazwa katika Hospitali ya Hindu Mandal, Dar es Salaam akisumbuliwa na kile kilichoelezwa kuwa ni uchovu wa safari.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassoro Mazrui, aliliambia MTANZANIA jana kuwa kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani Zanzibar, anaendelea na matibabu ya uchovu baada ya safari ndefu alipokuwa nchini India kwa matibabu ya upasuaji wa mgogo siku chache zilizopita.

Alisema Maalim Seif amelazwa jana asubuhi na hali yake inaendelea vyema, huku akisisitiza kuwa si mgonjwa wa kukatisha tamaa.

“Anakula na kufanya kila kitu mwenyewe na hata jioni hii nimeongea naye, anakula kila kitu, hivyo Watanzania wasiwe na wasiwasi juu ya afya ya Maalim.

“Hakuna taarifa za kidaktari zilizothibitisha kwamba Maalim  ana tatizo la moyo kama ambavyo habari zinavyosambaa mitandaoni. Anasumbuliwa zaidi na uchovu,” alisema Mazrui.

Kwa zaidi ya wiki tatu kiongozi huyo wa chama kinachounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alikuwa nchini India alikokuwa anapatiwa matibabu na baadaye alirudi nchini na kukutana na baadhi ya wanachama wa CUF nyumbani kwake Mbweni mjini Unguja, Zanzibar.

Katika mkutano huo, Maalim Seif alisisitiza msimamo wa chama chake kutoshiriki uchaguzi wa marudio Zanzibar unaotarajiwa kufanyika Machi 20.

Aidha alisema kuanzia sasa wanachama na viongozi wa CUF hawatokubali tena kudhalilishwa na vyombo vya ulinzi na usalama na ikitokea wakipigwa shavu la kulia hawatogeuza la kushoto.

Maalim Seif alisema hatua ya hivi karibuni ya viongozi wa Jeshi la Polisi Zanzibar kuwaita na kuwahoji viongozi wa CUF wakidaiwa kutoa kauli za uchochezi haivumiliki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles