28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif aibukia polisi

Na WAANDISHI WETU-Z’BAR/DAR

MSHAURI Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad na Mwenyekiti wa Kamati ya Itikadi, Uenezi na Mawasiliano na Umma wa chama hicho, Salim Bimani, wameitikia wito wa polisi na kuachiwa kwa dhamana.

Hatua hiyo inatokana na wito uliolewa juzi na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Visiwani Zanzibar, likiwataka viongozi hao kufika Kituo cha Polisi Wilaya ya Wete kwa mahojiano.

Barua ya wito huo iliyosainiwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kaskazini Pemba, Deusdedit Kasindo, ambayo ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii, iliwataka viongozi hao wa ACT Wazalendo, kufika katika kituo hicho kwa kuwa kuna mambo yanayowahusu na yanahitaji kupatiwa ufumbuzi.

Kutokana na wito huo, jana Maalim Seif na Bimani walifika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) Mkoa wa Kaskazini Pemba na kuachiwa kwa dhamana baada ya kuhojiwa kwa saa kadhaa.

Baada ya kuachiwa kwa dhamana, Maalim Seif na mwenzake walipokewa na mamia ya wanachama na wananchi waliopiga kambi nje ya Kituo cha Polisi cha Mkoa wa Kaskazini Pemba wakati wote wa mahojiano.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano na Umma wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu alisema katika mahojiano hayo, viongozi hao walidaiwa kufanya mkutano wa hadhara bila kibali cha polisi Desemba 9, mwaka jana katika Jimbo la Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Hata hivyo, Shaibu alisema kuwa siku hiyo viongozi hao hawakufanya mkutano wa hadhara bali kikao cha ndani kupitia ziara ya kukusanya maoni ya wananchi kuandaa ilani ya Uchaguzi Mkuu.

Katika taarifa yake kwa vyombo habari, Shaibu alisema chama hicho kinaliasa Jeshi la Polisi kutotumika kisiasa.

“Mathalani, wakati shughuli halali za ACT Wazalendo zikihujumiwa na viongozi wake kubughudhiwa na Jeshi la Polisi kupitia mahojiano yasiyo na msingi, kuelekea maadhimisho ya miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar, vijana wa UVCCM wengi wakikusanywa kutoka Tanzania Bara, walifanya maandamano Zanzibar kwa siku nane mfululizo bila kubughudhiwa na polisi.

“Vijana hao walifikia hatua ya kushusha bendera kwenye matawi ya ACT Wazalendo na licha ya matukio hayo kuripotiwa polisi, hakuna hatua iliyochukuliwa.

“Tunalikumbusha Jeshi la Polisi kuwa shughuli za vyama vya siasa zipo kwa mujibu wa sheria. Ni muhimu kwa jeshi hilo kujiendesha kwa weledi na haki badala ya kutumika kisiasa kuhujumu shughuli za vyama vya upinzani na kubariki shughuli za CCM pekee,” alisema Shaibu.

POLISI NA DPP

Alipoulizwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Juma Sadi, alisema wao walipewa maelekezo na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na kwamba tayari wamekamilisha kazi yao na wamerudisha jalada kwake.

“Ni kweli tumewahoji leo (jana) saa tatu na sababu kubwa ni kuhusu kufanya mkutano wa hadhara bila kibali cha polisi Desemba 9, mwaka jana na ikizingatiwa mikutano imepigwa marufuku.

“Baada ya kuhojiwa wameachiwa kwa dhamana na jalada tumerudisha kwa DPP,” alisema Kamanda Sadi.

AGIZO LA MASAUNI

Desemba 12, mwaka jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alimwagiza Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kuwaondoa makamanda wawili wa polisi kisiwani Pemba kwa kushindwa kuzuia mikutano ya viongozi hao wa ACT Wazalendo.

Alisema kwa muda mrefu Kisiwa cha Pemba kimekuwa na matukio yasiyoridhisha jambo linaloashiria kuwa wameshindwa kazi.

Makamanda hao ni Hassan Nassir Ally wa Mkoa wa Kusini Pemba na Sheikhan Mohamed Sheikhan wa Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Akitoa mfano wa matukio hayo, Masauni alisema Maalim Seif anafanya mikutano kila kona huku ikijulikana kuwa imezuiwa.

Alisema sababu nyingine ni kutojengwa nyumba za polisi kisiwani humo licha ya Serikali kutoa maagizo.

KAULI YA MAALIM SEIF

Hata hivyo agizo hilo lilimwibua tena Maalim Seif ambaye alihoji sababu za Masauni kushangaa polisi kutozuia mikutano anayoifanya kisiwani Pemba.

Maalim Seif alisema kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini kisiwani Pemba, Sheikhan alisema uchunguzi unaonyesha hakuna kosa lililofanyika.

Alisema amewahoji viongozi wa ACT Wazalendo na kuona walifanya mikutano yao bila ya kuvunja sheria.

Maalim Seif alitoa kauli hiyo baada ya agizo la Masauni, kwa IGP Sirro kumwondoa na kumshusha cheo Sheikhan na Kamanda wa Mkoa wa Kusini, Ally.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles