25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Maalim Seif aanza kazi ACT Wazalendo na hoja tano

LEONARD MANG’OHA – DAR ES SALAAM      

MWENYEKITI mpya wa Chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, ameanza kazi na kutoa maazimio matano yanayohusu uendeshaji wa chama hicho na hatima ya kisiasa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Maalim Seif alisema kuwa mkutano uliofanyika mwishoni mwa wiki pamoja na mambo mengine, uliazimia kufanya maboresho ya katiba ya chama hicho ili kuongeza ufanisi na kuimarisha chama.

Alisema kuwa maboresho hayo pia yanalenga kutekeleza matakwa ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 2019 ambayo pamoja na mambo mengine, inavitaka vyama vya siasa kurekebisha katiba zake ili kuendana na sheria hiyo.

“Maboresho ya Katiba ya ACT Wazalendo, pamoja na mambo mengine yamezingatia usawa wa kijinsia na uwiano wa pande mbili za Muungano,” alisema Maalim Seif.

Maalim Seif ambaye kabla ya uchaguzi huo alikuwa Mshauri Mkuu wa ACT Wazalendo, alisema kuwa mkutano huo pia ulipitia na kupitisha hesabu za chama kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita (2015-2020) na kusisitiza chama hicho kuendeleza utamaduni wake wa uwazi katika usimamizi na matumizi ya fedha za chama.

“Halmashauri Kuu iliwachagua pia wajumbe wa Halmashauri Kuu, chombo cha pili kwa ukubwa baada ya Mkutano Mkuu.

“Ni jambo linalotia moyo kuwa kati ya wajumbe 15 wa Halmashauri Kuu waliochaguliwa, wanane ni wanawake ambao ni sawa na asilimia 53.

“Hata kwa wajumbe wa Kamati Kuu ambao jana wamechaguliwa na Halmashauri Kuu, kati ya wajumbe wanane, wajumbe wanne ni wanawake sawa na asilimia 50.

“Bodi ya wadhamini ya chama chetu, ambacho ndicho chombo kikuu cha kusimamia fedha za chama, kina uwakilishi mkubwa wa wanawake kuliko wanaume. Kati ya wajumbe tisa, watano ni wanawake sawa na asilimia 55,” alisema Maalim Seif.

Alisema kuwa ACT Wazalendo imethibitisha kuwa ni chama kinachojali usawa wa kijinsia kwa vitendo kwa kuwachagua na kuwateua wanawake kwenye vyombo muhimu vya kimaamuzi na nafasi mbalimbali za kimkakati.

“Vijana pia wamepata nafasi ya kipekee kwenye nafasi na vyombo mbalimbali vya kimaamuzi.

“ACT Wazalendo tunaamini kwamba vijana baada ya kupata malezi ya kiuongozi, wanastahili kuaminiwa kwa kupewa nafasi za kuonyesha vipaji vyao,” alisema Maalim Seif.

Katika azimio la nne, alisema kuwa mkutano mkuu kwa kauli moja umeunga mkono ushirikiano wa chama hicho na vyama vingine vya siasa katika uchaguzi katika kuilinda na kuipigania demokrasia nchini.

Maalim Seif alisema mkutano huo umeazimia chama hicho kishirikiane na vyama vingine makini vya siasa na makundi mbalimbali ya kijamii kutekeleza Azimio la Zanzibar la Mwaka 2018 ambalo lilisisitiza juu ya kuundwa kwa mshikamano wa makundi mbalimbali ya kijamii katika kupambana na udhalimu, dhulma na udikteta wa CCM.

Kuhusu tume huru ya uchaguzi, alisema kuwa mkutano huo ulisisitiza ulazima wa chama kushirikiana na wadau wengine wa demokrasia kuipigania.

“Licha ya changamoto zilizopo katika mfumo mzima wa kusimamia chaguzi zetu, mkutano mkuu uliweka bayana kuwa chama hakitasusia uchaguzi kwa sababu kwetu huu ni uchaguzi muhimu.

“Kwa upande wa Zanzibar, ni dhahiri kuwa CCM imeshafahamu kuwa haiwezi kushinda uchaguzi. ACT Wazalendo tumejipanga na kujizatiti kuhakikisha kuwa tunalinda ushindi wetu kwa gharama yoyote,” alisema Maalim Seif.

Kwa upande wa Tanzania Bara, alisema kuwa chama hicho kimejipanga kuhakikisha kinashinda viti vingi vya udiwani na ubunge, kuongoza halmashauri na kushirikiana na vyama vingine makini vya upinzani kuhakikisha CCM inaondoka madarakani.

Katika uchaguzi huo, wajumbe wa Mkutano Mkuu waliwachagua Zitto Kabwe kuwa Kiongozi wa chama, Maalim Seif (Mwenyekiti), Dorothy Semu (Makamu Mwenyekiti Bara), Juma Duni Haji (Makamu Mwenyekiti Zanzibar) huku nafasi ya Katibu Mkuu akichaguliwa mwanasiasa kijana Ado Shaibu na manaibu wake Nassor Mazrui (Zanzibar) na Joran Bashange (Bara).

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,522FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles