27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Maajabu ya kisiwa kidogo cha uvuvi Migingo

                 JOSEPH HIZA NA MTANDAO

KWA wasomaji wengi watakuwa wamekisikia Kisiwa hiki cha Migingo chenye msongamano mkubwa wa vibanda na watu kuliko vyote duniani.

Kinafahamika pia kama Bugingo au Ugingo kikiwa na ukubwa wa eneo la mita mraba 2,000 sawa na nusu ya uwanja wa mpira wa miguu na wakazi 500 huishi humo.

Kinapakana na mataifa ya Uganda na Kenya ndani ya Ziwa Victoria, ambalo ni kubwa kuliko yote barani Afrika.

Ni nyumbani kwa baa nne, duka moja la dawa, sehemu ya kutengeneza nywele ‘hair salon,’ na madanguro zaidi ya 10 ambapo makahaba wanakadiriwa kufikia 70.

Pamoja na udogo wake, kimekuwa chanzo cha mizozo, vita ndogo na migogoro baina ya Serikali za Kenya na Uganda.

Askari baina yao wameshuhudia wakioneshana ubabe na hata damu kumwagika, wakishindana kusimika bendera za nchi zao.

Siri ya migogoro hiyo ni uwapo wa utajiri mkubwa wa samaki aina ya sangara kiasi kwamba huwapatia utajiri wa haraka wengi.

Awali wavuvi baina ya mataifa hayo mawili waliishi kwa amani kabla ya kuibuka vitendo vya kijambazi na kiharamia vikihusisha wizi wa mamilioni ya fedha, boti, mashine na kadhalika.

Maharamia hawa walitoka pembe nzima ya Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania na kuwafanya wavuvi kuziomba serikali zao utatuzi wa kero hizo.

Serikali ya Uganda ikawa ya kwanza kuingilia kati kusikiliza kilio chao bila kujali uraia wa wavuvi waliopo.

Lakini wakishangazwa na utajiri mkubwa wa ‘chee’ uliopo hapo,  askari wa Uganda wakanogewa na kuitana kujazana kwa wingi wakiweka kambi na baadaye kusimika bendera yao.

Licha ya hayo wavuvi wa Kenya hawakujali sana hilo, wao kwao muhimu kuvua na kuuza si kujiuliza umiliki wa kisiwa hicho.

Lakini ikumbukwe biashara ya sangara ni kubwa mno ikitengeneza kipato cha mamia kwa mamilioni ya doa si kwa wafanyabiashara tu bali pia serikali za Kenya, Uganda na Tanzania.

Soko kuu la dhahabu hiyo ya baharini inayosafirishwa kila siku ni Ulaya, Asia na Mashariki ya Kati.

Hivyo basi, askari hawa wa Uganda wakaanza kudai na kutoza vibali ghali kuingia eneo hilo, wale wasio navyo wakiwamo wavuvi wakakamatwa.

Wakenya ndipo wakashtuka na kuanza kulalamika, Serikali ya Kenya ikajibu kwa kudai kisiwa ni chake na hivyo Uganda ikaenda mbali zaidi kutuma jeshi la majini na kuionya Kenya.

Licha ya hayo, wavuvi waliendelea kuishi baina yao kidugu bila umiliki baina ya Uganda na Kenya, wakitaniana kila mtu kuvutia umiliki upande wake, lakini mwishowe wakisema ‘lengo letu tuvue na kuuza’ suala la umiliki lisituumize.’

Wakati wa mchana wavuvi hurusha baharini nyavu zao ili kunasa sangara.

Usiku unapoingia kisiwani hapo, giza kuficha tofauti zao na kufichua kundi la watu linalowaleta pamoja kwa mapenzi, mahaba, mapenzi na uongo ambao unapita mipaka ya kikabila au kieneo.

Nyakati hizo za usiku makahaba kutoka Kenya, Tanzania na Uganda humiminika na wafanyakazi baada ngumu za kutwa baharini hunywa katika baa zilizotengenezwa kwa mabati kabla ya kwenda kujifurahisha na makahaba hao.

Lakini katika miaka ya karibuni hali hiyo ya udugu baina ya mataifa imebadilika. Kuna uadui baina ya wavuvi wa mataifa haya mawili kiasi cha kutochangamana tena katika kisiwa hicho wakati ‘vita ndogo kabisa Afrika’ ikiunguruma.

Hata wanawake wanaowachukua sasa ni wa utaifa wao tu au lingine tofauti na hayo mawili. Kila kitu ni mipaka kutokana na mizozo kuzidi kuongeza chuki na uadui.

Lakini pia sehemu kubwa ya wavuvu hutumia fedha zao kwa wingi na fujo kisiwani humo nyingi zikipotelea zaidi kwenye pombe na ngono.

Na wengi wao hawana mafunzo au utaalamu na wakati waendapo kazini ziwani humo. Huenda wakiwa wamelewa na kwa sababu hiyo ajali za boti au boti kukosa vifaa vya usalama ni jambo la kawaida.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles